The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa 7 wa Yehu Yoasi akawa mfalme, akaushika ufalme mle Yerusalemu miaka 40, nalo jina la mama yake ni Sibia wa Beri-Seba.
2Yoasi akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana siku zake zote, mtambikaji Yoyada alizomfundisha.
3Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu wakaendelea bado kutoa ng'ombe za tambiko na kuvukiza vilimani pa kutambikia.[#1 Fal. 22:44; 2 Fal. 14:4.]
4Yoasi akawaambia watambikaji: Fedha zote zinazoletwa Nyumbani mwa Bwana, ziwe mali za Bwana, kama ni fedha, mtu anazozitoa mwenyewe, au kama ni fedha za kujikomboa, fedha zo zote, mtu atakazowaza moyoni mwake kuzipeleka Nyumbani mwa Bwana,
5watambikaji na wajitwalie kila mtu kwao, anaojuana nao. Kisha wao wenyewe wapatengeneze, Nyumba ilipobomoka, po pote panapoonekana palipobomoka.
6Lakini katika mwaka wa 23 wa mfalme Yoasi watambikaji walikuwa hawajapatengeneza bado, Nyumba ilipobomoka.
7Ndipo, mfalme Yoasi alipomwita mtambikaji Yoyada na watambikaji wengine, akawaambia: Mbona hamjapatengeneza, Nyumba ilipobomoka? Sasa msijitwalie fedha kwao, mnaojuana nao, ila sharti mzitoe za kupatengeneza, Nyumba ilipobomoka.
8Watambikaji wakaitikia, wasijitwalie tena fedha kwa watu, wala wasipatengeneze wao, Nyumba ilipobomoka.
9Ndipo, mtambikaji Yoyada alipochukua kasha moja, akatoboa tundu katika kifuniko chake, akaliweka penye meza ya kutambikia kuumeni kwake pa kuingia Nyumbani mwa Bwana; ndimo, watambikaji waliolinda vizingiti walimotia fedha zote zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana.
10Walipoona, ya kuwa fedha zimo nyingi mle kashani, mwandishi wa mfalme na mtambikaji mkuu wakapanda, wakazifunga na kuzihesabu fedha zote zilizooneka Nyumbani mwa Bwana.
11Fedha zilipokwisha kupimwa zikatiwa mikononi mwao wenye kazi hiyo waliowekwa kuisimamia Nyumba ya Bwana; nao wakazitumia kuwalipa maseremala na mafundi wengine walioijenga Nyumba ya Bwana,
12kama waashi na wachonga mawe. Tena walizitumia za kununua miti na mawe ya kuchonga ya kupatengeneza, Nyumba ya Bwana ilipobomoka, na kuvilipa vyote vingine vilivyotakiwa vya kuitengeneza Nyumba ya Bwana.
13Lakini mabakuli ya fedha na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na matarumbeta na vyombo vyo vyote vya dhahabu na vya fedha vya kutumiwa Nyumbani mwa Bwana havikutengenezwa kwa zile fedha zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana.
14Kwani waliozipata ni wale tu waliofanya kazi za kuitengeneza Nyumba ya Bwana,
15Nao hao, waliowapa hizo fedha mikononi mwao, wawalipe wafanya kazi, hawakuzihesabu nao, kwani walifanya kazi zao kwa welekevu.[#2 Fal. 22:7.]
16Fedha za tambiko la weuo nazo fedha za tambiko la upozi hazikupelekwa Nyumbani mwa Bwana, zilikuwa mali za watambikaji.
17Siku zile Hazaeli, mfalme wa Ushami, akapanda, akapiga vita huko Gati; alipokwisha kuuteka, Hazaeli akaulekeza uso wake kuupandia Yerusalemu.[#2 Fal. 10:32.]
18Ndipo, Yoasi, mfalme wa Wayuda, alipovichukua vipaji vitakatifu vyote, Yosafati na Yoramu na Ahazia walivyovitoa, viwe mali za Bwana, na vipaji vitakatifu, alivyovitoa yeye, nazo dhahabu zote zilizopatikana katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana namo katika vilimbiko vya nyumba ya mfalme, akampelekea Hazaeli, mfalme wa Ushami; ndipo, alipoondoka Yerusalemu.[#1 Fal. 15:18.]
19Mambo mengine ya Yoasi, nayo yote aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
20Watumishi wake wakamwinukia na kumlia njama, kisha wakamwua Yoasi katika boma la Milo panapotelemkia silo.[#2 Fal. 14:5.]
21Watumishi wake, Yozakari, mwana wa simati, na Yozabadi, mwana wa someri, ndio waliomwua; alipokufa, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Amasia akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 14:1.]