The chat will start when you send the first message.
1Yosia alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 31 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Yedida, binti Adaya, wa Boskati.
2Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, akaendelea na kuzishika njia zote za baba yake Dawidi, hakuziacha na kujiendea, wala kuumeni, wala kushotoni.[#5 Mose 5:32; 2 Fal. 18:3.]
3Ikawa katika mwaka wa 18 wa ufalme wake Yosia, ndipo, mfalme alipomtuma mwandishi Safani, mwana wa Asalia, mwana wa Mesulamu, kwenda Nyumbani mwa Bwana akimwambia:
4Nenda kwa mtambikaji mkuu Hilkia, azijumlishe fedha zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana, walinzi wa vizingiti wanazozikusanya kwa watu.
5Kisha wazitie mikononi mwa wenye kazi waliowekwa kuzisimamia kazi za Nyumbani mwa Bwana, nao wawape wazifanyao kazi hizo za Nyumbani mwa Bwana za kupatengeneza, Nyumba ilipobomoka,
6maseremala na mafundi wengine na waashi, tena wazitumie za kununua miti na mawe ya kuchonga ya kuitengeneza hiyo Nyumba.
7Lakini wakipewa hizo fedha mikononi mwao, zisihesabiwe nao, kwani walifanya kazi zao kwa welekevu.[#2 Fal. 12:15.]
8Ndipo, mtambikaji mkuu Hilkia alipomwambia mwandishi Safani: Nimeona kitabu cha Maonyo Nyumbani mwa Bwana. Kisha Hilkia akampa Safani hicho kitabu, akakisoma.
9Mwandishi Safani akaja kwa mfalme, akampasha mfalme habari na kumwambia: watumishi wako wamezimimina fedha zilizoonekana Nyumbani mwa Bwana, wakazitia mikononi mwao wenye kazi waliowekwa kuisimamia Nyumba ya Bwana.
10Kisha mwandishi Safani akamsimulia mfalme kwamba: Mtambikaji Hilkia amenipa kitabu; kisha Safani akakisoma mbele ya mfalme.
11Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya kitabu cha maonyo, akazirarua nguo zake.
12Kisha mfalme akamwagiza mtambikaji Hilkia na Ahikamu, mwana wa Safani, na Akibori, mwana wa Mikaya, na mwandishi Safani na Asaya aliyekuwa mtumishi wa mfalme kwamba:
13Nendeni kuniulizia Bwana mimi na ukoo huu na Wayuda wote kwa ajili ya maneno ya hiki kitabu kilichooneka! Kwani makali ya Bwana yenye moto ni makuu, nayo yanatuwakia sisi, kwa kuwa baba zetu hawakuyasikia maneno ya kitabu hiki na kuyafanya yote, tuliyoandikiwa humo.
14Ndipo, mtambikaji Hilkia na Ahikamu na Akibori na Safani na Asaya walipokwenda kwa mfumbuaji wa kike Hulda, mkewe Salumu, mwana wa Tikwa, mwana wa Harihasi aliyeyaangalia mavazi; naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili, wakasema naye.
15Akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mwambieni yule mtu aliyewatuma kwangu:
16Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikileta mabaya makali hapa, yawapate wenyeji wa hapa, ndiyo yote, kile kitabu kinayoyasema, alichokisoma mfalme wa Wayuda,
17Kwa kuwa wameniacha, wakavukizia miungu mingine, wanikasirishe kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo makali yangu yenye moto yatapawakia mahali hapa, nayo hayatazimika.[#5 Mose 31:29; 32:21-23.]
18Naye mfalme wa Wayuda aliyewatuma kumwuliza Bwana mwambieni haya: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kwa kuwa hapo, ulipoyasikia maneno yale,
19moyo wako umelegea, ukajinyenyekeza mbele ya Bwana papo hapo, ulipoyasikia, niliyoyasema ya mahali hapa na ya wenyeji wake kwamba: Patakuwa maangamizo na maapizo, basi, kwa kuwa umeyararua mavazi yako na kunililia mimi, mimi nami nimekusikia; ndivyo, asemavyo Bwana.
20Kwa sababu hii utaniona, nikikuita, uje kukutana na baba zako; ndipo, utakapopelekwa kulala kaburini mwako na kutengemana, macho yako yasiyaone hayo mabaya yote, mimi nitakayopaletea mahali hapa. Kisha wakampelekea mfalme majibu haya.[#Yes. 57:1-2.]