2 Wafalme 21

2 Wafalme 21

Mfalme Manase.

(Taz. 2 Mambo 33.)

1Manase alikuwa mwenye miaka 12 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 55 mle Yerusalemu, nalo jina la mama yake ni Hefusiba.

2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyafuata matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli.

3Akavijenga tena vijumba vya kutambikia vilimani, baba yake Hizikia alivyoviangamiza, akaweka nazo meza za kumtambikia Baali, akatengeneza nacho kinyago cha Ashera, kama Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, alivyofanya, akaviangukia navyo vikosi vyote vya mbinguni na kuvitumikia.[#1 Fal. 16:33.]

4Namo Nyumbani mwa Bwana akajenga penginepengine pa kutambikia, namo humo ndimo, Bwana alimosema: Yerusalemu ndimo, Jina langu litakamokaa.[#2 Fal. 21:7.]

5Katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana akajenga pa kuvitambikia vikosi vya mbinguni.[#2 Fal. 23:12.]

6Hata mwanawe akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni, tena akaagulia mawingu, akapiga bao, akatumia nao wakweza mizimu na wapunga pepo, akazidi kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, amkasirishe.[#2 Fal. 16:3.]

7Nacho kinyago cha Ashera, alichokitengeneza, akakiweka katika Nyumba ile, Bwana aliyomwambia Dawidi na mwanawe Salomo: Humu Nyumbani namo Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, nitalikalisha Jina langu kale na kale.[#1 Fal. 8:29; 9:3.]

8Sitaikimbiza tena miguu ya Waisiraeli katika nchi hii, niliyowapa baba zao, wakijiangalia tu na kuyafanya yote, niliyowaagiza, na kuyafuata Maonyo, mtumishi wangu Mose aliyowaagiza.

9Lakini hawakusikia, naye Manase akawaponza kufanya mabaya kuliko wamizimu, Bwana aliowaangamiza mbele ya wana wa Isiraeli.

10Kisha Bwana akasema vinywani mwa watumishi wake wafumbuaji kwamba:

11Kwa kuyafanya hayo matapisho Manase, mfalme wa Wayuda, amefanya mabaya kuliko yote, waliyoyafanya Waamori waliokuwako mbele yake, nao Wayuda akawakosesha kwa kuyatambikia magogo yake.

12Kwa sababu hii Bwana Mungu wa Isiraeli anasema hivi: Mtaniona, nikileta mabaya, yaingie Yerusalemu nako kwa Wayuda, nao watu wote watakaoyasikia masikio yao yote mawili yatawavuma.[#1 Sam. 3:11; Yer. 19:3.]

13Nitautandia Yerusalemu kamba ya kupimia iliyoupima Samaria, niweke nayo mizani iliyoupima mlango wa Ahabu, kisha nitausafisha mji wa Yerusalemu, kama mtu anavyosafisha bakuli, kisha hulifudikiza.

14Nao watakaosalia kwao waliokuwa wangu nitawatupa na kuwatia mikononi mwa adui zao, wanyang'anywe mali zao na kutekwa na adui zao wote,

15kwa kuwa wameyafanya yaliyo mabaya machoni pangu, wakanikasirisha tangu siku ile, baba zao walipotoka huko Misri, hata siku hii ya leo.

16Manase akazidi sana kumwaga damu za watu wasiokosa, akaujaza Yerusalemu hizo damu toka upande huu mpaka upande wa pili; tena kosa lake kubwa lilikuwa hilo la kuwakosesha Wayuda, wayafanye yaliyo mabaya machoni pake Bwana.[#2 Fal. 24:4.]

17Mambo mengine ya Manase nayo yote, aliyoyafanya, na makosa yake, aliyoyakosa, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?

18Manase alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa katika bustani penye nyumba yake, ndio katika bustani ya Uza, naye mwanawe Amoni akawa mfalme mahali pake.

Mfalme Amoni.

19Amoni alikuwa mwenye miaka 22 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 2 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Mesulemeti, binti Harusi, wa Yotiba.

20Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya.

21Akaendelea kuzishika njia zote, alizozishika baba yake, akayatumikia magogo ya kutambikia, baba yake aliyoyatumikia, naye akayaangukia.

22Akamwacha Bwana Mungu wa baba zake, hakuishika njia ya Bwana.

23Ndipo, watumishi wa Amoni walipomlia njama, wakamwua mfalme nyumbani mwake.[#2 Fal. 14:19.]

24Lakini watu wa nchi hiyo wakawaua wote waliomlia mfalme Amoni njama, kisha hao watu wa nchi hiyo wakamfanya mwanawe Yosia kuwa mfalme mahali pake.

25Mambo mengine ya Amoni, aliyoyafanya hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?

26Wakamzika kaburini mwake katika bustani ya uza, naye mwanawe Yosia akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 21:18.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania