The chat will start when you send the first message.
1Yosia alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 31 mle Yerusalemu.
2Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, akaendelea na kuzishika njia za baba yake Dawidi, hakuziacha na kujiendea kuumeni wala kushotoni.[#2 Mambo 29:2.]
3Katika mwaka wa nane wa ufalme wake, yeye alipokuwa akingali mvulana, alianza kumtafuta Mungu wa baba yake Dawidi; tena katika mwaka wa kumi na mbili alianza kuitakasa nchi ya Yuda na mji wa Yerusalemu na kuyaondoa matambiko ya vilimani na miti ya Ashera na vinyago vingine vya kuchonga navyo vilivyoyeyushwa.
4Usoni pake wakazivunjavunja meza za kuyatambikia Mabaali, nayo mifano ya jua iliyosimamishwa juu yao wakaikatakata, nayo miti ya Ashera na vinyago vingine vya kuchonga navyo vilivyoyeyushwa akavipondaponda, hata vikawa mavumbi, kisha hayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi yao waliovitambikia.[#2 Mambo 14:5; 3 Mose 26:30.]
5Nayo mifupa ya watambikaji wao akaiteketeza juu ya meza zao za kutambikia. Ndivyo, alivyoitakasa nchi ya Yuda na mji wa Yerusalemu.[#1 Fal. 13:2.]
6Namo mijini mwa Manase na mwa Efuraimu, hata mwa Nafutali katika mahame yao yaliyokuwapo po pote
7ndimo, alimozivunjavunja meza za kutambikia, akaiponda miti ya Ashera navyo vinyago vingine, hata vikawa mavumbi, nayo mifano yote ya jua akaikatakata katika nchi yote ya Isiraeli, kisha akarudi Yerusalemu.
8Katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wake alipokwisha kuitakasa nchi na Nyumba hiyo, akamtuma Safani, mwana wa Asalia, na Masea, mkuu wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa, kwenda kuitengeneza vizuri Nyumba ya Bwana Mungu wake.
9Wakaja kwa mtambikaji mkuu Hilkia, wakampa zile fedha zilizopelekwa Nyumbani mwa Mungu, ambazo wangoja vizingiti walizikusanya kwao Wamanase na Waefuraimu na kwa Waisiraeli wote wengine na kwa Wayuda na Wabenyamini wote, hata kwa wenyeji wa Yerusalemu.
10Wakazitia hizo fedha mikononi mwao wenye hiyo kazi waliowekwa kuzisimamia kazi za Nyumbani mwa Bwana; nao wenye hiyo kazi wakazipa wao waliozifanya kazi Nyumbani mwa Bwana za kuirudishia upya Nyumba ya Bwana kwa kuitengeneza vizuri.
11Nao wakazipa maseremala na waashi za kununua mawe ya kuchonga na miti ifaayo ya kuungia na ya boriti za vipaa vya nyumba.
12Watu hao walifanya kazi zao kwa welekevu; waliowekwa kuwasimamia katika kazi ni Walawi Yahati na Obadia waliokuwa wa mlango wa Merari, tena Zakaria na Mesulamu waliokuwa wa mlango wa Kehati. Nao walawi wote waliojua kupiga vyombo vya kuimbia
13walikuwa kwao wachukuzi, nao wakawasimamia wafanya kazi wote, kila mmoja katika utumishi wake, tena walikuwako Walawi walio waandishi na wenye amri na walinda malango.
14Walipozitoa zile fedha zilizopelekwa Nyumbani mwa Bwana, ndipo, mtambikaji Hilkia alipokiona kitabu cha Maonyo ya Bwana, aliyopewa Mose.
15Hilkia akasema na kumwambia mwandishi Safani: Nimeona Kitabu cha Maonyo Nyumbani mwa Bwana! Kisha Hilkia akampa Safani hicho kitabu.
16Safani akakipeleka hicho kitabu kwa mfalme, tena akampasha mfalme habari kwamba: Yote yaliyowekwa mikononi mwa watumishi wako, wao wanayafanya.
17Fedha zilizooneka Nyumbani mwa Bwana wamezimimina, wakawapa wasimamizi mikononi mwao namo mikononi mwao wafanya kazi.
18Kisha mwandishi Safani akamsimulia mfalme kwamba: Mtambikaji Hilkia amenipa kitabu; kisha Safani akasoma humo mbele ya mfalme.
19Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya Maonyo, akayararua mavazi yake.
20Kisha mfalme akamwagiza Hilkia na Ahikamu, mwana wa Safani, na Abudoni, mwana wa Mika, na mwandishi Safani na Asaya aliyekuwa mtumishi wa mfalme kwamba:
21Nendeni kuniulizia Bwana mimi na masao ya Waisiraeli na ya Wayuda kwa ajili ya maneno ya hiki kitabu kilichooneka, kwani makali ya Bwana yenye moto ni makuu, nayo humwagika kwetu, kwa kuwa baba zetu hawakulishika Neno la Bwana na kuyafanya yote yaliyoandikwa humu kitabuni.
22Ndipo, Hilkia alipokwenda pamoja nao wa mfalme kwa mfumbuaji wa kike Hulda, mkewe Salumu, mwana wa Tokati, mwana wa Hasira aliyeyaangalia mavazi; naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili, wakamwambia maneno yaleyale.
23Akawaambia: Ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mwambieni yule mtu aliyewatuma kwangu:
24Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikileta mabaya mahali hapa, yawapate wenyeji wa hapa, ndio viapo vyote vilivyoandikwa katika kitabu, walichokisoma masikioni pa mfalme wa Wayuda,[#3 Mose 26:14-39; 5 Mose 28:15-68.]
25kwa kuwa wameniacha, wakavukizia miungu mingine, wanikasirishe kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo makali yangu yenye moto yatamwagwa hapa, wala hayatazimika.
26Naye mfalme wa Wayuda aliyewatuma kumwuliza Bwana mwambieni haya: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kwa kuwa hapo, ulipoyasikia maneno yale,
27moyo wako umelegea, ukajinyenyekeza mbele ya Mungu papo hapo ulipoyasikia maneno yake, aliyoyasema ya mahali hapa na ya wenyeji wake, ukajinyenyekeza kweli mbele yangu na kuyararua mavazi yako na kunililia mimi, basi, kwa hiyo mimi nami nimekusikia; ndivyo, asemavyo Bwana.[#2 Mambo 33:12.]
28Utaniona, nikikuita, uje kukutana na baba zako; ndipo, utakapopelekwa kulala kaburini mwako na kutengemana, macho yako yasiyaone hayo mabaya yote, nitakayopaletea mahali hapa na wenyeji wa hapa. Kisha wakampelekea mfalme majibu haya.
29Ndipo, mfalme alipotuma wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Wayuda na wa Yerusalemu.
30Kisha mfalme akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana pamoja na Wayuda wote na wenyeji wa Yerusalemu na watambikaji na Walawi na watu wote pia, wakubwa kwa wadogo, akawasomea masikioni pao maneno yote ya kitabu cha Agano kilichooneka Nyumbani mwa Bwana.
31Kisha mfalme akaja kusimama katika ulingo wake, akafanya mbele ya Bwana agano la kumfuata Bwana na kuyaangalia maagizo yake na mashuhuda yake na maongozi yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, ayafanye maneno ya Agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.[#2 Mambo 15:12; Yos. 24:25.]
32Nao wote walioonekana mle Yerusalemu namo katika nchi ya Benyamini akawashurutisha kulisimamia hilo agano, nao wenyeji wa Yerusalemu wakafanya, kama Agano la Mungu aliye Mungu wa baba zao lilivyowatakia.[#2 Fal. 23:3.]
33Kisha Yosia akaondoa kabisa matambikoi yote yatapishayo katika nchi zote zilizokuwa zao wana wa Isiraeli, nao watu wote walioonekana kwa Waisiraeli akawashurutisha kumtumikia Bwana Mungu wao, nazo siku zake zote za kuwapo hawakuacha kumfuata Bwana Mungu wa baba zao.