2 Mambo 4

2 Mambo 4

Vyombo vya Nyumba ya Mungu.

(Taz. 1 Fal. 7:23-50.)

1Akatengeneza meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyokuwa ya shaba, urefu wake ulikuwa mikono 20, nao upana wake ulikuwa mikono 20, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono 10.[#2 Mambo 7:7.]

2Akaitengeneza nayo ile bahari kwa shaba zilizoyeyushwa, toka ukingo wake wa huku hata ukingo wake wa huko ilikuwa mikono 10; iliviringana pande zote, urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono 5, nayo kamba ya kuizungusha pande zote ilikuwa ya mikono 30.

3Chini yake palikuwa na mifano ya ng'ombe iliyoizunguka pande zote pia, kumi kwa mkono mmoja, ikaizunguka hiyo bahari kuwa ukingo wa chini wenye mistari miwili; nayo hii mifano ya ng'ombe ilikuwa imeyeyushiwa mumo humo, bahari ilipoyeyushwa.

4Ikakaa juu ya ng'ombe 12, tatu zikaelekea kaskazini, tatu zikaelekea baharini, tatu zikaelekea kusini, tatu zikaelekea maawioni kwa jua, nayo bahari ilikuwa juu yao nayo mapaja yao yote yalikuwa yameelekea ndani.

5Unene wake ulikuwa upana wa shibiri, nao ukingo wake wa juu ulikuwa kama wa kikombe au kama wa ua la uwago. Ndani yake zikaenea bati 3000, ndio pishi 27000.

6Akatengeneza hata mitungi 10 ya kuoshea, mitano akaweka kuumeni, mitano kushotoni; ndimo, walimosafishia vyombo vilivyotumika katika kazi za kuteketeza ng'ombe za tambiko, lakini bahari ilikuwa yao watambikaji ya kuogea.

7Akatengeneza hata vinara 10 vya dhahabu sawasawa, kama ilivyoagizwa kuvitengeneza, akaviweka mle jumbani vitano kuumeni, vitano kushotoni.

8Akatengeneza hata meza 10, akazisimamisha mle jumbani, tano kuumeni, tano kushotoni. Akatengeneza hata vyano 100 vya dhahabu.

9Kisha akautengeneza ua wa watambikaji na ua mwingine mkubwa na milango ya uani, hii milango akaifunika kwa mabati ya shaba.

10Ile bahari akaiweka upande wa kuume wa hilo jumba, ielekee mawioni kwa jua, lakini kusini kidogo.

11Kisha Huramu akatengeneza masufuria na majembe na vyano, akazimaliza kazi, alizomfanyizia mfalme Salomo hapo penye nyumba ya Mungu:

12nguzo mbili zenya vilemba na vichwa viwili juu ya hizo nguzo na misuko miwili kama ya mkeka ya kuvifunika vile vilemba viwili vilivyoko juu ya hizo nguzo;

13tena alitengeneza komamanga 400 zilizotiwa katika ile misuko, kila msuko mmoja ukipata mistari miwili ya komamanga ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo;

14tena alitengeneza vile vilingo 10, nayo mitungi aliitengeneza iliyowekwa juu ya hivyo vilingo;

15nayo ile bahari moja na zile ng'ombe 12 zilizokuwa chini yake,

16nayo masufuria na majembe na nyuma, navyo vyombo vingine vyote Huramu-Abiwu alivitengeneza kwa shaba zilizoyeyushwa, mfalme Salomo avitie nyumbani mwa Bwana.

17Naye mfalme alikuwa ameagiza kuviyeyusha katika bwawa la Yordani penye udongo mgumu katikati ya miji ya Sukoti na Sereda.

18Salomo akavitengeneza hivi vyote kuwa vingi mno, kwani shaba zilizotumika hazikupimwa, wala hazikuulizwa, kama ni ngapi.

19Ndivyo, Salomo alivyovitengeneza vyombo vyote vya kutumiwa nyumbani mwa Mungu, tena meza ya kutambikia iliyokuwa ya dhahabu na meza ya mikate, aliyowekewa Bwana,

20na vinara pamoja na taa zao zilizokuwa za dhahabu zilizong'azwa, wapate kuziwasha mbele ya Patakatifu Penyewe, kama walivyoagizwa;

21nayo maua na taa na koleo za dhahabu zilikuwa dhahabu zisizochanganywa na menginemengine;

22nayo makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata na sinia zilikuwa za dhahabu zilizong'azwa, napo pa kuingia nyumbani ile milango ya ndani pa kupaingilia Patakatifu Penyewe nayo milango ya nyumbani pa kupaingilia Patakatifu ilikuwa ya dhahabu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania