2 Wakorinto 8

2 Wakorinto 8

Kuchanga vipaji.

1Ndugu, twawatambulisha kipaji cha Mungu, wateule wa Makedonia walichogawiwa:[#Rom. 15:26.]

2maana walipojaribiwa na maumivu yao mengi wameshinda, wakachangamka sana; kwa hiyo hao walio wenye umaskini usiopimika wakajikaza kuonyesha wingi wa mali zilizomo katika mioyo yenye neno moja tu.

3Kwani nawashuhudia kwamba: Wenyewe walipendezwa na kuchanga, kama walivyoweza, na kupapita hapo, walipoweza.

4Wakatubembeleza sana na kutuomba, tusiwakataze kulitoa fungu lao la kuingia katika bia hiyo ya kuwatumikia watakatifu.[#2 Kor. 9:1; Tume. 11:29.]

5Tena hawakutoa, kama tulivyowangojea, ila kwanza walijitoa wenyewe kumtumikia Bwana na sisi; hivyo wameyamaliza, Mungu ayatakayo.

6Kwa hiyo tulimhimiza Tito, aitimize hata kwenu kazi hiyo ya vipaji, kama alivyoianza kwanza.

7Lakini kama mwapitavyo wengine katika mambo yo yote, ikiwa kumtegemea Mungu au kupiga mbiu au kutaka utambuzi au kujihimiza kufanya mema yo yote au kutupenda kwa moyo, kama tunavyowapenda ninyi, hivyo sharti mwapite hata katika vipaji hivi.[#1 Kor. 1:5; 16:1-2.]

8Sisemi, kwamba niwatolee nguvu, lakini kwa hivyo, wengine walivyojihimiza, nataka, upendo wenu nao utambulike, ya kama ni wa kweli.

9Kwani mmekitambua kipaji, tulichopewa na Bwana wetu Yesu Kristo: Huyu alikuwa mwenye mali nyingi, akawa maskini kwa ajili yenu, kwamba umaskini wake yeye uwapatie ninyi mali nyingi.[#Mat. 8:20; Fil. 2:7.]

10Nami niliyoyatambua humu, ndiyo, ninayowatolea, kwani yanawafalia ninyi: mwaka wa jana mlitangulia kuifanya kazi hiyo; tena siko kuifanya tu, mlianza hata kuiitikia.

11Lakini sasa sharti mmalize kuifanya, maana kama mapenzi yenu ya kuiitikia yalivyotokea upesi, vivyo hivyo mtokeze nayo mapenzi ya kuifanya mkichanga kwa vile, mlivyo navyo.

12Kwani kama yako mapenzi, mtu hupendezeka akivitoa, alivyo navyo, asivitoe, asivyo navyo.[#Fano. 3:28; Mar. 12:43.]

13Kwani hatuchangii kwamba: Wengine wapate kutulia, ninyi mkiumizwa, ila sharti yalinganike:

14mapato mengi yenu yao wale sharti yapunguze makosekano yenu ya siku nyingine; hivyo yatalinganika,[#2 Kor. 9:12.]

15kama ilivyoandikwa kwamba:

Aliyeokota nyingi hakufurikiwa;

wala aliyeokota chache hakupungukiwa.

Kumtuma Tito na ndugu wengine.

16Lakini na tumshukuru Mungu aliyempa Tito kujihimiza vivyo hivyo moyoni mwake kwa ajili yenu.

17Kwani tulipombembeleza, akaitikia. Lakini kwa hivyo, alivyokaza kujihimiza, aliondoka kwenda kwenu kwa mapenzi yake mwenyewe.

18Tukatuma pamoja naye ndugu mmoja anayesifiwa kwenye wateule wote hivyo, anavyoutangaza Utume mwema.[#2 Kor. 12:18.]

19Lakini sivyo hivyo tu, ila hata kuchaguliwa amechaguliwa nao wateule kuwa mfuasi wetu wa kutusaidia katika kazi hii ya vipaji, tutumikiayo sisi, tumtukuze Bwana, tukijulikana kuwa wenye kumpendeza.[#Gal. 2:10.]

20Hivyo twajikinga, mtu asitusengenye kwa ajili ya machango haya makubwa yatumikiwayo nasi.

21Kwani twajilindia, yaendelee vizuri, sipo mbele ya Bwana tu, ila napo mbele ya watu.

22Tena pamoja nao tulituma ndugu yetu, tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi, anavyojihimiza. Lakini sasa anakaza kujihimiza, kwa sababu yako mengi, anayoyatazamia kwenu.

23Basi, Tito mwamjua kuwa mwenzangu anayenisaidia kazi za kwenu; nao hao ndugu zetu ni mitume wa wateule, maana wampatia Kristo utukufu.[#2 Kor. 7:13; 12:18; Rom. 16:7.]

24Basi, hao waonyesheni upendo wenu, tuliojivunia tulipowatukuza ninyi! Uonyesheni mbele yao wateule![#2 Kor. 7:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania