2 Mambo 8

2 Mambo 8

Miji, Salomo aliyoijenga.

(Taz. 1 Fal. 9:10-28.)

1Ile miaka ishirini, ambayo Salomo aliijenga Nyumba ya Bwana na nyumba yake, ilipokwisha,

2ndipo, Salomo alipoijenga ile miji, Huramu aliyompa Salomo, akakalisha humo wana wa Isiraeli.

3Kisha Salomo akaenda Hamati-Soba, akauchukua.

4Akajenga Tadimori ulioko nyikani, hata miji yote yenye vilimbiko, aliyoijenga kule Hamati.

5Kisha akajenga Beti-Horoni wa juu na Beti-Horoni wa chini kuwa miji yenye maboma iliyokuwa na kuta na malango na makomeo.

6Ndivyo, alivyojenga hata Balati na miji yote yenye vilimbiko, Salomo aliyokuwa nayo, hata miji yote ya magari na miji ya farasi na majengo yote yaliyompendeza Salomo, aliyotaka kuyajenga kwa mapenzi yake mle Yerusalemu nako huko Libanoni na katika nchi yo yote ya ufalme wake.

7Watu aliowatumia, ndio wote waliosalia na Wahiti na wa Waamori na wa Waperizi na wa Wahiwi na wa Wayebusi wasiokuwa wa Waisiraeli;

8wana wao wale waliosalia na kuachwa na wenzao katika nchi hii, kwa kuwa wana wa Isiraeli hawakuwamaliza, basi, hao wote Salomo akawafanyisha kazi za utumwa hata siku hii ya leo.[#Yos. 16:10.]

9Lakini wana wa Isiraeli Salomo hakuwataka kuwa watumwa wa kumfanyizia kazi, kwani hawa walikuwa wapiga vita na wakuu wa thelathini na wakuu wa magari yake na wapanda farasi wake.

10Nao wakuu wa mfalme Salomo waliowekwa kusimamia kazi walikuwa 250, ndio waliowatawala watu wa kazi,

11Binti Farao Salomo akamtoa mjini mwa Dawidi, akampeleka kukaa katika nyumba, aliyomjengea, kwani alisema: Mwanamke asikae kwangu nyumbani mwa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli, kwa kuwa ni takatifu, kwani Sanduku la Bwana liliingia mumo humo.

Salomo anayatengeneza matambiko.

12Tangu hapo ndipo, Salomo alipomtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa hapo mezani pa kumtambikia Bwana, alipopajenga mbele ya ukumbi;[#2 Mambo 1:3-6; 4:1.]

13akatoa ng'ombe za tambiko zipasazo kila siku moja, kama Mose alivyoagiza: za mapumziko, za miandamo ya mwezi, za sikukuu zilizo tatu za kila mwaka: sikukuu ya Mikate isiyochachwa, sikukuu ya Majuma na sikukuu ya Vibanda.[#4 Mose 28:2,9,11,17,26; 29:12.]

14Kama baba yake Dawidi alivyoviagiza, akayaweka mafungu ya watambikaji ya kuzifanya kazi zao nayo ya Walawi kwa zamu zao: wa kuimba mashangilio nao wa kuwatumikia watambikaji, kama ilivyopasa kila siku moja; akawaweka nao walinda malango kwa mafungu yao, walingoje kila lango moja, kama Dawidi aliyekuwa mtu wa Mungu alivyoviagiza.[#1 Mambo 23—26.]

15Hawakutangua agizo la mfalme, alilowaagiza la watambikaji na la Walawi kwa ajili ya mambo yote, hata kwa ajili ya vilimbiko.

16Kwa hiyo kazi zote za Salomo zikaendelea vema tangu siku ile, misingi ya Nyumba ya Bwana ilipowekwa, hata siku hiyo, Nyumba yote nzima ya Bwana ilipomalizika.

Safari za baharini.

17Kisha Salomo akaenda Esioni-Geberi na Eloti huko pwani kwenye bahari iliyoko katika nchi ya Edomu.

18Huramu akatuma kwake vyombo vilivyopelekwa na watumishi wake pamoja na watumishi walioyajua mambo ya baharini; wakaenda Ofiri pamoja na watumishi wake Salomo, wakachukua huko vipande vya dhahabu 450, ndio frasila 1350, wakampelekea mfalme salomo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania