The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa 27 wa Yeroboamu, mfalme wa Waisiraeli, Azaria, mwana wa Amasia, akapata kuwa mfalme wa Wayuda.[#2 Fal. 14:21.]
2Alikuwa mwenye miaka 16 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 52. Jina la mama yake ni Yekolia wa Yerusalemu.
3Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Amasia aliyoyafanya.
4Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia.[#2 Fal. 14:3-4.]
5Bwana akampiga mfalme, akawa mwenye ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya wagonjwa waliotengwa, naye mwanawe Yotamu akawa mkuu nyumbani mwa mfalme, akawaamua watu wa nchi hii.[#3 Mose 13:46.]
6Mambo mengine ya Azaria nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
7Azaria alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Yotamu akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 15:32.]
8Katika mwaka wa 38 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Zakaria, mwana wa Yeroboamu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miezi 6.[#2 Fal. 14:29.]
9Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba zake walivyofanya, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 12:26-33.]
10Salumu, mwana wa Yabesi, akamlia njama, akampiga machoni pa watu, akamwua, akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 15:14; Amo. 7:9.]
11Mambo mengine ya Zakaria tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli.
12Hapo limetimia lile neno la Bwana, alilomwambia Yehu kwamba: Wanao wa vizazi vinne watakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Ikawa hivyo.[#2 Fal. 10:30.]
13Salumu, mwana wa Yabesi, akapata kuwa mfalme katika mwaka wa 39 wa Uzia, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme mle Samaria siku za mwezi mmoja.
14Ndipo, Menahemu, mwana wa Gadi, wa Tirsa, alipopanda, akaingia Samaria, akampiga Salumu, mwana wa Yabesi, mle Samaria, akamwua, akawa mfalme mahali pake.[#1 Fal. 16:17.]
15Mambo mengine ya Salumu nayo njama yake, aliyomlia mfalme, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli.
16Siku zile Menahemu akaupiga mji wa Tifusa nao wote waliokuwamo na mipakani kwake toka Tirsa; kwa kuwa hawakumfungulia lango la mji, akawaua, nao wanawake waliokuwa wenye mimba akawatumbua.
17Katika mwaka wa 39 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Menahemu, mwana wa Gadi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 10.
18Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, siku zake zote hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#2 Fal. 15:9.]
19Puli, mfalme wa Asuri, alipijia nchi hiyo, ndipo, Menahemu alipompa Puli vipande vya fedha 1000, ndio shilingi milioni 12, kusudi amsaidie kwa mikono yake kuushupaza ufalme wake mkononi mwake.
20Kisha Menahemu akawatoza Waisiraeli hizo fedha kwa kwamba: Kwao wenye mali kila mmoja ampe mfalme wa Asuri vipande vidogo vya fedha 50, ndio shilingi 200. Kisha mfalme wa Asuri akarudi, hakukaa huko katika nchi hiyo.[#2 Fal. 23:35.]
21Mambo mengine ya Menahemu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?
22Menahemu alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Pekaya akawa mfalme mahali pake.
23Katika mwaka wa 50 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Pekaya, mwana wa Menahemu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 2.
24Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#2 Fal. 15:9.]
25Peka, mwana wa Remalia, mkuu wake wa askari 30 akamlia njama, akamwua pamoja na Argobu na Arie huko Samaria katika jumba kubwa lililokuwa nyumba ya mfalme, hata watu 50 wa wana wa Gileadi walikuwa naye. Alipokwisha kumwua akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 15:10,14,30.]
26Mambo mengine ya Pekaya nayo yote, aliyoyafanya, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli.
27Katika mwaka wa 52 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Peka, mwana wa Remalia, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 20.
28Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#2 Fal. 15:9.]
29Siku za Peka, mfalme wa Waisiraeli, akaja Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri, akaiteka miji ya Iyoni na Abeli-Beti-Maka na Yanoa na Kedesi na Hasori na Gileadi na Galila, ndiyo nchi yote ya Nafutali, nao watu akawahamisha kwenda Asuri.[#1 Mambo 5:26.]
30Ndipo, Hosea, mwana wa Ela, alipomlia njama Peka, mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, kisha akawa mfalme mahali pake katika mwaka wa 20 wa Yotamu, mwana wa Uzia.[#2 Fal. 15:25; 17:1.]
31Mambo mengine ya Peka nayo yote, aliyoyafanya, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli.
32Katika mwaka wa 2 wa Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Waisiraeli, Yotamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme.[#2 Fal. 15:5,7.]
33Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 16. Jina la mama yake ni Yerusa, binti Sadoki.
34Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Uzia aliyoyafanya.[#2 Fal. 15:3-4.]
35Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia. Yeye ndiye aliyelijenga lango la juu la Nyumba ya Bwana.
36Mambo mengine ya Yotamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
37Siku zile Bwana akaanza kumtuma Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, waijie nchi ya Yuda.[#2 Fal. 16:5.]
38Yotamu alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Ahazi akawa mfalme mahali pake.