2 Wafalme 14

2 Wafalme 14

Ufalme wa Wayuda: Mfalme Amasia.

(1-22: 2 Mambo 25-26:2.)

1Katika mwaka wa 2 wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Waisiraeli, Amasia, mwana wa Yoasi, akapata kuwa mfalme wa Wayuda.[#2 Fal. 12:21.]

2Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 29. Jina la mama yake ni Yoadani wa Yerusalemu.

3Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, lakini hakuwa kama baba yake Dawidi; naye akayafanya yote, baba yake Yoasi aliyoyafanya.[#2 Fal. 12:2-3.]

4Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia.[#2 Fal. 15:4.]

5Ikawa, ufalme ulipopata kushupaa mkononi mwake, akawaua watumishi wake waliomwua baba yake mfalme.[#2 Fal. 12:20-21.]

6Lakini wana wao wale wauaji hakuwaua, kwa kuwa imeandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, Bwana aliyomwagiza kwamba: Baba wasiuawe kwa ajili ya wana, wala wana wasiuawe kwa ajili ya baba, ila kila mtu na auawe kwa kosa lake yeye![#5 Mose 24:16.]

7Naye ndiye aliyewapiga Waedomu watu 10000 katika Bonde la Chumvi, akauteka nao mji wa Sela katika vita hivyo, akauita jina lake Yokiteli mpaka siku hii ya leo.

8Kisha Amasia akatuma wajumbe kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Waisiraeli, kumwambia: Njoo, tuonane uso kwa uso!

9Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akatuma wajumbe kwa Amasia, mfalme wa Wayuda, kwamba: Kingugi kilichoko Libanoni kilituma kwa mwangati ulioko Libanoni kwamba: Mpe mwanangu mwanao wa kike, awe mkewe! Ndipo, nyama wa porini wa huko Libanoni alipopita, akakikanyaga kile kingugi na kukiponda.[#Amu. 9:14.]

10Kwa kuwa umewapiga Waedomu, moyo wako unakukuza; jitutumue, lakini kaa nyumbani mwako! Mbona unataka kujitia katika vita vibaya, uanguke wewe na Wayuda pamoja nawe?

11Lakini Amasia hakusikia; ndipo, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, alipopanda, wakaonana uso kwa uso, yeye na Amasia, mfalme wa Wayuda, huko Beti-Semesi katika nchi ya Wayuda.

12Wayuda wakashindwa na Waisiraeli, wakakimbia kila mtu hemani kwake.

13Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akamkamata Amasia, mfalme wa Wayuda, aliyekuwa mwana wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, kule Beti-Semesi, kisha akaja Yerusalemu, akalivunja boma la Yerusalemu toka lango la Efuraimu hata lango la pembeni, ndio mikono 400.

14Akachukua dhahabu na fedha zote, navyo vyombo vyote vilivyopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme nao watu, aliowataka kuwa kole, kisha akarudi Samaria.

15Mambo mengine ya Yoasi aliyoyafanya na matendo yake yenye nguvu aliyoyatenda alipopiga vita na Amasia, mfalme wa Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

16Yoasi alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa Samaria kwa wafalme wa Waisiraeli, naye mwanawe Yeroboamu akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 13:13.]

17Naye Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, akawapo tena miaka 15 baada ya kufa kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Waisiraeli.

18Mambo mengine ya Amasia hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?

19Walipomlia njama mle Yerusalemu, akakimbilia Lakisi; ndipo, walipotuma watu kumfuata huko Lakisi, wakamwua huko.[#2 Fal. 12:20-21; 21:23.]

20Wakamchukua kwa farasi, akazikwa mle Yerusalemu kwa baba zake mjini mwa Dawidi.[#2 Fal. 9:28.]

21Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria aliyekuwa mwenye miaka 16, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Amasia.[#2 Fal. 15:1-2.]

22Yeye akaujenga Elati, akaurudisha kwao Wayuda, mfalme alipokuwa amelala na baba zake.[#2 Fal. 16:6.]

Ufalme wa Waisiraeli: Mfalme Yeroboamu.

23Katika mwaka wa 15 wa Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, Yeroboamu, mwana wa Yoasi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 41.[#2 Fal. 14:16; Hos. 1:1; Amo. 1:1.]

24Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 12:26-33.]

25Yeye akairudisha mipaka ya Waisiraeli toka Hamati mpaka kwenye bahari ya nyikani, kama Bwana Mungu wa Isiraeli alivyosema kinywani mwa mtumishi wake mfumbuaji Yona, mwana wa Amitai, wa Gati-Heferi.[#Yona 1:1.]

26Kwani Bwana aliyaona mateso ya Waisiraeli yaliyokuwa yenye machungu sana, akaona, ya kuwa waliofungwa nao waliofunguliwa wanamalizika, kwa kuwa hakuwako aliyewasaidia Waisiraeli.[#5 Mose 32:36.]

27Naye Bwana alikuwa hajasema, ya kuwa atalifuta jina la Isiraeli, litoweke chini ya mbingu, kwa hiyo akawasaidia kwa mkono wa Yeroboamu, mwana wa Yoasi.[#2 Fal. 13:5.]

28Mambo mengine ya Yeroboamu, nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yaliyokuwa yenye nguvu, alipopiga vita, tena jinsi alivyoirudisha kwa Waisiraeli miji ya Damasko na ya Hamati iliyokuwa kale ya Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

29Yeroboamu alipokwenda kulala na baba zake wafalme wa Waisiraeli, mwanawe Zakaria akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 15:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania