The chat will start when you send the first message.
1Manase alikuwa mwenye miaka 12 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 55 mle Yerusalemu.
2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyafuata matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli.[#5 Mose 18:9.]
3Akavijenga tena vijumba vya kutambikia vilimani, baba yake Hizikia alivyovibomoa, akaweka hata meza za kutambikia Mabaali, akatengeneza navyo vinyago vya Ashera, akaviangukia vikosi vyote vya mbinguni na kuvitumikia.[#2 Fal. 18:4.]
4Namo Nyumbani mwa Bwana akajenga penginepengine pa kutambikia, naye Bwana alisema: Yerusalemu ndimo, Jina langu litakamokaa.[#5 Mose 12:5,11; 1 Fal. 9:3.]
5Katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana akajenga pa kuvitambikia vikosi vyote vya mbinguni.
6Hata wanawe akawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni katika Bonde la Bin-Hinomu; tena akaagulia mawingu, akapiga bao, tena akafanya uchawi, akatumia nao wakweza mizimu na wapunga pepo; akazidi kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, amkasirishe.
7Nacho kinyago cha kuchora, alichokitengeneza, akakiweka katika Nyumba ya Mungu, ambayo Mungu alimwambia Dawidi na mwanawe Salomo: Humu Nyumbani namo Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, nitalikalisha Jina langu kale na kale.
8Sitaiondoa tena miguu ya Waisiraeli katika nchi hii, niliyowawekea baba zenu, wao wakijiangalia tu na kuyafanya yote, niliyowaagiza kinywani mwa Mose kuwa Maonyo na maongozi na maamuzi.
9Lakini Manase akawaponza Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu kufanya mabaya kuliko wamizimu, Bwana aliowaangamiza mbele ya wana wa Isiraeli.
10Bwana akasema na Manase na watu wake, lakini hawakusikiliza.
11Kisha Bwana akawaletea wakuu wa vikosi vya mfalme wa Asuri, wakamkamata Manase kwa vyuma vyenye kulabu, wakamfunga kwa mapingu, wakampeleka Babeli.
12Aliposongeka hivyo akaulalamikia uso wa Bwana Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele ya Mungu wa baba zake.
13Alipomlalamikia hivyo na kumlilia, akayasikia maombo yake, akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo, Manase alipotambua, ya kuwa Bwana ndiye Mungu.[#1 Fal. 18:39.]
14Baada ya hayo akaujenga ukuta wa nje wa mji wa Dawidi ulioko upande wa machweoni kwa jua kulielekea bonde la kijito cha Gihoni mpaka kufika penye lango la Samaki na kuzunguka Ofeli, akaupandisha kwenda juu sana. Tena akaweka wakuu wa vikosi katika miji yote yenye maboma katika nchi ya Yuda.
15Kisha akaiondoa miungu migeni pamoja na kile kinyago Nyumbani mwa Bwana, nazo meza zote za kutambikia, alizozijenga milimani penye Nyumba ya Bwana namo Yerusalemu, akazitupa huko nje ya mji.
16Akaitengeneza tena meza ya kumtambikia Bwana, akachoma juu yake ng'ombe za tambiko za kushukuru na za kusifu, nao Wayuda akawaagiza kumtumikia Bwana Mungu wa Isiraeli.
17Lakini watu hawakuacha kutambika vilimani, lakini huko nako siku zile wakamtambikia Bwana Mungu wao tu.
18Mambo mengine ya Manase na maombo yake, aliyomwomba Mungu wake, na mambo ya wachunguzaji waliosema naye katika Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli tunayaona, yametiwa katika mambo ya wafalme wa Waisiraeli.
19Maombo yake na vilio vyake na makosa yake yote ya kuvunja maagano na mahali, alipojenga vijumba vya kutambikia vilimani, napo aliposimamisha miti ya Ashera na vinyago vingine, alipokuwa hajajinyenyekeza bado, yote yamekwisha kuandikwa katika mambo ya wachunguzaji.
20Kisha Manase akaja kulala na baba zake, wakamzika nyumbani mwake, naye mwanawe Amoni akawa mfalme mahali pake.
21Amoni alikuwa mwenye miaka 22 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 2 mle Yerusalemu.
22Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya, navyo vinyago vyote, baba yake Manase alivyovitengeneza, Amoni akavitambikia na kuvitumikia.
23Hakujinyenyekeza mbele ya Bwana, kama baba yake Manase alivyojinyenyekeza, kwani yeye Amoni alikora manza nyingi.[#2 Mambo 33:12.]
24Ndipo, watumishi wake walipomlia njama, wakamwua nyumbani mwake.
25Lakini watu wa nchi hiyo wakawaua wote waliomlia mfalme Amoni njama, kisha hao watu wa nchi hiyo wakamfanya mwanawe Yosia kuwa mfalme mahali pake.