2 Wafalme 11

2 Wafalme 11

Ufalme wa Wayuda: Ubaya wa Atalia na kuuawa kwake.

(Taz. 2 Mambo 22:10—23:21.)

1Atalia, mamake Ahazia, alipoona, ya kuwa mwanawe amekufa, akaondoka, akawaangamiza wazao wote wa kifalme.[#2 Fal. 8:26; 9:27.]

2Lakini Yoseba, binti mfalme Yoramu, umbu lake Ahazia, akamchukua Yoasi, mwana wa Ahazia, akamwiba katikati ya wana wa mfalme waliokwenda kuuawa, akamweka pamoja na mnyonyeshaji wake katika chumba cha kulalia. Ndivyo, alivyomficha, Atalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa.

3Akakaa naye na kufichwa Nyumbani mwa Bwana miaka sita, Atalia alipokuwa mfalme wa kike wa nchi hiyo.

4Katika mwaka wa saba Yoyada akatuma kuwachukua wakuu wa mamia ya askari na wapiga mbio, akawapeleka kwake Nyumbani mwa Bwana, akafanya maagano nao akiwaapisha mle Nyumbani. Kisha akawaonyesha mwana wa mfalme,

5akawaagiza kwamba: Hili ndilo neno, mtakalolifanya: fungu lenu la tatu watakaoingia kazi siku ya mapumziko na walinde ulinzi wa nyumba ya mfalme;

6fungu jingine la tatu na walinde penye lango la Suri, nalo fungu jingine la tatu na walinde langoni nyuma ya wapiga mbio! Ndivyo, mtakavyolinda ulinzi wa hiyo nyumba na kuzuia watu.

7Navyo vikosi vyenu viwili watakaotoka kazini siku ya mapumziko, wote sharti walinde ulinzi wa Nyumba ya Bwana kwake mfalme!

8Sharti mmzunguke mfalme pande zote kila mtu akiyashika mata yake, kila atakayeingia katika hii mipango ya watu na auawe! Hivyo sharti mwe na mfalme, akitoka, hata akiingia.

9Wakuu wa mamia wakayafanya yote, kama mtambikaji Yoyada alivyowaagiza; kila mtu akawachukua watu wake walioingia kazi siku ya mapumziko nao waliotoka kazi siku ya mapumziko, wakaja kwa mtambikaji Yoyada.

10Kisha huyu mtambikaji akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao za mfalme Dawidi zilizokuwamo Nyumbani mwa Bwana.[#2 Sam. 8:7.]

11Wakawapanga wapiga mbio, kila mtu na mkuki wake mkononi mwake kuanzia upande wa kuume wa Nyumba kuufikia upande wa kushoto wa Nyumba, kuifikia meza ya kutambikia na tena kuifikia Nyumba yenyewe, wamzunguke mfalme pande zote.

12Kisha akamtoa mwana wa mfalme, akamvika kilemba cha kifalme, wakampa nacho kizingo cha Ushahidi, wakamfanya kuwa mfalme wakimpaka mafuta. Kisha wakapiga makofi na kusema: Pongezi, mfalme![#5 Mose 17:18-19.]

13Atalia alipozisikia sauti za wapiga mbio na za watu, akaja naye hapo, watu walipokuwa, penye Nyumba ya Bwana.

14Alipotazama, akamwona mfalme, akisimama katika ulingo kama desturi, nao wakuu na wapiga matarumbeta wakisimama kwake mfalme, nao watu wote wa nchi yao wakawa wenye furaha na kupiga matarumbeta. Ndipo, Atalia alipoyararua mavazi yake na kupiga kelele kwamba: Mmedanganyika! Mmedanganyika!

15Ndipo, mtambikaji Yoyada alipowaagiza wakuu wa mamia waliovisimamia vikosi, akawaambia: Mtoeni hapa penye mipango ya watu! Naye atakayemfuata na auawe kwa upanga! Kwani mtambikaji alisema, asiuawe Nyumbani mwa Bwana.

16Wakamkamata kwa mikono, naye alipofika penye njia, farasi waliyoishika ya kuingia nyumbani mwa mfalme, akauawa hapo.[#Neh. 3:28.]

Waisiraeli wanarudi kwake Mungu.

17Kisha Yoyada akafanya agano na Bwana, yeye na mfalme wa watu, wawe ukoo wake Bwana; agano jingine akamfanyia mfalme na watu.

18Ndipo, watu wote wa nchi hiyo walipoiingia nyumba ya Baali, wakaibomoa, nazo meza za kumtambikia na vinyago vyake wakavivunjavunja kabisa, naye Matani, mtambikaji wa Baali, wakamwua mbele ya meza za kutambikia. Kisha yule mtambikaji akaweka wakaguzi wa Nyumba ya Bwana.[#2 Fal. 10:26-27; Amu. 6:25.]

19Kisha akawachukua wakuu wa mamia nao askari nao wapiga mbio pamoja na watu wote wa nchi hii, wakamtoa mfalme Nyumbani mwa Bwana, wakaingia nyumbani mwa mfalme na kushika njia ya lango la wapiga mbio; ndivyo, alivyopata kukaa katika kiti cha kifalme cha wafalme.

20Nao watu wote wa nchi hii wakafurahi, nao mji ukatulia. Lakini Atalia walikuwa wamemwua kwa upanga nyumbani mwa mfalme.

21Naye Yoasi alikuwa mwenye miaka saba alipoupata ufalme.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania