The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa 23 wa Yoasi, mwana wa Ahazia, mfalme wa Wayuda, Yoahazi, mwana wa Yehu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria miaka 17.[#2 Fal. 10:35.]
2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akayafuata makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Asipoyaepuka,[#1 Fal. 12:26-33.]
3makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli, mfalme wa Ushami, namo mkononi mwa Benihadadi, mwana wa Hazaeli, siku zote.[#2 Fal. 10:32.]
4Lakini Yoahazi alipokuwa anamlalamikia Bwana, Bwana akamsikia, kwani aliyaona masongano ya Waisiraeli, kwa kuwa mfalme wa Ushami aliwasonga.
5Ndipo, Bwana alipowapa Waisiraeli mwokozi, wakatoka mikononi mwa Washami, wana wa Isiraeli wakapata kukaa tena mahemani kwao kama huko kale,[#2 Fal. 14:27.]
6Lakini hawakuyaepuka makosa ya mlango wa Yeroboamu aliyewakosesha Waisiraeli, ila wakaendelea kuyafanya, nacho kinyago cha Ashera kilisimama bado mle Samaria.[#1 Fal. 16:33.]
7Kwa hiyo Bwana hakusaza kwa Yoahazi watu wa kupiga vita, ni wapanda farasi 50 na magari 10 na watu 10000 waliokwenda kwa miguu, kwani mfalme wa Ushami aliwaangamiza na kuwafananisha na uvumbi ulioko kwenye kupuria.
8Mambo mengine ya Yoahazi nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?
9Yoahazi alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika Samaria, naye mwanawe Yoasi akawa mfalme mahali pake.
10Katika mwaka wa 37 wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, Yoasi, mwana wa Yoahazi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria miaka 16.
11Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, ila akaendelea kuyafanya.[#2 Fal. 13:2.]
12Mambo mengine ya Yoasi nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yenye nguvu, aliyoyatenda alipopiga vita na Amasia, mfalme wa Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?[#2 Fal. 14:8-16.]
13Yoasi alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha kifalme, naye Yoasi akazikwa Samaria kwao wafalme wa Waisiraeli.[#2 Fal. 14:23.]
14Elisa alipopata ugonjwa wake uliomwua, ndipo, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, aliposhuka kuja kwake, akalia machozi mbele yake na kusema: Baba yangu! Baba yangu! Wewe gari la Waisiraeli na wapanda farasi wake![#2 Fal. 2:12.]
15Elisa akamwambia: Chukua upindi na mishale! Basi, akajichukulia upindi na mishale.
16Kisha akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Shika upindi mkononi mwako! Alipoushika mkononi mwake, Elisa akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17Kisha akamwambia: Fungua dirisha upande wa maawioni kwa jua! Alipoifungua, Elisa akamwambia: Piga mshale! Alipopiga mshale, akasema: Huu ni mshale wa wokovu wa Bwana, ndio mshale wa kuokoa mikononi mwa Washami. Utawapiga Washami kule Afeki, hata uwamalize.
18Kisha akasema: Chukua mishale! Alipoichukua, akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Ipige nchi! Akaipiga mara tatu, kisha akasimama.
19Ndipo, yule mtu wa Mungu alipomkasirikia, akamwambia: Ungaliipiga mara tano au mara sita, ungaliwapiga Washami, hata uwamalize kabisa. Lakini sasa utawapiga Washami mara tatu tu.
20Elisa alipokwisha kufa, wakamzika. Hapo vikosi vya Wamoabu wakaingia katika nchi hii, nao wakaja kila mwaka.
21Ikawa, walipotoka, waende kuzika mtu, mara wakaona kikosi; kwa hiyo wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisa. Lakini yule mtu alipofika ndani na kuigusa mifupa ya Elisa, mara akawa mzima tena, akaweza kusimama miguuni pake.
22Hazaeli, mfalme wa Washami, alikuwa akiwasonga Waisiraeli siku zote za Yoahazi.
23Kisha Bwana akawawia mpole tena na kuwahurumia, akawaelekea kwa ajili ya Agano lake, alilomwekea Aburahamu na Isaka na Yakobo; kwa hiyo hakutaka kuwaangamiza kabisa, wala hakuwatupa mpaka siku hizo waondoke usoni pake.[#3 Mose 26:42.]
24Hazaeli, mfalme wa Washami, alipokufa, mwanawe Benihadadi akawa mfalme mahali pake.
25Ndipo, Yoasi, mwana wa Yoahazi, alipoichukua tena ile miji mkononi mwa Benihadadi, mwana wa Hazaeli, baba yake aliyoichukua vitani mkononi mwa Yoahazi. Yoasi alipokwisha kumpiga mara tatu, alikuwa ameirudisha ile miji ya Waisiraeli.[#2 Fal. 10:32-33; 13:19.]