2 Wakorinto 9

2 Wakorinto 9

Vipaji vinavyompendeza Mungu.

1Kwa ajili ya hayo matumikio yanayochangiwa watakatifu hainipasi kuwaandikia ninyi.[#2 Kor. 8:4,20.]

2Kwani najua, yalivyowapendeza; nami ninajivunia kwa ajili yenu kwa wamakedonia kwamba: Waakea wamejitengeneza tangu mwaka wa jana. Nako kujihimiza kwenu kumehimiza wengine wengi.[#2 Kor. 8:19.]

3Lakini nimewatuma hao ndugu, maana hivyo, tulivyojivuna kwa ajili yenu, visipungukiwe katika jambo hili, ila mjulikane, ya kuwa mmejitengeneza, kama nilivyosema.[#2 Kor. 8:24.]

4Maana kama Wamakedonia wanakuja pamoja nami, wakawaona ninyi, hamkujitengeneza, tutakuwa waongo sisi, nisiseme: Ninyi, kwa ajili ya hayo majivuno yetu.

5Kwa hiyo nalijishurutisha kuwaonya ndugu waliotangulia kufika kwenu, waanze kuvichanga vipaji vya upendo wenu, mlivyotuagia kale, tuvikute, vimekwisha kuchangwa kuwa vipaji vya upendo wa kweli, sivyo vya choyo.

6*Twajua hayo: Mwenye kupanda kwa choyo huvuna yenye choyo; naye mwenye kupanda kwa kubariki huvuna yenye mbaraka.[#Fano. 11:24; 19:17.]

7Kila mtu atoe, kama alivyoanza kupima moyoni, asitoe akiwa na mafundo au akishurutishwa! Kwani Mungu humpenda mwenye kutoa na kushangilia.[#Fano. 22:9; Rom. 12:8.]

8Naye Mungu anaweza kuwapatia matunzo yote, kwamba hayo, mpaswayo nayo, siku zote yawatoshee kabisa, tena yasalie ya kutolea kazi njema zote,

9kama ilivyoandikwa:

Alizimwaga, akawagawia wao waliozikosa;

huu wongofu wake hukaa kale na kale.

10Lakini yeye anayemtolea mpanzi mbegu hutoa nao mkate wa kula; yeye ataziongeza nazo mbegu zenu, ziwe nyingi, kisha atayachipuza mazao ya wongofu wenu.[#Yes. 55:10; Hos. 10:12.]

11Hivyo mtakuwa wenye mali katika mambo yote, mpate mioyo yenye neno moja tu; hii ndiyo inayomfanyia Mungu kazi na kutupa mikononi vipaji vya kumtukuza.*[#2 Kor. 1:11; 4:15.]

12Kwani kazi hii ya kuchanga vipaji, tunayoitumikia, siyo ya kuyaondoa tu mapungufu ya watakatifu, ila kupita hapo inatimilika kwao wengi, wakimtolea Mungu vipaji vya kumshukuru.[#2 Kor. 8:14.]

13Kazi hii, tunayoitumikia, ikijulikana kuwa ya upendo wa kweli, watamtukuza Mungu, maana mmeyatii hayo, mnayoyaungama kuwa Utume mwema wa Kristo, nayo mioyo yenu ikajulika kwao kuwa yenye neno moja tu kwa hivyo, mlivyowagawia hao nao wengine wote.

14Kwa ajili hii watawaombea ninyi wakitunukia kuwaona, kwa sababu Mungu aliwapa makuu kuliko wengine.

15Na tumshukuru Mungu, kwani ametupa kipaji kisichowezekana kusimuliwa chote!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania