The chat will start when you send the first message.
1Watu wa nchi hii wakamchukua Yoahazi, mwana wa Yosia, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia mle Yerusalemu.
2Yoahazi alikuwa mwenye miaka 23 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi 3 mle Yerusalemu;
3ndipo, mfalme wa Misri alipomwondoa Yerusalemu, akailipisha nchi hii vipande 100 vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000, na kipande kimoja cha dhahabu, ndio shilingi 220000.
4Mfalme wa Misri akamfanya ndugu yake Eliakimu kuwa mfalme wa Wayuda na wa Wayerusalemu, akaligeuza jina lake, akamwita Yoyakimu; lakini ndugu yake Yoahazi Neko akamchukua, akampeleka Misri.
5Yoyakimu alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wake.
6Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akamjia, akamfunga kwa minyororo kumpeleka Babeli.[#Yer. 22:18.]
7Navyo vyombo vingine vya Nyumba ya Bwana Nebukadinesari akavipeleka Babeli, akvitia jumbani mwake huko Babeli.[#Ezr. 1:7.]
8Mambo mengine ya Yoyakimu na matapisho yake, aliyoyafanya, na mengine yaliyooneka kwake tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda. Naye mwanawe Yoyakini akawa mfalme mahali pake.
9Yoyakini alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi mitatu na siku kumi mle Yerusalemu, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana.
10Mwaka mwingine ulipoanza, mfalme Nebukadinesari akatuma, akampeleka Babeli pamoja na vyombo vya Nyumba ya Bwana, alivyovitamani, akamfanya ndugu yake Sedekia kuwa mfalme wao Wayuda na Wayerusalemu.[#Yer. 22:24-30.]
11Sedekia alikuwa mwenye miaka 21 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu.[#Yer. 52:1-27.]
12Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wake; hakujinyenyekeza mbele ya mfumbuaji Yeremia aliyekuwa kinywa cha Bwana.[#Yer. 37—38.]
13Hata mfalme Nebukadinesari akamkataa akiacha kumtii, naye alikuwa amemwapisha na kumtaja Mungu, akaushupaza ukosi wake, nao moyo wake akaufanya kuwa mgumu, asirudi kwake Bwana Mungu wa Isiraeli.
14Nao wakuu wote wa watambikaji na wa watu wakazidi kuyavunja maagano na kufanya mengi kama hayo matapisho yote ya wamizimu, hata Nyumba ya Bwana wakaichafua, aliyoitakasa mle Yerusalemu.[#5 Mose 18:9.]
15Yeye Bwana Mungu wa baba zao akatuma kwao wajumbe pasipo kuchoka kuwatumia, kwani aliwaonea walio ukoo wake huruma, hata Kao lake.
16Lakini wao wakawasimanga wajumbe wa Mungu, nayo maneno yake wakayabeza na kuwafyoza wafumbuaji wake, mpaka makali ya Bwana yawakayo moto wa kuwakasirikia walio ukoo wake yakamkwea, asipatikane aliyeweza kuwaponya.[#Luk. 20:10-12; Tume. 7:52.]
17Ndipo, alipomhimiza mfalme wa Wakasidi kupanda kwenda kwao, akawaua vijana wao kwa panga katika Nyumba iliyokuwa Patakatifu pao, hakuwahurumia, wala mvulana wala mwanamwali, wala wazee wala wakongwe, wote pia Mungu aliwatia mkononi mwake.
18Navyo vyombo vyote vya Nyumbani mwa Mungu, vikubwa kwa vidogo, navyo vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana, navyo vilimbiko vya mfalme na vya wakuu wake, vyote pia akavipeleka Babeli.
19Kisha wakaiteketeza Nyumba ya Mungu wakazibomoa kuta za boma la Yerusalemu, nayo majumba mazuri yote wakayateketeza kwa moto, navyo vyombo vyote vyenye kima wakaviangamiza.
20Nao wote waliosalia, wasiouawa na panga, akawahamisha kwenda Babeli, wakawa watumwa wake yeye na wa wanawe, mpaka Wapersia walipopata ufalme.
21Ndivyo, lilivyotimia neno la Bwana, alilolisema kinywani mwa Yeremia, nchi hii ipate kuimaliza miaka yake ya mapumziko; kwani siku zote za kukaa peke yake tu ilipumzika, hata ikatimia miaka 70.[#3 Mose 26:34; Yer. 25:8-11.]
22Katika mwaka wa kwanza wa Kiro, mfalme wa Wapersia, ndipo, lilipotimia neno la Bwana, alilolisema kinywani mwa Yeremia, maana Bwana akaiamsha roho yake Kiro, mfalme wa Wapersia, akatangaza mbiu katika ufalme wake wote kwa vinywa vya watu na kwa barua kwamba:[#Yer. 29:10; Yes. 44:28.]
23Hivi ndivyo, anavyosema Kiro, mfalme wa Wapersia: Ufalme wote wa nchi hii amenipa Bwana Mungu wa mbinguni, naye mwenyewe akaniagiza kumjengea Nyumba kule Yerusalemu katika nchi ya Yuda; ye yote wa kwenu aliye wa ukoo wake na apande kurudi kwao, naye Bwana Mungu wake awe naye!