The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, Salomo aliposema: Bwana alisema, ya kuwa hukaa mawinguni mwenye weusi.
2Nami nimekujengea Nyumba ya kukaa, iwe Kao lako la kukaa humu kale na kale.
3Kisha mfalme akaugeuza uso wake, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli, nao wote wa mkutano wa Waisiraeli walikuwa wamesimama.
4Akasema: Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! Aliyomwambia baba yangu Dawidi kwa kinywa chake, ameyatimiza kwa mikono yake, ya kwamba:
5Tangu siku ile, nilipowatoa walio ukoo wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji katika mashina yote ya Isiraeli, ndimo wanijengee Nyumba, Jina langu likae humo, wala sikuchagua mtu wa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli.
6Kisha nikachagua Yerusalemu, Jina langu liwemo, nikamchagua Dawidi wa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli.
7Baba yangu Dawidi akawaza moyoni kulijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli nyumba,[#2 Sam. 7:2-13.]
8lakini Bwana akamwambia baba yangu Dawidi: Ukiwaza moyoni mwako kulijengea Jina langu nyumba, umefanya vema kuyawaza hayo moyoni mwako.
9Lakini wewe hutaijenga hiyo nyumba, kwani mwanao atakayetoka viunoni mwako ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba.
10Bwana akalitimiza hilo neno, alilolisema, nami nikaondokea mahali pa baba yangu Dawidi, nikakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, kama Bwana alivyosema, nikalijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba hii.
11Nikaliweka humu Sanduku, Agano la Bwana lilimo, alilolifanya na wana wa Isiraeli.
12Kisha akaja kusimama mbele ya meza ya kumtambikia Bwana machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake.
13Kwani Salomo alikuwa ametengeneza hapo ulingo wa shaba, akauweka hapo uani katikati, urefu wake ulikuwa mikono mitano, nao upana wake mikono mitano, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu, akasimama hapo juu, akayapiga magoti yake machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake na kuielekeza mbinguni,
14akasema: Bwana Mungu wa Isiraeli, hakuna Mungu afananaye na wewe, wala mbinguni wala nchini. Unawashikia watumishi wako agano lako na upole wako, wakiendelea mbele yako kwa mioyo yao yote.
15Umemshikia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia; uliyoyasema kwa kinywa chako, umeyatimiza kwa mkono wako, kama inavyoonekana siku hii ya leo.
16Na sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, mshikie mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa machoni pangu katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, wanao wakiziangalia tu njia zao, waendelee kuyafuata Maonyo yangu, kama wewe ulivyoendelea kuwa machoni pangu.[#2 Sam. 7:16.]
17Sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, hilo neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Dawidi, na lishupazwe!
18Inakuwaje? Mungu anakaa kweli na watu huku nchini? Tazama! Mbingu nazo mbingu zilizoko juu ya mbingu hazikuenei, sembuse Nyumba hii, niliyoijenga![#2 Mambo 2:6.]
19Yageukie maombo ya mtumishi wako na malalamiko yake, Bwana Mungu wangu, uvisikilize vilio na maombo, mtumishi wako anayokuomba usoni pako!
20Uwe macho kuiangalia Nyumba hii mchana na usiku, ipate kuwa mahali pale, uliposema: Mahali hapa ndipo, Jina langu litakapokuwa! Kwa hiyo yasikie maombo, mtumishi wako atakayokuomba mahali hapa![#2 Mose 20:24.]
21Yasikie nayo malalamiko ya mtumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, watakayokuomba mahali hapa! Wewe wasikie huko juu mbinguni, unakokaa! Tena utakapowasikia uwaondolee makosa!
22Mtu akikosana na mwenziwe, akachukuliwa, aape, basi, wakimwapisha hivyo, naye akija kuapia mbele ya meza ya kutambikia katika Nyumba hii,[#2 Mose 22:11.]
23wewe umsikie huko mbinguni, ulitengeneze jambo hilo na kuwaamua watumishi wako, ukimrudishia yule aliyekosa na kumtwika kichwani pake matendo yake, tena yule asiyekosa ukimtokeza kuwa pasipo kosa, ukimpa yaliyo haki yake.
24Itakuwa, walio ukoo wako wa Waisiraeli wakimbizwe na adui, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapokurudia na kuliungama Jina lako, wakuombe na kukulalamikia humu Nyumbani,[#5 Mose 28:25.]
25wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee walio ukoo wako wa Waisiraeli makosa yao! Kisha warudishe katika nchi hii, uliyowapa baba zao.
26Itakuwa, mbingu zizibane, mvua isinye, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapoombea mahali hapa na kuliungama Jina lako na kuyaacha makosa yao, kwa kuwa umewatesa,[#5 Mose 28:23-24.]
27wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee makosa yao walio watumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli! Kisha wafundishe njia iliyo njema, waishike, upate kuinyeshea nchi yako mvua tena, kwa kuwa umeipa watu wa ukoo wako, iwe fungu lao.
28Itakuwa, njaa iingie katika nchi hii au magonjwa mabaya, itakuwa, jua kali linyaushe mashamba yote, itakuwa, nzige na funutu wamalize vilaji vyote, itakuwa, adui zao wawasonge watu kwao malangoni mwao, itakuwa, mapigo menginemengine na magonjwa yo yote yawapate,
29basi, lisikie kila ombo na kila lalamiko litakalokutokea, kama ni la mtu awaye yote, au la watu wote walio ukoo wako wa Waisiraeli, kwa kuwa kila mtu anayajua mapigo yake na maumivu yake! Hapo, watakapokuja kuikunjua mikono yao humu Nyumbani,
30wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uwaondolee makosa na kumrudishia kila mtu, kama njia zake zilivyo, kwa hivyo, unavyoujua moyo wake! Kwani wewe peke yako unaijua mioyo ya wana wa watu,[#1 Mambo 29:17; Sh. 7:10.]
31kusudi wakuogope na kuzishika njia zako siku zote, watakazokuwapo katika nchi hii, uliyowapa baba zetu.
32Tena itakuwa, hata mgeni asiye wa ukoo wako wa Waisiraeli aje huku na kutoka katika nchi ya mbali kwa ajili ya Jina lako lililo kuu na kwa ajili ya kiganja chako kilicho na nguvu na kwa ajili ya mkono wako uliokunjuka; basi, hapo watakapokuja, waombee humu Nyumbani,
33wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uyafanye yote, yule mgeni atakayokuomba na kukulilia, makabila yote ya nchi yalijue Jina lako, wakuogope kama wao walio ukoo wako wa Waisiraeli, tena wajue, ya kuwa Nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa Jina lako.
34Itakuwa, walio ukoo wako wakitoka kupigana na adui zao na kuishika njia, utakayowatuma, wakuombe njiani na kuuelekea mji huu, uliouchagua, hata Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako,[#Dan. 6:10.]
35basi, hapo na uyasikie huko mbinguni maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao.
36Tena itakuwa, wakukosee, kwani hakuna mtu asiyekosa, nawe utawakasirikia, uwatie mikononi mwao adui, wawateke na kuwahamisha wakiwapeleka katika nchi ya mbali au ya karibu;
37lakini hapo, watakapojirudia wenyewe mioyoni mwao katika nchi hiyo, walikohamishiwa, basi, hapo watakapokulalamikia tena katika nchi ya uhamisho wao na kusema: Tumekosa, tumekora manza, tumefanya maovu,[#Dan. 9:5.]
38watakapokurudia hivyo kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote katika nchi ya uhamisho wao, walikohamishiwa, watakapokuomba na kuielekea nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji, uliouchagua, na Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako,
39basi, wewe huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa na uyasikie maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao na kuwaondolea walio ukoo wako makosa yao, waliyokukosea!
40Sasa Mungu wangu, uwe macho, nayo masikio yako yawe yametegwa kuyasikiliza maombo ya mahali hapa!
41Sasa inuka, Bwana Mungu, uingie hapa, ndipo utulie na Sanduku lililo na nguvu yako! Watambikaji wako, Bwana Mungu, na wavikwe wokovu, nao wakuchao wayafurahie mema![#Sh. 132:8-9.]
42Bwana Mungu, usikatae kuuona uso wa mtu wako aliyepakwa mafuta! Yakumbuke nayo matendo ya upole ya mtumishi wako Dawidi![#2 Sam. 7:13.]