2 Mambo 29

2 Mambo 29

Hizikia anaitengeneza tena Nyumba ya Mungu.

1Hizikia akaupata ufalme alipokuwa mwenye miaka 25, akawa mfalme miaka 29 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Abia, binti Zakaria.[#2 Fal. 18:1-3.]

2Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, aliyoyafanya baba yake Dawidi.

3Katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake katika mwezi wa kwanza akaifungua milango ya Nyumba ya Bwana, akaitengeneza vema.

4Kisha akaleta watambikaji na Walawi, akawakusanya uwanjani upande wa maawioni kwa jua.

5Akawaambia: Nisikieni, ninyi Walawi! Sasa jieueni, mpate kuieua nayo Nyumba ya Bwana Mungu wa baba zenu na kuutoa uchafu hapa Patakatifu!

6Kwani baba zetu wameyavunja maagano, wakayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wetu, wakamwacha na kuzigeuza nyuso zao, zisilitazame Kao la Bwana, wakalielekezea migongo.

7Wakaifunga nayo milango ya ukumbi, wakazizima taa zake, hawakumvukizia Mungu wa Isiraeli mavukizo, wala hawakumtolea ng'ombe za tambiko hapa Patakatifu.[#2 Mambo 28:24.]

8Kwa hiyo makali ya Bwana yakaikalia nchi ya Yuda na Yerusalemu, akawatoa, watupwe huko na huko, wastukiwe kabisa na kuzomewa, kama ninyi mnavyoviona wenyewe kwa macho yenu.

9Tazameni! Baba zetu waliuawa kwa panga, nao wana wetu wa kiume na wa kike pamoja na wanawake wetu wakatekwa kwa sababu hiyo.[#2 Mambo 28:5-8.]

10Sasa mimi nimejipa moyo, nifanye agano na Bwana Mungu wa Isiraeli, makali yake yawakayo moto yatuondokee.

11Sasa ninyi wanangu, msizurure! Kwani ninyi Bwana aliwachagua, msimame mbele yake na kumtumikia, mwe watumishi wake na wavukizaji wake.

12Ndipo, walipoinuka Walawi: Mahati, mwana wa Amasai, na Yoeli, mwana wa Azaria, walio wana wa Kehati; nao waliokuwa wana wa Merari: Kisi, mwana wa Abudi, na Azaria, mwana wa Yehaleleli, nao waliokuwa wana wa Gersoni: Yoa, mwana wa Zima, na Edeni, mwana wa Yoa;

13nao waliokuwa wana wa Elisafani: Simuri na Yieli; nao waliokuwa wana wa Asafu: Zakaria na Matania;

14nao waliokuwa wana wa Hemani: Yehieli na Simei; nao waliokuwa wana wa Yedutuni: Semaya na Uzieli.

15Wakawakusanya ndugu zao, wakajieua; kisha wakaja kwa agizo la mfalme kuitakasa Nyumba ya Bwana, kama Bwana alivyosema.

16Watambikaji wakaingia Nyumbani mwa Bwana ndani kuitakasa na kuyatoa machafu yote, waliyoyaona Jumbani mwa Bwana, wakayapeleka uani penye Nyumba ya Bwana; ndiko, Walawi walikoyachukua, wayapeleke nje mtoni kwa Kidoroni.

17Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakaanza kuitakasa, siku ya nane ya huo mwezi wakafika penye ukumbi wa Bwana, wakaitakasa Nyumba ya Bwana tena siku nane, wakaimaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza.

18Kisha wakaingia nyumbani kwa mfalme Hizikia, wakamwamiba: Tumeitakasa Nyumba yote ya Bwana, hata meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote,, hata meza ya mikate, aliyowekewa Bwana, na vyombo vyake vyote.

19Navyo vyombo vyote, mfalme Ahazi alivyovichafua katika ufalme wake, alipoyavunja maagano, tumevitengeneza na kuvitakasa, utaviona, viko mbele ya meza ya kumtambikia Bwana.

Nyumba ya Mungu inaeuliwa.

20Ndipo, mfalme Hizikia alipoamka na mapema, akawakusanya wakuu wa mji, akapanda kwenda Nyumbani kwa Bwana.

21Wakaleta madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo na wana kondoo saba na madume saba ya mbuzi kuwa ng'ombe za tambiko za weuo kwa ajili ya ufalme na kwa ajili ya Patakatifu na kwa ajili ya Wayuda. Akawaambia watambikaji, wana wa Haroni, wawatoe kuwa ng'ombe za tambiko hapo pa kumtambikia Bwana.

22Ndipo, walipowachinja hao ng'ombe, nao watambikaji wakazichukua damu zao, wakazinyunyizia meza ya kutambikia; wakawachinja nao madume ya kondoo, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya kutambikia, wakawachinja nao wana kondoo, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya kutambikia.

23Kisha wakawapeleka madume ya mbuzi ya weuo mbele ya mfalme na mbele ya huo mkutano, wakawabandikia mikono yao.

24Kisha watambikaji wakawachinja, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya Bwana kuwa mweuo wa kuwapatia Waisiraeli wote upozi, kwani mfalme aliagiza kwa ajili ya Waisiraeli wote kutoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za weuo.

25Naye alikuwa amewasimamisha Walawi penye Nyumba ya Bwana, wakiyashika matoazi na mapango na mazeze, kama Dawidi na Gadi aliyekuwa mchunguzaji wa mfalme na mfumbuaji Natani walivyoviagiza; kwani agizo hilo lilitoka kwa Bwana, likatokea vinywani mwa wafumbuaji wake.[#1 Mambo 25:1.]

26Kwa hiyo Walawi wakasimama na kuvishika vyombo vya Dawidi, nao watambikaji wakashika matarumbeta.

27Hizikia alipoagiza kuziteketeza ng'ombe za tambiko mezani pa kutambikia, papo hapo tambiko lilipanzia, ndipo, wimbo wa Bwana ulipoanzia pamoja na matarumbeta yaliyoongozwa na vyombo vya Dawidi, mfalme wa Waisiraeli.

28Mkutano wote pia ukamwangukia Bwana, wimbo ulipoimbwa, nayo matarumbeta yalipolia; yote yakawa hivyo, hata ng'ombe za tambiko zikaisha kuteketezwa.

29Walipokwisha kuziteketeza hizo ng'ombe za tambiko, wakapiga magoti, yeye mfalme nao wote waliokuwako naye, wakamwangukia Bwana.

30Kisha mfalme Hizikia na wakuu wakawaambia Walawi, wamtukuze Bwana na kuyaimba maneno ya Dawidi na ya mchunguzaji Asafu. Ndipo, walipomtukuza kwa furaha, kisha wakainama, wakamwangukia.[#2 Mambo 23:18.]

31Kisha Hizikia akawaitikia akisema: Sasa mmeyajaza magao yenu kumtumikia Bwana, basi, karibuni, mlete huku kwenye Nyumba ya Bwana ng'ombe za tambiko na vipaji vya shukrani! Ndipo, watu wa huo mkutano walipoleta ng'ombe za tambiko na vipaji vya shukrani, kila mtu akatoa ng'ombe za tambiko, kama moyo ulivyopenda.

32Hesabu ya ng'ombe za tambiko, watu wa huo mkutano walizozitoa, ikawa ng'ombe 70, madume ya kondoo 100, wana kondoo 200; hawa wote walikuwa wa kumteketezea Bwana.

33Tena za matambiko mengine wakatolewa ng'ombe 600 na kondoo na mbuzi 3000.

34Watambikaji tu walikuwa wachache, hawakuweza kuwachuna ng'ombe wote wa kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia, mpaka kazi hii ikaisha, tena mpaka watambikaji wakajieua, kwani Walawi walikuwa wenye mioyo iliyojihimiza kujieua kuliko yao watambikaji.[#2 Mambo 30:3,16-17.]

35Nao ng'ombe wa kuteketezwa nzima walikuwa wengi, vilevile vipande vyenye mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukurani na vinywaji vya tambiko vilivyopasa kila ng'ombe ya tambiko. Ndivyo, utumishi wa Nyumbani mwa Bwana ulivyotengenezwa tena.[#3 Mose 3:3,16-17; 4 Mose 15:5,7,10.]

36Hizikia na watu wote wakafurahi kwa hayo, Mungu aliyowatengenezea watu, kwani jambo hili lilifanyika kwa upesi sana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania