2 Wafalme 16

2 Wafalme 16

Mfalme Ahazi.

(Taz. 2 Mambo 28.)

1Katika mwaka wa 17 wa Peka, mwana wa Remalia, Ahazi, mwana wa Yotamu, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme.[#2 Fal. 15:38.]

2Ahazi alikuwa mwenye miaka 20 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 16. Hakuyafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi,

3ila akaendelea kuzishika njia za wafalme wa Waisiraeli, hata mwanawe akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni akiyafuata hayo matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele yao Waisiraeli.[#2 Fal. 21:6; 3 Mose 18:21.]

4Akatambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia napo pengine palipoinukia juu, hata chini yake kila mti uliokuwa wenye majani mengi.

5Hapo Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Waisiraeli, wakaupandia Yerusalemu kupiga vita, wakamsonga Ahazi kwa kumzinga, lakini hawakuweza kumshinda vitani.[#Yes. 7:1-9.]

6Wakati huo Resini, mfalme wa Ushami, akaurudisha mji wa Elati kwa Washami, nao Wayuda akawafukuza mle Elati; ndipo, washami wlipokuja kukaa Elati, wakakaa humo mpaka siku hii ya leo.[#2 Fal. 14:22.]

7Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri, kumwambia: Mimi ni mtumwa wako na mtoto wako; panda, uniokoe mkononi mwa mfalme wa Ushami namo mkononi mwa mfalme wa Waisiraeli walioniinukia![#2 Fal. 15:29.]

8Ahazi akazichukua fedha na dhahabu zilizopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, akazituma kwa mfalme wa Asuri kuwa matunzo.[#1 Fal. 15:18.]

9Mfalme wa Asuri akamwitikia; kisha mfalme wa Asuri akaupandia mji wa Damasko, akauteka, nao watu akawahamisha kwenda Kiri, lakini Resini akamwua.

10Mfalme Ahazi akaenda Damasko kuonana na Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri. Alipoiona meza ya kutambikia iliyoko Damasko mfalme Ahazi akatuma mfano wa hiyo meza ya kutambikia kuionyesha namna yake, ilivyotengenezwa kazi zake zote, akaupeleka kwa mtambikaji Uria.

11Ndipo, mtambikaji Uria alipojenga kutambikia, pote pawe sawa na ule mfano, mfalme Ahazi alioutuma toka Damasko; ndivyo, mtambikaji Uria alivyovifanya, mfalme Ahazi alipokuwa hajarudi bado toka Damasko.

12Mfalme aliporudi toka Damasko, mfalme akaiona hiyo meza ya kutambikia; ndipo, mfalme alipoikaribia hiyo meza ya kutambikia, akateketeza juu yake ng'ombe ya tambiko

13pamoja na kuivukizia na kutoa vilaji vya tambiko, akaimwagia vinywaji vya tambiko nazo damu za ng'ombe za tambiko za shukrani, alizozitoa kuzinyunyizia ile meza ya kutambikia.

14Nayo ile meza ya shaba ya kutambikia iliyokuwako mbele ya Bwana akaiondoa mahali pake mbele ya Nyumba, isiwe tena katikati ya hiyo meza mpya ya kutambikia na Nyumba ya Bwana, akaiweka upande wa kaskazini wa hiyo meza mpya ya kutambikia.

15Kisha mfalme Ahazi akamwagiza mtambikaji Uria kwamba: Katika hii meza kubwa utachoma ng'ombe za tambiko za asubuhi na vilaji vya tambiko vya jioni na ng'ombe za tambiko za mfalme na vilaji vyake vya tambiko na ng'ombe za tambiko za watu wote wa nchi hii na vilaji vyao vya tambiko na vinywaji vyao vya tambiko, nazo damu zote za ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima nazo damu za ng'ombe nyingine za tambiko uinyunyizie. Nayo mambo ya ile meza ya shaba ya kutambikia nitayafikiri, yatakavyokuwa.

16Mtambikaji Uria akayafanya yote, kama mfalme Ahazi alivyomwagiza.

17Mfalme Ahazi akavivunja navyo vibao vya kufungia vya vile vilingo, akaiondoa nayo ile mitungi ya shaba iliyowekwa humo, nayo bahari ya shaba akaiondoa juu ya zile ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya mawe yaliyopangwa.[#1 Fal. 7:23-39.]

18Nao ukumbi wa siku ya mapumziko, walioujenga penye Nyumba hiyo, nao mlango wa nje wa kuingilia mfalme akauondoa na kuuweka pengine penye Nyumba hiyo kwa ajili ya mfalme wa Asuri.

19Mambo mengine ya Ahazi, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?

20Ahazi alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Hizikia akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 18:1.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania