2 Wakorinto 11

2 Wakorinto 11

Mitume wa uwongo.

1Ingefaa, mnivumilie, nikitumia upuzi kidogo; najua, mtanivumilia.

2Kwani wivu, ninaouona kwa ajili yenu, ni wa Kimungu; maana naliwaposea ninyi mume mmoja, ni Kristo, niwapeleke kwake kuwa mwanamwali mwenye kutakata.[#Ef. 5:26-27.]

3Lakini kama nyoka alivyomdanganya Ewa kwa werevu wake mbaya, ninao woga wa kwamba: Vivyo hivyo nayo mawazo yenu yataangamizwa, msiweze tena kuandamana na Kristo peke yake tu na kumng'alia.[#1 Mose 3:4,13.]

4Kwani mtu anapokuja kwenu na kutangaza Yesu mwingine, tusiyemtangaza sisi, au mnapopata roho nyingine, msiyoipata, au mnapotangaziwa Utume mwema mwingine, msioupokea, basi, ninyi huvumilia vizuri.[#Gal. 1:8-9.]

5Lakini nadhani, hakuna nishindwacho nao wale wajipao macheo yote ya utume.[#2 Kor. 12:11; 1 Kor. 15:10; Gal. 2:6,9.]

6Hata nikiwa mpumbavu wa kusema, si mpumbavu wa kutambua, nanyi mmetuona kuwa hivyo po pote katika mambo yote.[#1 Kor. 2:1-2,13; Ef. 3:4.]

7Au nimekosa, nilipojinyenyekeza, ninyi mpate kuwa wakubwa? Au nimekosa, kwa kuwa nimewatangazia Utume mwema wa Mungu pasipo malipo?[#1 Kor. 9:12-18.]

8Wateule wengine nimewapokonya na kutwaa matunzo, nipate kuwatumikia ninyi.[#Fil. 4:10,15.]

9Napo, nilipokuwako kwenu, nikawa nimekosa vyakula, hakuna, niliyemsumbua. Kwani ndugu waliokuja toka Makedonia waliniongezea, nilivyovikosa. Katika mambo yote nimejiangalia, nikae kwenu pasipo kuwasumbua, navyo ndivyo, nitakavyojiangalia.[#2 Kor. 12:13.]

10Kwa hivyo ukweli wake Kristo ulivyomo mwangu, hayo majivuno yangu hayatavunjika katika nchi za Akea.[#1 Kor. 9:15.]

11Kwa sababu gani? Kwamba siwapendi ninyi? Mungu amevijua!

12Lakini nifanyalo nitafuliza kulifanya, niiumbue mizungu yao wale wanaotafuta mizungu ya kujivunia kwamba: Sisi tulivyo, nao huonekana kuwa vivyo hivyo.

13Kwani hao ndio mitume wa uwongo na wafanya kazi wajanja, hujigeuza kuwa mitume wa Kristo.[#2 Kor. 2:17; Fil. 3:2.]

14Nalo hili silo la kustaajabu. Kwani Satani mwenyewe hujigeuza kuwa malaika mwenye mwanga.

15Kwa hiyo si neno kubwa, watumishi wake nao wakijigeuza kuwa watumishi wenye wongofu, lakini mwisho wao utakuwa umepatana na kazi zao.

Majivuno ya Paulo.

16Nasema tena, mtu asiniwazie kuwa mpuzi. Kama hamtaki, vilevile nipokeeni kama mpuzi, nijivune nami kidogo![#2 Kor. 12:6.]

17Ninayoyasema sasa, siyasemi kuwa maneno ya Bwana, ila nayasema kama ya upuzi tu kwa hivyo, tulivyoyafikia majivuno.

18Kwa sababu wengi hujivuna kimtu, nami nitajivuna.

19Kwani ninyi mlio wenye akili hupenda kuwavumilia wapuzi.

20Mwavumilia, mtu akiwafanya watumwa, akiwala, akiyatwaa yaliyo yenu, akijikuza, akiwapiga usoni.

21Naona soni nikisema: Hayo hatuyawezi, tu wanyonge; lakini jambo lo lote, mtu alilojipa moyo wa kujivunia, (nasema kipuzi) nami najivunia lilo hilo.

22Ni Waebureo? Hata mimi. Ni Waisiraeli? Hata mimi. Ni uzao wake Aburahamu? Hata mimi.[#Fil. 3:5.]

23Ni watumishi wa Kristo? Mimi nawapita; nasema kama mwenye wazimu. Nimesumbuka kuwapita, nimefungwa kuwapita, nimepigwa kuwapita kabisa, mara nyingi nimetakiwa kufa.[#2 Kor. 6:4-5; 1 Kor. 15:10.]

24Mara tano nalipata kwa Wayuda fimbo 40 kupungua moja,[#5 Mose 25:3.]

25mara tatu nalipigwa viboko, mara moja nalipigwa mawe, mara tatu chombo changu kimevunjika baharini, nikawamo kilindini usiku na mchana.[#Tume. 14:19; 16:22.]

26Safari zangu ni nyingi, nikapata masumbuko ya mito na masumbuko ya wanyang'anyi na masumbuko ya watu wa ukoo wetu na masumbuko ya wamizimu na masumbuko ya mijini na masumbuko ya nyikani na masumbuko ya baharini na masumbuko yaliyoko kwenye ndugu wa uwongo.

27Nimeumia, mpaka nikachoka, nikikesheshwa mara nyingi, nikiumizwa na njaa na kiu, nikinyimwa mara nyingi vyakula, nikiwekwa penye baridi pasipo nguo.[#2 Kor. 6:5.]

28Hayo ya nje hupitwa nayo yanijiayo kila siku, nikiwasumbukia wateule wote.[#Tume. 20:18-21,31.]

29Yuko mnyonge asiyenitia unyonge nami? Yuko anayekwazwa, nisipoumizwa nami?[#1 Kor. 9:22.]

30Nikishurutishwa kujivuna nitajivunia unyonge wangu.[#2 Kor. 12:5.]

31Mungu, Baba wa Bwana Yesu, atukuzwaye kale na kale anajua: sisemi uwongo.[#2 Kor. 1:23.]

32Huko Damasko mtawala watu wa mfalme Areta aliulinda mji wa Damasko, apate kunikamata.

33Nami nikatolewa dirishani, nikashushwa katika kapu ukutani, nikaokoka mikononi mwake.[#Tume. 9:24-25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania