2 Mambo 31

2 Mambo 31

Matambiko ya kimizimu yanaondolewa.

1Walipokwisha kuyamaliza hayo yote, Waisiraeli wote waliokuwako wakatoka kwenda zao katika miji ya Yuda, wakazivunja nguzo za kutambikia, wakaikatakata nayo miti ya Ashera, wakavibomoa vijumba vya kutambikia vilimani pamoja na meza zao za kutambikia katika nchi zote za Yuda na za Benyamini na za Efuraimu na za Manase, mpaka wakavitowesha kabisa hivyo vyote, kisha wana wote wa Isiraeli wakarudi kila mtu mahali palipokuwamali yake katika miji yao.[#5 Mose 7:5; 2 Fal. 18:4.]

Matengenezo mapya ya mambo ya watambikaji na ya Walawi.

2Kisha Hizikia akaweka kazi za zamu za watambikaji na za Walawi zizipasazo zamu zao, kila mtu akawa na kazi yake ya utumishi wake, watambikaji na Walawi: kuteketeza ng'ombe za tambiko na kutengeneza ng'ombe za tambiko za shukrani na kutumikia malangoni kwa matuo yake Bwana na kumshukuru na kumshangilia.

3Akayaweka nayo yampasayo mfalme kuyatoa katika mali zake kuwa ng'ombe za tambiko za asubuhi na za jioni na za matambiko ya siku za mapumziko na ya miandamo ya mwezi na ya sikukuu, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Bwana.[#4 Mose 28:29.]

4Tena akawaagiza watu waliokaa Yerusalemu kuwapa watambikaji na Walawi yawapasayo, wapate kuyashika Maonyo ya Bwana.

5Agizo hili lilipoenea, wana wa Isiraeli wengi wakaleta malimbuko ya ngano na ya mvinyo na ya mafuta na ya asali na ya mazao yote ya mashamba, wakayaleta nayo mafungu ya kumi ya mali zote, yakawa mengi.[#2 Mose 23:19; 5 Mose 14:22-23.]

6Nao wana wa Isiraeli na wa Yuda waliokaa katika miji ya Yuda wakaleta nayo mafungu ya kumi ya ng'ombe na ya mbuzi na ya kondoo nayo mafungu ya kumi ya vipaji vitakatifu vilivyotolewa kuwa mali za Bwana Mungu wao, wakaviweka machungu machungu.

7Katika mwezi wa tatu walianza kuyaweka hayo machungu, wakayamaliza katika mwezi wa tisa.

8Ndipo, Hizikia na wakuu walipokuja kuyatazama hayo machungu, wakamtukuza Bwana nao Waisiraeli walio ukoo wake.

9Hizikia alipoulizana na watambikaji na Walawi maana ya hayo machungu,

10Azaria aliyekuwa mtambikaji mkuu wa mlango wa Sadoki akamjibu, akamwambia: Tangu hapo, walipoanza kuyaleta haya matoleo Nyumbani mwa Bwana, tumekula na kushiba, nayo haya mengi ndiyo yaliyosalia, kwani Bwana amewabariki walio ukoo wake, kwa hiyo vimesalia hivyo vipaji vingi mno.

11Ndipo, Hizikia alipoagiza, watengeneze vyumba katika Nyumba ya Bwana: walipokwisha kuvitengeneza,

12wao kwa kuwa welekevu wakaingiza humo yale matoleo na mafungu ya kumi na vipaji vitakatifu vyote pia, Mlawi Konania akawekwa kuyaangalia, naye ndugu yake Simei akawa wa pili.

13Nao Yehieli na Azazia na Nahati na Asaheli na Yerimoti na Yozabadi na Elieli na Isimakia na Mahati na Benaya wakawekwa kuwa wasimamizi kumsaidia Konania na ndugu yake Simei kwa agizo lake mfalme Hizikia na Azaria aliyekuwa mwenye amri Nyumbani mwa Mungu.

14Tena Mlawi Kore, mwana wa Imuna, aliyelilinda lango lililoelekea maawioni kwa jua akawekwa kuviangalia vipaji vya Mungu, watu walivyovitoa kwa kupenda kwao wenyewe, agawe yaliyo matoleo ya Bwana nayo yaliyo matakatifu yenyewe.

15Waliomsaidia katika miji ya watambikaji ni Edeni na Minyamini na Yesua na Semaya na Amaria na Sekania, wawagawie kwa kweli ndugu zao yawapasayo kwa zamu zao, mkubwa kwa mdogo,

16kuliko wale wanawaume walioandikwa katika kitabu chao walio wa miaka mitatu na zaidi; nao hawa ndio wote waingiao Nyumbani mwa Bwana kwa mambo ya kila siku moja kufanya kazi za utumishi wao ziwapasazo kuziangalia kwa zamu zao.

17Katika kile kitabu cha udugu wa watambikaji imeandikwa milango ya baba zao, nacho cha Walawi kimeandikwa walio wenye miaka ishirini na zaidi kwa kazi zao ziwapasazo kuziangalia kwa zamu zao.

18Humo katika kitabu cha udugu wakaandikwa nao watoto wao wadogo wote na wake zao na wana wao wa kiume na wa kike wa mkutano wote pia, kwani kwa kuwa welekevu walijitakasa kuwa watakatifu kweli.

19Nao wana wa Haroni waliokuwa watambikaji mashambani kwenye mitaa ya miji yao wakapata watu katika kila mji mmoja walioandikwa majina yao, wawagawie yawapasayo, kila mume mmoja fungu lake miongoni mwa watambikaji, namo mwa Walawi wote walioandikwa katika kitabu cha udugu.

20Ndivyo, Hizikia alivyofanya katika nchi yote ya Yuda, akayafanya yaliyokuwa mema na manyofu na ya kweli machoni pake Bwana Mungu wake.

21Nazo kazi zote, alizozianza za kuitumikia Nyumba ya Mungu na za kuyafuata Maonyo na maagizo, kwa hivyo, alivyomtafuta Mungu, akazifanya kwa moyo wake wote, akafanikiwa.[#Sh. 1:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania