2 Wafalme 10

2 Wafalme 10

Yehu anaumaliza mlango wa Ahabu na ndugu zake Ahazia.

1Ahabu alikuwa na wana 70 kule Samaria. Kwa ajili yao Yehu akaandika barua, akazituma Samaria kwa wakuu wa Izireeli na kwa wazee na kwa watunzaji wa wana wa Ahabu kwamba:

2Kwa kuwa mnao wana wa bwana wenu na magari na farasi na maboma na mata, basi, barua hii itakapofika, kwenu,

3mtazameni aliye mwema mwenye unyofu katika wana wa bwana wenu, mkalisheni katika kiti cha kifalme cha baba yake, kisha mwupigie vita mlango wa bwana wenu!

4Wakashikwa na woga sanasana, wakasema: Wale wafalme wawili hawakuweza kusimama usoni pake, nasi tutawezaje kusimama?

5Kwa hiyo wale waliousimamia ule mlango na mji pamoja na wazee na watunzaji wa wana wakatuma kwa Yehu kumwambia: Sisi tu watumwa wako, nayo yote, utakayotuagiza, tutayafanya, lakini hatuwezi kumweka mtu kuwa mfalme; fanya tu yaliyo mema machoni pako!

6Akawaandikia barua ya pili kwamba: Kama ninyi ni watu wangu, kama ninyi mnataka kunisikia, nikiwaambia neno, vitwaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, mvilete kwangu Izireeli kesho saa hizi! Nao wana wa mfalme, wakuu wa mji waliowakuza, walikuwa 70.

7Barua hii ilipofika kwao, wakawachukua wana wa mfalme, wakawachinja wote 70, navyo vichwa vyao wakavitia katika makapu, wakavituma kwake Izireeli.

8Mjumbe alipokwenda kumpasha habari, ya kuwa wamevileta vichwa vya wana wa mfalme, akasema: Viwekeni machungu mawili hapo pa kuingia langoni mwa mji mpaka kesho!

9Ikawa, alipotoka asubuhi akasimama hapo, akawaambia watu wote: Ninyi hamna kosa lo lote. Nitazameni mimi! Mimi nimemlia bwana wangu njama, nikamwua. Lakini aliyewaua hawa wote ni nani?

10Hapa jueni, ya kuwa hakuna neno lo lote la Bwana, Bwana alilolisema la mlango wa Ahabu, lililoanguka chini, kwani Bwana anayafanya, aliyoyasema kinywani mwa mtumishi wake Elia.[#1 Fal. 21:22.]

11Ndipo, Yehu alipowaua wote waliosalia wa mlango wa Ahabu huko Izireeli nao wakuu wake wote na rafiki zake wote na watambikaji wake wote, kwao hakusazwa hata mmoja aliyepona.

12Kisha akaondoka, akaenda Samaria. Alipofika njiani penye nyumba, wachungaji walimokatia manyoya ya kondoo,

13Yehu akawakuta ndugu zake Ahazia, mfalme wa Wayuda, akawauliza: Ninyi wa nani? Wakajibu: Sisi ndugu zake Ahazia, tukashuka kuamkiana nao wana wa mfalme na wana wa bibi wake mfalme.[#2 Mambo 22:8.]

14Ndipo, alipoagiza: Wakamateni hivyo, walivyo hai! Wakawakamata hivyo, walivyokuwa hai, wakawachinja hapo penye kisima cha hiyo nyumba, walimokatia manyoya ya kondoo, watu 42, hakusaza hata mmoja wao.

15Alipoondoka huko, akamkuta Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyekuja kuonana naye, akamwuliza: Moyo wako unanielekea, kama moyo wangu unavyouelekea moyo wako? Yonadabu alipojibu: Ndio, akasema: Kama ndivyo, nipe mkono wako! Alipompa mkono wake akampandisha garini mwake,[#Yer. 35:6.]

16akamwambia: Twende pamoja, uone wivu wangu, nilio nao kwa ajili ya Bwana! Kisha akaenda naye garini mwake.

17Alipofika Samaria, akawaua wote waliosalia huko Samaria wa mlango wa Ahabu, mpaka akiwaangamiza kabisa kwa lile neno la Bwana, alilomwambia Elia.[#1 Fal. 21:21-22.]

Yehu anayakomesha matambiko ya Baali.

18Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia: Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini Yehu atamtumikia kabisa.[#1 Fal. 16:31-33.]

19Sasa waiteni wafumbuaji wote wa Baali na watumishi wake wote na watambikaji wake wote, waje kwangu, asikoseke hata mmoja! Kwani ninataka kumtolea Baali ng'ombe nyingi za tambiko; kila atakayekoseka hatapona. Lakini Yehu aliyafanya haya kwa ujanja, kusudi apate kuwaangamiza wamtumikiao Baali.

20Kisha Yehu akawaambia: Takaseni mkutano wa kumtambikia Baali! Walipoutangaza,

21Yehu akatuma kwa Waisiraeli wote, wakaja wote waliomtumikia Baali, hakusalia hata mmoja asiyekuja. Kisha wakaingia nyumbani mwa Baali, nayo hiyo nyumba ya Baali ikajaa watu huku na huko.

22Kisha akamwagiza msimamizi wa nguo za watu wa mfalme: Wape wote wanaomtumikia Baali kila mmoja vazi moja. Huyu alipokwisha kuwapa hayo mavazi,

23Yehu akaingia nyumbani mwa Baali pamoja na Yonadabu, mwana wa Rekabu, akawaambia wanaomtumikia Baali: Chunguzeni na kutazama, kusiweko huku kwenu na watumishi wa Bwana, ila wawe wao peke yao wanaomtumikia Baali![#2 Fal. 10:15.]

24Kisha wakaja kutoa vipaji vya tambiko na ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Lakini Yehu alikuwa amejiwekea nje watu 80, akawaambia: Mtu atakayepona kwao hao, nitakaowaleta na kuwatia mikononi mwenu, basi, roho yake itakuwa mahali pa roho yake yule.[#1 Fal. 20:39.]

25Walipokwisha kuzitoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, Yehu akawaambia wale wapiga mbio na wakuu wa askari thelathini: Ingieni, mwaue, mtu hata mmoja asipate kutoka! Ndipo, wale wapiga mbio na wakuu wa askari thelathini walipowaua kwa ukali wa panga, wakawatupa nje; kisha wakaingia mle ndani nyumbani mwa Baali,[#1 Fal. 18:40.]

26wakazitoa nguzo za kutambikia mle nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.[#2 Fal. 11:18.]

27Kisha wakaivunjavunja ile nguzo ya mawe ya kumtambikia Baali, nayo nyumba ya Baali wakaivunjavunja, wakaitumia kuwa mahali pa vyoo hata siku hii ya leo.[#2 Fal. 3:2.]

28Ndivyo, Yehu alivyoyakomesha matambiko ya Baali kwao Waisiraeli.

Mwisho wa mambo ya Yehu.

29Lakini makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, Yehu hakuacha kuyafuata akizitambikia ndama za dhahabu zilizowekwa Beteli na Dani.[#1 Fal. 12:26-33.]

30Bwana akamwambia Yehu: Kwa kuwa umetenda vema ukiyafanya yanyokayo machoni pangu, tena ukiufanyizia mlango wa Ahabu yote yaliyokuwamo moyoni mwangu, kwa hiyo wanao wa vizazi vinne watakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli.[#2 Fal. 15:12.]

31Lakini Yehu hakuangalia kuendelea na kuyashika Maonyo ya Bwana Mungu wa Isiraeli kwa moyo wake wote, wala hakuyaacha makosa ya Yeroboamu aliyewakosesha Waisiraeli.

32Siku hizo Bwana akaanza kuikatakata nchi ya Waisiraeli, Hazaeli akawapiga Waisiraeli po pote penye mipaka,[#2 Fal. 8:12.]

33akaichukua nchi yote ya Gileadi iliyoko ng'ambo ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, ndiyo nchi ya Gadi na ya Rubeni na ya Manase kutoka Aroeri ulioko kwenye mto wa Arnoni, hata Gileadi na Basani.

34Mambo mengine ya Yehu nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yote ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

35Yehu alipokuja kulala na baba zake, wakamzika Samaria, naye mwanawe Yoahazi akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 13:1.]

36Nazo siku, Yehu alizokuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria, ni miaka 28.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania