The chat will start when you send the first message.
1*Nasi tulio wenziwe wa kazi twawaonya, msigawiwe bure kipaji cha Mungu.[#2 Kor. 1:24; 5:20.]
2Kwani anasema:
Nimekuitikia, siku zilipokuwa za kupendezwa,
nikakusaidia siku ya wokovu.
Tazameni, siku za kupendezwa kweli ndizo za sasa hivi! Tazameni, leo ni siku ile ya wokovu!
3Hakuna hata mmoja, tumkwazaye kwa jambo lo lote, utumishi wetu usibezwe.
4Ila po pote twajitokeza kwamba: Sisi humtumikia Mungu, kwa hivyo twavumilia mengi; maumivu, mahangaiko, masongano,[#2 Kor. 4:2.]
5mapigo, mafungo, mashambulio, masumbuko, kukesha na kufunga.[#2 Kor. 11:23-27.]
6Twataka kujijulisha kuwa wenye utakato, utambuzi, uvumilivu, utu, Roho takatifu, upendo usiojua ujanja,[#1 Tim. 4:12.]
7neno la kweli, nayo nguvu ya Mungu. Mata yanayotupa kushinda kuumeni na kushotoni ndiyo ya wongofu,[#1 Kor. 2:4; Ef. 6:13-17.]
8ikiwa twatukuzwa, au ikiwa twabezwa; ikiwa twasingiziwa, au ikiwa twashangiliwa. Tuko kama wapotezaji, lakini tu wa kweli;
9tuko kama wasiojulika, lakini tumetambulikana; tuko kama wenye kufa, lakini tazameni, tu wenye kuishi! Tuko kama wenye kupondwa, lakini hatuuawi;[#2 Kor. 4:10-11; Sh. 118:18.]
10tuko kama wenye kusikitika, lakini twafurahi po pote; tuko kama maskini, lakini twagawia wengi mali nyingi; tuko kama wasio na kitu cho chote, lakini vyote tunavyo.*[#Fil. 4:12-13.]
11Enyi Wakorinto, tumewafumbulia vinywa vyetu, tena mioyo yetu nayo imewafungukia kabisa.
12Humu ndani yetu penu sipo padogo, lakini mioyoni mwenu mnasongeka.
13Nasema nanyi kama na watoto wangu, nikiwaambia: Tulipeni vivyo hivyo, mkitupatia nasi pakubwa mioyoni mwenu![#1 Kor. 4:14.]
14*Msiingie utumwa wa mwingine pamoja nao wasiomtegemea Mungu! Je? Yako magawio wongufu na upotovu unayoyagawiana? Au iko bia ya mwanga na ya giza?[#Ef. 5:11.]
15Yako mapatano ya Kristo na ya Beliali? Au liko fungu lililo lake amtegemeaye Mungu nalo lake asiyemtegemea Mungu?
16Au iko nyumba yake Mungu inayofanana napo penye mizimu? Kwani sisi tu nyumba yake Mungu aliye Mwenye uzima; kama Mungu alivyosema:
Nitakaa katikati yao, tena nitatembea katikati yao,
nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa ukoo wangu.
17Kwa hiyo Bwana anasema:
Tokeni kati yao, mjitenge,
msiguse yenye uchafu, nami nipate kuwapokea!
18Ndipo, nitakapokuwa Baba yenu,
nanyi mtakuwa wanangu wa kiume na wa kike.
Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mwenyezi.