2 Wakorinto 4

2 Wakorinto 4

Utume wa Paulo.

1Kwa sababu tumepewa utumishi huo, nasi kwa hivyo, tulivyohurumiwa, hatuchoki;[#2 Kor. 3:6; 1 Kor. 7:25.]

2tukayakataa mambo ya kufichaficha, maana ni yenye soni, kwani hatuendelei kwa werevu mbaya, wala hatuchanganyi Neno la Mungu na uwongo. Ila kwa hivyo, tunavyoyafumbua yaliyo ya kweli, twajitokeza waziwazi mioyoni mwa watu wote, wajue, ya kuwa tupo machoni pa Mungu.[#2 Kor. 2:17; 1 Tes. 2:5.]

3*Lakini Utume wetu mwema ukiwa umefunikwa, uko umefunikwa kwao walio wenye kuangamia;[#1 Kor. 1:18.]

4maana kwao ndiko, mungu wa nchini alikopofusha mawazo yao wasiomtegemea Mungu, wasiangazwe na mwangaza wa Utume mwema wa utukufu wake Kristo aliye mfano wa Mungu.[#Ebr. 1:3.]

5Kwani hatujitangazi sisi wenyewe, ila twatangaza kwamba: Kristo Yesu ni Bwana, nasi tu watumwa wenu kwa ajili ya Yesu.[#1 Kor. 1:24.]

6Kwani Mungu aliyesema: Penye giza pamulike mwanga! ndiye aliyeiangaza mioyo yetu, ndani yao utokee mwanga unaotambulisha hata wengine utukufu wa Mungu uliopo usoni pake Kristo.*[#2 Kor. 3:18; 1 Mose 1:3.]

Nguvu ya kumtegemea Mungu.

7Hiki kilimbiko chetu tunacho, lakini kimo katika vyombo vya udongo, kusudi zile nguvu nyingi zilizomo zijulike kwamba: Ndizo zake Mungu, kwamba: Hazotoki kwetu sisi.[#2 Kor. 5:1.]

8Po pote twaumizwa, lakini hatusongeki; twahangaishwa, lakini hatuhangaikiki,[#2 Kor. 1:8; 7:5.]

9twakimbizwa, lakini hatuachwi peke yetu; twaangushwa chini, lakini hatuangamiki.

10Po pote, tunapozunguka, twakujulisha kuuawa kwake Yesu miilini mwetu, kwamba nako kuishi kwake Yesu kupate kutokea miilini mwetu.[#1 Kor. 15:31; Gal. 6:17.]

11Kwani sisi tunaoishi hutolewa kila siku, tuuawe kwa ajili ya Yesu kwamba: Nako kuishi kwake Yesu kupate kutokea katika miili yetu iliyo yenye kufa.[#Rom. 8:36.]

12Kwa hivyo kufa hupata nguvu mwetu, nako kuishi mwenu.[#Sh. 116:10.]

13Lakini tulivyo wenye Roho yule yule wa kumtegemea Mungu, hutimia kwetu lililoandikwa la kwamba:

Nilikuwa nimemtegemea Mungu, kwa hiyo nilisema. Nasi tunamtegemea Mungu, kwa hiyo husema.

14Kwani twajua: Aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua hata sisi pamoja na Yesu, kisha atatuweka mahali, tutakapokuwa pamoja nanyi.[#1 Kor. 6:14.]

15Kwani yote hutupata kwa ajili yenu, maana wenye kugawiwa kipaji wakiwa wengi, hao wengi nao watakazana kuutukuza utukufu wake Mungu.[#2 Kor. 1:3-6.]

16Kwa hiyo hatuchoki, maana ikiwa miili yetu huchakaa, mioyo yetu hupata upya siku kwa siku.[#2 Kor. 4:10; Ef. 3:16.]

17Kwani maumivu yetu yaliyo ya sasa hivi tu, yapitayo upesi, huzidi kutupatia utukufu usiopimika, usio na mwisho,[#Rom. 8:17-18; Ebr. 12:11.; Ebr. 11:1.]

18tusipoyatazama yaonekanayo, ila yale yasiyoonekana. Kwani yaonekanayo hukaa siku chache tu, lakini yasiyoonekana ni ya kale na kale.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania