2 Wafalme 18

2 Wafalme 18

Ufalme wa Wayuda: Mfalme Hizikia.

1Katika mwaka wa 3 wa Hosea, mwana wa Ela, mfalme wa Waisiraeli, Hizikia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme.[#2 Fal. 16:20.]

2Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miake 29; jina la mama yake ni Abi, binti Zakaria.[#2 Mambo 29:1-2.]

3Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Dawidi aliyoyafanya.[#2 Fal. 20:3.]

4Yeye akayakomesha matambiko ya vilimani, akazivunja nguzo za mawe za kutambikia, navyo vinyago vya Ashera akavikatakata, nayo ile nyoka ya shaba, Mose aliyoitengeneza, akaipondaponda, kwani mpaka siku hizo wana wa Isiraeli walikuwa wakiivukizia na kuiita Nehustani (Kinyago cha Shaba).[#2 Mambo 31:1; 2 Fal. 15:35; 4 Mose 21:8-9.]

5Akamwegemea Bwana Mungu wa Isiraeli; hakuwako mwingine aliyekuwa kama yeye, wala miongoni mwao wafalme waliomfuata, wala miongoni mwao waliomtangulia.[#2 Fal. 23:25.]

6Akagandamana na Bwana, hakuacha kabisa kumfuata, akayaangalia maagizo yake Bwana, aliyomwagiza Mose.

7Bwana akawa naye, akafanikiwa po pote, alipotoka kufanya kitu; naye mfalme wa Asuri akamkataa akiacha kumtii na kumtumikia.

8Nao Wafilisti akawapiga, hata mji wa Gaza na mipaka yake kutoka kwenye mnara wa walinzi hata mjini mwenye boma.

Ufalme wa Waisiraeli unaangamizwa, watu wanahamishwa Asuri.

9Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Hizikia, ndio mwaka wa saba wa Hosea, mwana wa Ela, mfalme wa Waisiraeli, ndipo, Salmaneseri, mfalme wa Asuri, alipoupandia mji wa Samaria, akausonga kwa kuuzinga.[#2 Fal. 17:3-6.]

10Akauteka baada ya miaka mitatu katika mwaka wa sita wa Hizikia, ndio mwaka wa tisa wa Hosea, mfalme wa Waisiraeli; ndipo, Samaria ulipotekwa.

11Kisha mfalme wa Asuri akawahamisha Waisiraeli kwenda Asuri, akawakalisha katika miji ya Hala, tena Habori penye mto wa Gazoni na katika miji ya Wamedi,

12kwa kuwa hawakuisikia sauti ya Bwana Mungu wao wakalivunja Agano lake, maana yote, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza, hawakuyasikia, wala hawakuyafanya.

Saniheribu analeta vita Yerusalemu.

(13-37: 2 Mambo 32:1-19; Yes. 36.)

13Ikawa katika mwaka wa 14 wa mfalme Hizikia, ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoipandia miji yote ya Wayuda iliyokuwa na maboma, akaiteka.

14Naye Hizikia, mfalme wa Wayuda, akatuma Lakisi kwa mfalme wa Asuri kumwambia: Nimekosa, ondoka kwangu! Nayo, utakayonitoza, basi, nitayachukua, nikupe. Naye mfalme wa Asuri akambandikia Hizikia, mfalme wa Wayuda, kutoa vipande 300 vya fedha, ndio shilingi milioni tatu na nusu na vipande 30 vya dhahabu, ndio shilingi milioni sita na nusu.[#2 Fal. 18:7.]

15Hizikia akampa fedha zote zilizopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme.[#2 Fal. 16:8.]

16Wakati huo Hizikia akayaondoa mabati ya dhahabu penye milango ya Jumba la Bwana, hata penye zile nguzo, alizozifunika kwa mabati ya dhahabu yeye Hizikia, mfalme wa Wayuda, akampa mfalme wa Asuri.

17Lakini mfalme wa Asuri akamtuma mkuu wa vita na mkuu wa watumishi wa nyumbani na mkuu wa askari, watoke Lakisi kwenda Yerusalemu na kikosi kikubwa, wakaupandia, wakafika Yerusalemu. Walipokwisha kupanda na kufika wakasimama kwenye mfereji wa ziwa la juu katika barabara iendayo Shambani kwa dobi.

18Walipomwita mfalme, akawatokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa.

19Mkuu wa askari akawaambia: Mwambieni Hizikia: Hivi ndivyo, anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Asuri: Hilo egemeo, unaloliegemea, ndio nini?

20Unasema maneno ya midomo tu kwamba: Nimekata shauri na kujipa moyo wa kupiga vita. Sasa unamwegemea nani ukinikataa na kuacha kunitii?

21Tazama, egemeo lako, unaloliegemea, ni Misri, hilo fimbo la utete unyongekao! Mtu akilikongojea, litamwingia kiganjani, limchome. Ndivyo, Farao, mfalme wa Misri, anavyowawia wote wamwegemeao.[#Ez. 29:6-7.]

22Mkiniambia: Tunamwegemea Bwana Mungu wetu, basi, yeye siye, ambaye Hizikia aliwakataza watu kumtambikia vilimani pake pa kutambikia, napo penye meza zake za kutambikia, alipowaambia Wayuda na Wayerusalemu: Sharti mmwangukie mbele ya meza hii ya kumtambikia humu Yerusalemu tu?[#2 Mose 20:24; 5 Mose 12:14.]

23Sasa na upinge na bwana wangu, mfalme wa Asuri: nitakupa farasi 2000, kama wewe unaweza kujipatia watu wa kuwapanda.

24Usipowapata utawezaje kuuelekeza nyuma uso wa mwenye amri mmoja tu, ijapo awe mdogo katika watumishi wa bwana wangu? Tena unawaegemea Wamisri, kwa kuwa wako na magari na wapanda farasi.

25Bwana alikuwa hayuko, nilipopapandia sasa mahali hapa, nipaangamize? Bwana ndiye aliyeniambia: Ipandie nchi hii, uiangamize!

26Ndipo, Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Sebuna na Yoa walipomwambia mkuu wa askari: Sema Kishami na watumishi wako! Kwani tunakisikia; usiseme na sisi Kiyuda masikioni pa watu hawa walioko ukutani!

27Mkuu wa askari akawajibu: je? Bwana wangu amenituma kwa bwana wako na kwako kuyasema hayo maneno? Siko kwa watu hawa wanaokaa ukutani watakaokula pamoja nanyi mavi yao na kunywa mikojo yao?

28Kisha mkuu wa askari akatokea, akapaza sauti sana na kusema Kiyuda kwamba: Yasikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Asuri!

29Ndivyo, mfalme anavyosema: Hizikia asiwadanganye! Kwani hataweza kuwaponya ninyi mkononi mwangu!

30Wala Hizikia asiwaegemeze Bwana kwamba: Bwana ndiye atakayetuponya, mji huu usitiwe mkononi mwa mfalme wa Asuri!

31Msimwitikie Hizikia! Kwani hivi ndivyo, mfalme wa Asuri anavyosema: Fanyeni na mimi maagano ya mbaraka, mje kunitokea, mpate kula kila mtu mazao ya mzabibu wake na ya mkuyu wake, mpate kunywa kila mtu maji ya shimo lake mwenyewe,[#1 Fal. 4:25.]

32mpaka nitakapokuja, niwachukue kuwapeleka katika nchi iliyo kama nchi yenu. Nayo ni nchi inayojaa ngano na pombe, ni nchi yenye vyakula na mizabibu, tena ni nchi yenye mafuta ya michekele na asali, mpate kuwapo, msife. Msimwitikie Hizikia! Kwani atawapoteza na kusema: Bwana atatuponya.

33Je? Miungu ya wamizimu iliweza mmoja tu kuiponya nchi yake, isichukuliwe na mfalme wa Asuri?[#Yes. 10:10-11.]

34Ilikuwa wapi miungu ya Hamati na ya Arpadi? Ilikuwa wapi miungu ya Sefarwaimu, nayo yao Hena na Iwa? Hata Samaria haikuweza kuiponya, nisiichukue.

35Katika miungu yote ya nchi hizi ni ipi iliyoweza kuziponya nchi zao, nisizichukue? Basi, Bwana atawezaje kuuponya Yerusalemu,. nisiuchukue?

36Watu wakanyamaza, hawakumjibu neno, kwani mfalme alikuwa amewaagiza kwamba: msimjibu!

37Kisha Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa, wakaja kwa Hizikia wenye nguo zilizoraruliwa, wakamsimulia maneno ya mkuu wa askari.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania