The chat will start when you send the first message.
1Hayo yalipokwisha kufanyika kwa welekevu, akaja Saniheribu, mfalme wa Asuri; akaingia katika nchi ya Yuda, akapiga makambi kwenye miji yenye maboma, akataka kujipenyeza humo, iwe yake.[#2 Mambo 31:20.]
2Hizikia alipoona, ya kuwa Saniheribu amekuja na kuuelekeza uso wake kuja kupiga vita Yerusalemu,
3akafanya shauri na wakuu wake na mafundi wake wa vita kuyaziba maji ya chemchemi zilizoko nje ya mji, nao wakamsaidia.
4Wakakusanyika watu wengi, wakaziziba chemchemi zote, hata kijito kilichopita katikati ya nchi hiyo wakisema: Mbona tuache, wafalme wa Asuri wakifika waone maji mengi?
5Akakaza kuutengeneza ukuta wote wa boma na kuujenga tena hapo, ulipobomoka, hata minara akaipandisha kwenda juu zaidi, nao ukuta wa pili wa nje akaujenga tena, hata ngome ya mji wa Dawidi akaitia nguvu, akatengeneza mata na ngao nyingi.[#2 Mambo 25:23.]
6Nao watu akawawekea wakuu wa vita, akawakusanya kwake uwanjani penye lango la mji, akawashikiza mioyo akiwaambia:[#2 Mambo 30:22.]
7Jipeni mioyo, mpate nguvu! Msiogope, wala msiingiwe na vituko mkimwona mfalme wa Asuri nao wale watu wengi mno, alio nao wote! Kwani walio upande wetu ndio wengi kuliko wao walio upande wake.[#2 Fal. 6:16.]
8Yeye anayo mikono yenye nyama, lakini sisi tunaye Bwana Mungu wetu kuwa msaada wetu kwa kutupigania mapigano yetu. Nao watu wakashikizwa na haya maneno ya Hizikia, mfalme wa Yuda.[#Yer. 17:5,7.]
9Baada ya hayo Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipokuwa Lakisi pamoja na utukufu wake wote akatuma watumishi wake kwenda Yerusalemu kwa Hizikia, mfalme wa Wayuda, na kwa Wayuda wote waliokuwamo Yerusalemu kuwaambia:
10Hivi ndivyo, anavyosema Saniheribu, mfalme wa Asuri: Ninyi mnaegemea nini mkikaa ngomeni Yerusalemu na kusongwa?
11Je? Siye Hizikia anayewaponza na kuwatoa, mfe kwa njaa na kwa kiu akiwaambia: Bwana Mungu wetu atatuponya mkononi mwa mfalme wa Asuri?
12Huyu Hizikia siye aliyewakataza watu kumtambikia pake pa kutambikia vilimani napo penye meza zake za kutambikia akiwaambia Wayuda na Wayerusalemu kwamba: Sharti mmwangukie mbele ya meza moja tu ya kumtambikia na kumvukizia hapo tu?
13Hamyajui, mimi na baba zangu tuliyoyafanyia makabila yote ya nchi hizo? Je? Miungu yao mataifa ya nchi hizi iliweza kweli kuziponya nchi zao mikononi mwangu?
14Katika miungu yote ya haya mataifa, baba zangu waliyoyatia mwiko wa kuwapo, ulikuwa upi ulioweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu? Naye Mungu wenu atawezaje kuwaponya mkononi mwangu?
15Sasa Hizikia asiwadanganye na kuwaponza ninyi kwa maneno kama hayo! Msimtegemee! Kwani hakuna mungu wo wote wa taifa au ufalme wo wote ulioweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu wala mikononi mwa baba zangu. Sembuse Mungu wenu atawezaje kuwaponya mkononi mwangu?
16Yako na mengine, watumishi wake waliyoyasema ya kumkataa Bwana Mungu na mtumishi wake Hizikia.
17Akaandika nazo barua za kumfyoza Bwana Mungu wa Isiraeli, akisema humo kwamba: Kama miungu ya mataifa ya nchi hizi isivyoweza kuwaponya watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo naye Mungu wa Hizikia hataweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu.
18Nao wa Yerusalemu waliokuwa ukutani juu wakawaambia haya Kiyuda na kuzipaza sana sauti zao, wawaogopeshe na kuwastusha, wapate kuuteka mji huu.
19Mambo ya Mungu wa Yerusalemu wakayawazia kuwa kama mambo ya miungu ya makabila mengine ya nchi hii iliyokuwa kazi za mikono ya watu tu.
20Ndipo, mfalme Hizikia na mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, walipoomba kwa ajili ya hayo na kumlilia Alioko mbinguni.
21Bwana akatuma malaika wake, akaangamiza katika makambi ya mfalme wa Asuri mafundi wa vita wote waliokuwa wenye nguvu na wenye amri na wakuu, naye yeye hakuwa na budi kurudi kwao na kuuinamisha uso chini kwa soni. Alipoingia nyumbani mwa mungu wake, ndipo, wanawe wengine waliozaliwa naye mwenyewe walipomwua kwa upanga.
22Ndivyo, Bwana alivyomwokoa Hizikia na wenyeji wa Yerusalemu mkononi mwa Saniheribu, mfalme wa Wasuri, namo mikononi mwao wote wengine akiwalinda pande zote.
23Watu wengi wakamtolea Bwana vipaji na kuvipeleka Yerusalemu, naye Hizikia, mfalme wa Wayuda, wakampa matunzo, naye tangu hapo akatukuka sana machoni pao wamizimu wote.
24Siku hizo Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu sana; alipomlalamikia Bwana, huyu akasema naye na kumtolea kielekezo.
25Lakini Hizikia hakuyarudisha hayo mema aliyofanyiziwa, kwa kuwa moyo wake ulijikuza. Kwa hiyo makali ya Bwana yakaja kumkalia yeye, hata Wayuda na Wayerusalemu.[#2 Mambo 26:16.]
26Lakini Hizikia kwa hivyo, moyo wake ulivyojikuza, akajinyenyekeza tena yeye pamoja na wenyeji wa Yerusalemu; kwa sababu hii makali ya Bwana hayakuwatokea siku za Hizikia.
27Hizikia akawa mwenye mali na macheo mengi, akajipatia vilimbiko vya fedha na vya dhahabu na vya vito vyenye kima na vya manukato na vya ngao na vya vyombo vyo vyote, alivyovitamani,
28hata mawekeo ya mazao ya ngano na ya mvinyo mbichi na ya mafuta, hata mabanda ya nyama wote wa kufuga na makundi mazizini.
29Akajenga hata miji, kwani alikuwa na mbuzi na kondoo na ng'ombe wengi, kwani Mungu alimpa kupata mali nyingi sana.
30Naye Hizikia ndiye aliyeliziba tokeo la juu la maji ya kijito cha Gihoni na kuyapeleka moja kwa moja, yaushukie mji wa Dawidi upande wa machweoni kwa jua. Ndivyo, Hizikia alivyofanikiwa katika kazi zote.
31Hapo tu, wakuu wa Babeli walipotuma wasemaji kwake wa kuuliza maana ya kielekezo kilichofanyika katika nchi hii, Mungu alimwacha, amjaribu, ayajue yote yaliyokuwa moyoni mwake.[#2 Fal. 20:12-18.]
32Mambo mengine ya Hizikia nayo matendo ya upole wake tunayaona, yameandikwa katika maono ya mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, na katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli.
33Hizikia alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika pa kupandia penye makaburi ya wana wa Dawidi; Wayuda wote na wenyeji wa Yerusalemu wakamheshimu sana, alipokufa. Naye mwanawe Manase akawa mfalme mahali pake.[#2 Mambo 16:14.]