The chat will start when you send the first message.
1Ahabu alipokwisha kufa, Wamoabu wakawavunjia Waisiraeli maagano.[#2 Fal. 3:5.]
2Ahazia akaanguka dirishani penye chumba chake cha juu mle Samaria, akapata kuugua; ndipo, alipotuma wajumbe, aliowaambia: Nendeni kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni, kama nitapona ugonjwa huu.[#1 Fal. 22:52; Yes. 19:3.]
3Lakini malaika wa Bwana akamwambia Elia wa Tisibe: Inuka, uwaendee wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaambie: Je? Kwao Waisiraeli hakuna Mungu, ninyi mkienda kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni?[#Yes. 8:19.]
4Kwa sababu hii Bwana anasema: Hutaondoka tena hapo kitandani, unapolala, ila utakufa kweli, Kisha Elia akaenda zake.
5Wajumbe waliporudi kwake mfalme, akawauliza: Mbona mnarudi?
6Wakamwambia: Mtu ametujia, akatuambia: Haya! Rudini kwa mfalme aliyewatuma, mmwambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Kwao Waisiraeli hakuna Mungu, wewe ukituma kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu hii hutaondoka tena hapo kitandani, unapolala, ila utakufa kweli.
7Akawauliza: Yule mtu aliyewajia na kuwaambia maneno hayo alikuwa na sura gani?
8Wakamwambia: Yule mtu alikuwa amevaa ngozi yenye manyoya, aliyoifunga kwa ukanda wa ngozi viunoni pake. Ndipo, aliposema: Ndiye Elia wa Tisibe.[#Zak. 13:4; Mat. 3:4.]
9Kisha mfalme akatuma kwake Elia mkuu wa kikosi cha hamsini pamoja na watu wake hamsini; alipopanda huko, aliko, akamwona, akikaa juu mlimani, akamwambia: Mtu wa Mungu, mfalme anakuagiza: Shuka!
10Lakini Elia akamjibu huyu mkuu wa hamsini na kumwambia: Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke toka mbinguni, ukule wewe na watu wako hamsini.[#Luk. 9:54; Ufu. 11:5.]
11Akatuma tena kwake mkuu mwingine wa kikosi cha hamsini na watu wake hamsini, naye akasema na kumwambia: Mtu wa Mungu, ndivyo, mfalme anavyosema: Shuka upesi!
12Elia akawajibu kwamba: Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke toka mbinguni, ukule wewe na watu wako hamsini. Ndipo, moto uliposhuka toka mbinguni, ukamla na watu wake hamsini.
13Akatuma mara ya tatu mkuu wa kikosi cha hamsini na watu wake hamsini; huyu mkuu wa tatu wa kikosi cha hamsini alipopanda na kufika kwake akampigia Elia magoti, akamwambia na kumbembeleza: Mtu wa Mungu, roho yangu nazo roho za hawa watumishi wako hamsini usiziwazie kuwa si kitu!
14Tazama, moto ulishuka toka mbinguni, ukawala wale wakuu wa hamsini wawili wa kwanza na watu wao hamsini hamsini, sasa roho yangu usiiwazie kuwa si kutu!
15Ndipo, malaika wa Bwana alipomwambia Elia: Shuka naye, usimwogope! Basi, akaondoka, akashuka naye kwenda kwa mfalme.
16Akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa umetuma wajumbe kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni, kama hakuna Mungu kwao Waisiraeli wa kumwuliza, atakavyosema, kwa sababu hii hutaondoka tena hapa kitandani, unapolala, ila utakufa kweli.[#2 Fal. 1:3-4.]
17Akafa, kwa hilo neno la Bwana, Elia alilolisema; kisha Yoramuakawa mfalme mahali pake katika mwaka wa pili wa Yoramu, mwana wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, kwani Ahazia hakuwa na mwana.[#2 Fal. 3:1.]
18Mambo mengine ya Ahazia, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?