2 Mambo 35

2 Mambo 35

Sikukuu ya Pasaka.

(Taz. 2 Fal. 23:21-30.)

1Kisha Yosia akamfanyia Bwana huko Yerusalemu sikukuu ya Pasaka, wakachinja wana kondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.

2Akawaagiza watambikaji kuja kuzifanya kazi zao ziwapasazo, akawashikiza mioyo, watumikie Nyumbani mwa Bwana.

3Akawaambia Walawi waliowafundisha Waisiraeli wote, waliokuwa watakatifu wa Bwana: Liwekeni Sanduku takatifu katika hiyo Nyumba, aliyoijenga Salomo, mwana wa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli! Msilichukue tena mabegani! Sasa mtumikieni Bwana Mungu wenu, mwatumikie nao walio ukoo wake,[#1 Fal. 6:1.]

4mkijiweka tayari kwa milango ya baba zenu na kwa zamu zenu, kama Dawidi, mfalme wa Isiraeli, alivyoviandika, na kama mwanawe Salomo alivyoviandika naye.

5Simameni Patakatifu kwa vyama vya milango ya baba vya ndugu zenu walio watuwatu tu, kila fungu la mlango mmoja lipate Walawi.

6Kisha wachinjeni wana kondoo wa Pasaka na kujitakasa, kuwatengenezeeni ndugu zenu na kufanya, kama Bwana alivyoagiza kinywani mwa Mose!

7Kisha mfalme akawatolea watu kondoo na wana mbuzi, wote kuwa wa Pasaka wa watu wote waliooneka, wote wakawa 30000 na ng'ombe 3000, wote walitoka katika makundi ya mfalme.[#2 Mambo 30:24.]

8Nao wakuu wake waliwatolea watu na watambikaji na Walawi vipaji kwa kupenda wenyewe: Hilkia na Zakaria na Yehieli waliokuwa wenye amri Nyumbani mwa Mungu waliwapa watambikaji wana kondoo wa Pasaka 2600 na ng'ombe 300.

9Nao wakuu wa Walawi Konania na ndugu zake Semaya na Netaneli, tena Hasabia na Yieli na Yozabadi waliwatolea Walawi kondoo wa Pasaka 5000 na ng'ombe 500.

10Utumishi ulipokwisha kutengenezwa, watambikaji wakaja kusimama mahali pao, nao Walawi kwa zamu zao, kama mfalme alivyoagiza.

11Walipowachinja wana kondoo wa Pasaka, watambikaji wakazipokea damu mikononi mwao wakazinyunyiza, nao Walawi wakawa wakichuna.

12Wakaziondoa nyama za kuchoma na kuvipa vyama vya milango yao walio watuwatu tu, wenyewe wamtolee Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo.

13Kisha nyama za Pasaka wakazioka motoni, kama walivyoagizwa; lakini zile za vipaji vitakatifu wakazipika katika vyungu na katika masufuria na katika makaango, wakazipelekea upesi wale walio watuwatu tu.

14Kisha wakajiandalia wenyewe na watambikaji, kwani watambikaji, wana wa Haroni, walifanya kazi za kuziteketeza ng'ombe za tambiko pamoja na mafuta mpaka usiku. Kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe na watambikaji, wana wa Haroni.

15Nao waimbaji, wana wa Asafu, walisimama mahali pao, kama Dawidi na Asafu na Hemani na Yedutuni, mchunguzaji wa mfalme, walivyoviagiza; nao walinda malango walisimama kila penye lango lake, hawakuwa na shuruti kuondoka katika utumishi wao, kwani ndugu zao Walawi waliwaandalia.[#1 Mambo 25:1; 26:1.]

16Ndivyo, kazi zote za utumishi wa Bwana zilivyotengenezwa siku ile ya kufanya Pasaka pamoja na kuteketeza ng'ombe za tambiko mezani pa kumtambikia Bwana, kama mfalme Yosia alivyoagiza.

17Nao wana wa Isiraeli waliokuwako wakafanya Pasaka siku hiyo, nayo hiyo sikukuu ya Mikate isiyochachwa wakaila siku saba.

18Pasaka kama hii haikufanywa kwa Waisiraeli tangu siku za mfumbuaji Samweli; wafalme wote wa Waisiraeli hawakufanya Pasaka, kama Yosia alivyoifanya pamoja na watambikaji na Walawi na Wayuda na Waisiraeli wote waliokuwako na wenyeji wa Yerusalemu.[#2 Mambo 30:26.]

19Pasaka hii ikafanywa katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wa Yosia.

Kufa na kuombolezewa kwake Yosia.

20Hayo yote, aliyoyafanya ya kuitengeneza Nyumba hiyo, yalipokwisha kufanyika, akapanda Neko, mfalme wa Misri, kwenda kupigana Karkemisi penye jito la Furati, naye Yosia akatoka kumpinga.

21Yule akatuma wajumbe kwake kumwambia: Tuko na neno gani mimi na wewe, mfalme wa Yuda? Leo sikukujia wewe, ila ule mlango ninaotaka kupigana nao. Naye Mungu ameniagiza kwenda upesi; jiepushe kwake Mungu aliye upande wangu, asije kukuangamiza!

22Lakini Yosia hakuugeuza uso wake na kumwacha, ila alijipa moyo mwingine kwenda kupigana naye, asiyasikie maneno ya Neko yaliyotoka kinywani mwa Mungu, akaenda kupigana naye bondeni kwa Megido.

23Wenye kupiga mishale wakampiga mfalme Yosia; ndipo, mfalme alipowaambia watumishi wake: Nipitisheni huku! Kwani nimeumia sana.

24Ndipo, watumishi wake walipomtoa katika gari na kumweka katika gari la pili, alilokuwa nalo, wakampeleka Yerusalemu; ndiko, alikokufa. Wakamzika makaburini kwa baba zake. Nao Wayuda na Wayerusalemu wote wakamlilia Yosia,

25naye Yeremia akamwombolezea Yosia. Nao waimbaji wote waume na wake humtaja Yosia katika maombolezo yao hata siku hii ya leo; hivi vikawa desturi kwao Waisiraeli, nayo yamekwisha kuandikwa katika maombolezo.[#Yer. 22:10-11.]

26Mambo mengine ya Yosia na matendo ya upole wake yaliyopatana nayo yaliyoandikwa katika Maonyo ya Bwana,

27nayo mambo yake ya kwanza na ya mwisho tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania