The chat will start when you send the first message.
1Siku zile Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu. Ndipo, mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, alipokuja kwake, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: yaliyo yako yaagizie walio wa mlango wako! Kwani wewe utakufa, hutarudi kuwa mzima tena.
2Akageuka na kuuelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana kwamba:
3E Bwana, na uukumbuke mwenendo, nilioufanya mbele yako kwa welekevu, nikayafanya kwa moyo wote mzima yaliyo mema machoni pako. Kisha Hizikia akalia kilio kikubwa.
4Ikawa, Yesaya alipokuwa hajatokea mjini katikati, ndipo, neno la Bwana lilipomjia kwamba:
5Rudi kumwambia Hizikia aliye mkuu wao walio ukoo wangu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: Nimesikia kuomba kwako, nikayaona nayo machozi yako; na nikuponye, kesho kutwa upate kupanda kuingia Nyumbani mwa Bwana.
6Siku zako nitaziongeza na kukupa tena miaka kumi na mitano. Namo mkononi mwake mfalme wa Asuri nitakuponya, hata mji huu, maana nitaukingia mji huu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi.[#2 Fal. 19:34.]
7Kisha Yesaya akasema: Leteni andazi la kuyu! Wakalileta, wakalibandikia jipu lake, akapata kupona.
8Kisha Hizikia akamwambia Yesaya: Kielekezo changu ndicho nini cha kwamba: Bwana ataniponya, kesho kutwa nipande kuingia Nyumbani mwa Bwana?
9Yesaya akamwambia: Hiki kitakuwa kielekezo chako kitokacho kwa Bwana cha kwamba: Bwana atalifanya neno hili, alilolisema: Unataka nini? Kivuli kiende mbele vipande kumi au kirudi vipande kumi?
10Hizikia akasema: Ni vyepesi, kivuli kusogea vipande kumi, kwa hiyo nataka, kivuli kirudi nyuma vipande kumi.
11Mfumbuaji Yesaya akamlilia Bwana, naye akakirudisha kivuli nyuma vipande vile, kilivyokuwa kimevishuka penye saa ya jua ya Ahazi, navyo vilikuwa vipande kumi.
12Wakati huo Berodaki-Beladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, akatuma barua na matunzo kwake Hizikia, kwani alisikia, ya kuwa Hizikia aliugua.
13Hizikia akawasikiliza, akawaonyesha nyumba yote ya kuwekea mali zake, mlimo na fedha na dhahabu na manukato na mafuta mazuri, na nyumba ya mata yake nayo yote pia yaliyooneka katika vilimbiko vyake. Hakikuwako kitu, ambacho Hizikia hakuwaonyesha, wala nyumbani mwake, wala katika ufalme wake wote.
14Kisha mfumbuaji Yesaya akaja kwa mfalme Hizikia, akamwuliza: Waume hao wamesema nini? Wametoka wapi wakija kwako? Hizikia akajibu: Wametoka nchi ya mbali, wametoka Babeli.
15Akauliza: Wameona nini katika nyumba yako? Hizikia akajibu: Wameyaona yote yaliyomo nyumbani mwangu, hakuna kitu katika vilimbiko vyangu, ambacho sikuwaonyesha.
16Ndipo, Yesaya alipomwambia Hizikia: Sikia neno la Bwana!
17Tazama, ziko siku zitakazokuja, ndipo, yote yaliyomo nyumbani mwako, nayo yote, baba zako waliyoyalimbika hata siku hii ya leo, yatakapopelekwa Babeli, hakitasalia hata kimoja; ndivyo, Bwana anavyosema.[#2 Fal. 24:13-14.]
18Namo katika wanao wa kiume waliotoka mwilini mwako, uliowazaa mwenyewe, watachukuliwa wengine, watumikie jumbani mwa mfalme wa Babeli.[#Dan. 1:3-4.]
19Hizikia akamwambia Yesaya: Neno la Bwana, ulilolisema, ni jema; kisha akasema moyoni: Je? Sivyo, katika siku zangu utakuwako utengemano wa kweli?[#1 Sam. 3:18.]
20Mambo mengine ya Hizikia nayo matendo yake yote ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu nayo, aliyoyafanya ya kutengeneza ziwa na mifereji ya kupeleka maji mjini, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
21Hizikia alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Manase akawa mfalme mahali pake.