2 Mambo 26

2 Mambo 26

Uzia anafanikiwa katika ufalme wake.

(Taz. 2 Fal. 14:21,22; 15:1-7.)

1Watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia aliyekuwa mwenye miaka 16, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Amasia.

2Yeye akaujenga Eloti, akaurudisha kwao Wayuda, mfalme alipokuwa amelala na baba zake.

3Uzia alikuwa mwenye miaka 16 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 52 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Yekolia wa Yerusalemu.

4Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, kama yote, baba yake Amasia aliyoyafanya.[#2 Mambo 25:2.]

5Akawa akimtafuta Mungu siku, alizokuwapo Zakaria aliyemfundisha maana ya kumtazamia Mungu; nazo siku zile, alipomtafuta Bwana, Mungu akayaendesha mambo yake.

6Akatoka, akapigana na Wafilisti, akalivunja boma la Gati na boma la Yabune na boma la Asdodi, akajenga miji kwao Waasdodi nako kwao Wafilisti.

7Mungu akamsaidia kuwashinda Wafilisti na Waarabu waliokaa Guri-Baali na Wameuni.

8Ndipo, Waamoni walipompa Uzia mahongo, jina lake likafika hata Misri, kwani alijipatia nguvu zaidi.

9Kisha Uzia akajenga minara huko Yerusalemu penye lango la pembeni napo penye lango la bondeni napo, boma lilipojipinda, akaitia nguvu.

10Hata nyikani akajenga minara, akachimba visima vingi, kwani alikuwa na makundi mengi katika nchi ya tambarare, nako kwenye mbuga; akawa na wakulima na watunza mizabibu milimani na mashambani kwenye wiva, kwani alipenda kazi za ulimaji.

11Tena Uzia alikuwa na vikosi vya wapiga vita waliotoka kupigana, kila kimoja chenye hesabu ya watu waliokaguliwa na mwandishi Yieli na mwenye amri Masea kwa msaada wa Hanania aliyekuwa mkuu wa mfalme;

12hesabu yote ya wakuu wa milango ya mafundi wa vita ilikuwa 2600.

13Mikononi mwao vilikuwa vikosi vya askari, watu 307500 waliopiga vita kwa nguvu nyingi, wamsaidie mfalme kushinda adui.

14Hivyo vikosi vyote Uzia akavipatia ngao na mikuki na kofia ngumu na shati za vyuma na pindi na mawe ya makombeo.

15Akatengeneza mle Yerusalemu makombeo makubwa, akitumia mafundi wenye mawazo ya kutunga matengenezo kama hayo, akayaweka juu ya minara, hata pembenipembeni ya kutupia mishale na mawe makubwa; kwa hiyo jina lake likafika hata katika nchi za mbali, kwani vikastaajabisha, alivyosaidiwa, akaendelea kupata nguvu.

Uzia anapata ukoma kwa majivuno yake.

16Alipopata nguvu, moyo wake ukajikuza, afanye yasiyofanywa, akamvunjia Bwana Mungu wake maagano akiingia Jumbani mwa Bwana kumvukizia mezani pa kuvukizia.[#2 Mambo 25:19.]

17Mtambikaji Azaria akamfuata pamoja na watambikaji wa Bwana 80 waliokuwa wenye nguvu.

18Wakajipanga, wamkinge mfalme Uzia wakimwambia: Siyo kazi yako, Uzia, kumvukizia Bwana, ila ni yao watambikaji walio wana wa Haroni, wametakaswa, wavukize. Toka Patakatifu, kwani umeyavunja maagano, kwani hutajipatia macheo kwa Bwana Mungu.[#4 Mose 18:7.]

19Ndipo, Uzia alipochafuka, nacho kivukizio cha kuvukizia kilikuwa mkononi mwake; alipowatolea watambikaji machafuko yake, ukoma ukamtoka pajini pake usoni pa watambikaji mle Nyumbani mwa Bwana kando ya meza ya kuvukizia.

20Mtambikaji mkuu Azaria na watambikaji wote walipomgeukia, mara wakamwona kuwa na ukoma pajini; ndipo, walipomfukuza huko upesiupesi, naye akajihimiza kutoka, kwa kuwa Bwana amempiga.

21Mfalme Uzia akawa mwenye ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa akiwa mwenye ukoma katika nyumba ya wagonjwa waliotengwa, kwani alikatazwa kuiingia Nyumba ya Bwana, mwanawe Yotamu akawa mkuu nyumbani mwa mfalme, akawaamua watu wa nchi hii.[#4 Mose 5:2.]

Kufa kwake Uzia.

22Mambo mengine ya Uzia, ya mwanzo na ya mwisho, aliyaandika mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi.[#Yes. 1:1; 6:1.]

23Uzia akaja kulala na baba zake, wakamzika kwa baba zake porini kwenye makaburi ya wafalme, kwani walisema: Huyu ni mkoma. Kisha mwanawe Yotamu akawa mfalme mahali pake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania