2 Mambo 3

2 Mambo 3

Kuijenga Nyumba ya Mungu.

(Taz. 1 Fal. 6; 7:15-22.)

1Salomo akaanza kuijenga nyumba ya Bwana Yerusalemu katika mlima wa Moriya, Bwana alikomtokea baba yake Dawidi, mahali pale, Dawidi alipopaagiza penye kupuria ngano pa Myebusi Ornani.[#1 Mose 22:2; 1 Mambo 21:18-26.]

2Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa ufalme wake.

3Nayo misingi, Salomo aliyoiweka ya kuijenga nyumba ya Mungu, ni hii: urefu wa kwenda mbele kwa kipimo cha kale ulikuwa mikono 60, nao upana wake ulikuwa mikono 20.

4Ukumbi uliokuwa mbele ya nyumba ulikuwa mikono 20 kwa kuupatanisha na upana wa nyumba, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono 120, ndani akazifunika kuta zake kwa mabati ya dhahabu tupu.

5Nyumba kubwa akaipigilia kutani mbao za mivinje, nazo akazivika mabati ya dhahabu nzuri, humo namo akachora mitende na mikufu.

6Akaipamba hiyo nyumba kwa vito vyenye kima, ipate utukufu; zile dhahabu zilikuwa dhahabu za Parawaimu.

7Boriti na vizingiti na kuta zake na milango yake ya humu nyumbani akaivika mabati ya dhahabu, napo kutani akachora Makerubi.

8Kisha akapatengeneza Patakatifu Penyewe, urefu wake ulikuwa mikono 20 kwa kuupatanisha na upana wa nyumba, upana wake nao ulikuwa mikono 20, akapavika mabati ya dhahabu nzuri za vipande vya dhahabu 600, ndio frasila 1800.

9Misumari ilipopimiwa uzito wa dhahabu yao, ukawa sekeli za dhahabu 50, ndio ratli mbili. Navyo vyumba vya juu akavivika dhahabu.

10Kisha mle Patakatifu Penyewe akatengeneza Makerubi mawili yaliyochongwa na mafundi, nayo akayafunikiza dhahabu.

11Mabawa ya haya Makerubi urefu wao ulikuwa mikono 20: bawa la moja lenye mikono mitano liligusa ukuta wa nyumba, nalo la pili lenye mikono mitano liligusa bawa la Kerubi la pili;

12vilevile bawa la Kerubi la pili lenye mikono mitano liligusa ukuta wa nyumba, nalo bawa la pili lenye mikono mitano lilishikamana na bawa lake lile Kerubi jingine.

13Hivyo, haya mabawa ya Makerubi yalivyokuwa yamekunjuka, yalikuwa yenye mikono 20, nayo yalisimama kwa miguu yao, nazo nyuso zao zilielekea nyumbani.

14Akatungika pazia la nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na za rangi na za bafta, namo akashonea mifano ya Makerubi.[#2 Mose 26:31.]

15Mbele ya nyumba akaweka nguzo mbili zenye urefu wa mikono 35, nacho kichwa kilichokuwa juu ya kila moja kilikuwa chenye urefu wa mikono mitano.

16Akatengeneza hata mikufu kuwa ukingo wa chini wa hivyo vichwa, akaitia juu ya hizo nguzo; kisha akatengeneza komamanga 100, akaziangika pale penye mikufu.

17Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya jumba hili, moja kuumeni, moja kushotoni; ya kuumeni akaiita Yakini (Hushikiza), ya kushotoni Boazi (Nguvu imo).

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania