The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, mfalme alipotuma wajumbe, wakusanye kwake wazee wote wa Wayuda na wa Yerusalemu.
2Kisha mfalme akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana pamoja na Wayuda wote na wenyeji wote wa Yerusalemu na watambikaji na wafumbuaji na watu wote pia, wadogo kwa wakubwa, wakaenda naye, akawasomea masikioni pao maneno yote ya kitabu cha Agano kilichooneka Nyumbani mwa Bwana.
3Kisha mfalme akaja kusimama penye ile nguzo, akafanya mbele ya Bwana agano la kumfuata Bwana na kuyaangalia maagizo yake na mashuhuda yake na maongozi yake kwa moyo wote na kwa roho yote, ayasimamishe maneno ya Agano hili yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Nao watu wote wakaliitikia agano hili, walishike na kulisimamia.[#2 Fal. 11:14; Yos. 24:25.]
4Kisha mfalme akamwagiza mtambikaji mkuu Hilkia na watambikaji wa pili na walinzi wa vizingiti, watoe Jumbani mwa Bwana vyombo vyote vilivyotengenezwa vya kumtambikia Baali na Ashera na vikosi vyote vya mbinguni, wakavichoma moto nje ya Yerusalemu kwenye mashamba ya Kidoroni, nayo majivu yao akayatuma kupelekwa Beteli.[#2 Fal. 21:3.]
5Akawakomesha watambikaji wa kimizimu, wafalme wa Wayuda waliowaweka, wavukize vilimani pa kutambikia katika miji ya Wayuda na katika mitaa ya Yerusalemu, ndio waliomvukizia Baali, hata jua na mwezi na nyota zilizoko njiani kwa jua na vikosi vyote vya mbinguni.
6Nacho kinyago kile cha Ashera akakitoa Nyumbani mwa Bwana na kukipeleka nje ya Yerusalemu kwenye mto wa Kidoroni, akakichoma moto huko kwenye mto wa Kidoroni na kukipondaponda, kiwe mavumbi tu, nayo hayo mavumbi akayatupa kwenye makaburi yao walio watuwatu tu.
7Navyo vyumba vya wagoni wa Patakatifu vilivyokuwamo Nyumbani mwa Bwana akavibomoa; ndimo, wanawake walimofuma mahema ya Ashera.[#1 Fal. 14:24.]
8Nao watambikaji wote akawatoa katika miji ya Wayuda, akavichafua vijumba vya vilimani, hao watambikaji walimovukizia toka Geba mpaka Beri-Seba, navyo vijumba vya kutambikia vilimani vilivyokuwa malangoni upande wa kushoto wa hapo pa kuliingilia lango la Yosua, mkuu wa mji, watu walipoingia mjini, navyo akavibomoa kabisa.
9Lakini wale watambikaji wa vilimani hawakupata ruhusa kutambika penye meza ya kumtambikia Bwana mle Yerusalemu, wakala tu kwa ndugu zao mikate isiyochachwa.
10Akapachafua napo Tofeti katika bonde la wana wa Hinomu, mtu asiweze tena kumtolea Moleki mwanawe wa kiume au wa kike, awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni.[#3 Mose 18:21; 2 Fal. 17:17.]
11Akawakomesha nao wale farasi, wafalme wa Wayuda waliowekea jua hapo pa kuingia Nyumbani mwa Bwana karibu ya chumba cha kulalia cha mtumishi wa nyumbani Natani-Meleki kilichokuwa katika kijumba kile kilichojengwa upande wa machweoni kwa jua, nayo magari ya jua akayateketeza motoni.
12Nazo meza za kutambikia zilizokuwa darini penye chumba cha juu cha Ahazi zilizotengenezwa na wafalme wa Wayuda nazo meza za kutambikia, Manase alizozitengeneza katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana, mfalme akazivunjavunja na kuzitoa hapo, kisha akayatupa mavumbi yao katika mto wa Kidoroni.[#2 Fal. 16:10-11; 21:4-5; 2 Mambo 28:24.]
13Mfalme akavichafua navyo vijumba vya vilimani pa kutambikia vilivyoko ng'ambo ya Yerusalemu kuumeni kwenye Mlima wa Mwangamizaji, Salomo, mfalme wa Waisiraeli, alivyovijenga vya kutambikia Astoreti, lile tapisho la Wasidoni, na Kemosi, lile tapisho la Wamoabu, na Milkomu, lile chukizo la wana wa amoni.[#1 Fal. 11:7.]
14Akazivunja nazo nguzo za mawe za kutambikia, nayo miti ya Ashera akaikatakata, kisha akapajaza mahali pao mifupa ya watu.
15Akaivunjavunja nayo meza ya kutambikia iliyokuwa Beteli kilimani. Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, alikotengeneza kijumba cha kutambikia; basi, ile meza yenyewe pamoja na kijumba cha kutambikia pale kilimani akaivunjavunja, kisha yote pia yaliyokuwako huko kilimani akayateketeza kwa moto, akayapondaponda, yawe mavumbi tu, hata kinyago cha Ashera akakiteketeza.[#1 Fal. 12:32.]
16Yosia alipogeuka akaona makaburi yaliyokuwa katika mlima ule, akatuma kuichukua mifupa iliyokuwa mle makaburini, akaiteketeza juu ya meza ya kutambikia, akaichafua hivyo kwa lile neno la Bwana, alilolitangaza yule mtu wa Mungu aliyeyatangaza mambo haya.[#1 Fal. 13:2.]
17Akauliza tena: Hicho kijengo, ninachokiona, ndio nini? Watu wa huo mji wakamwambia: Ni kaburi la mtu wa Mungu aliyetoka Yuda na kuyatangaza haya, uliyoyafanya juu ya meza ya kutambikia huku Beteli.[#1 Fal. 13:30.]
18Ndipo, aliposema: Mwacheni huyu, alale! Mtu asiisumbue mifupa yake! Basi, wakaacha kuigusa mifupa yake nayo mifupa ya mfumbuaji aliyetoka Samaria.
19Nazo nyumba zote zilizojengwa za kutambikia vilimani kwenye miji ya Samaria, wafalme wa Waisiraeli walizozijenga, wamkasirishe Bwana, Yosia akaziondoa, nazo akazifanyizia mambo kama yale yote, aliyoyafanya huko Beteli.
20Nao watambikaji wote wa vilimani waliokuwako huko akawachinja, wawe ng'ombe za tambiko juu ya zile meza za kutambikia, hata mifupa ya watu akaiteketeza juu yao, kisha akarudi Yerusalemu.
21Kisha mfalme akawaagiza watu wote kwamba: Fanyeni sikukuu ya Pasaka ya Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha Agano![#2 Mose 12.]
22Kwani Pasaka kama hiyo haikufanywa tangu siku za waamuzi waliowaamua Waisiraeli hata siku zote za wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda.
23Ila Pasaka hii ya Bwana ilifanywa mle Yerusalemu katika mwaka wa 18 wa mfalme Yosia.
24Nao wakweza mizimu na wapunga pepo na vinyago vya nyumbani na magogo ya kutambikia na matapisho yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda namo Yerusalemu Yosia akayaondoa, kusudi ayatimize maneno ya Maonyo yaliyoandikwa katika kile kitabu, mtambikaji Hilkia alichokiona Nyumbani mwa Bwana.[#3 Mose 20:27; 5 Mose 29:17-18.]
25Mfalme kama yeye hakuwako mbele yake aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na kwa nguvu yake yote, ayafanye Maonyo yote ya Mose, wala nyuma yake hakuondokea aliyekuwa kama yeye.[#2 Fal. 18:5.]
26Lakini Bwana hakuyaacha makali yake makuu yenye moto yaliyowawakia Wayuda kwa ajili ya matendo ya kumkasirisha, manase aliyomkasirisha nayo.[#2 Fal. 21:11-16.]
27Kwa hiyo Bwana akasema: Wayuda nao nitawaondoa usoni pangu, kama nilivyowaondoa Waisiraeli, tena nitautupa nao mji huu wa Yerusalemu, niliouchagua, nayo Nyumba hii, niliyoisema: Jina langu litakaa humu.[#1 Fal. 8:29; 2 Fal. 17:18.]
28Mambo mengine ya Yosia nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
29Hizo siku zake akapanda Farao Neko, mfalme wa Misri, kwenda kupigana na mfalme wa Asuri kwenye mto wa Furati. Mfalme Yosia alipotoka kumpinga, yule akamwua kule Megido papo hapo, alipomwona.
30Watumishi wake wakamchukua garini, alipokwisha kufa, wakamtoa Megido na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika kaburini mwake. Kisha watu wa nchi hii wakamchukua Yoahazi, mwana wa Yosia, wakampaka mafuta, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake.[#2 Fal. 9:28.]
31Yoahazi alikuwa mwenye miaka 23 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi 3 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Hamutali, binti Yeremia, wa Libuna.
32Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, baba zake waliyoyafanya.
33Farao Neko akamfunga huko Ribula katika nchi ya Hamati, asiwe mfalme mle Yerusalemu, akailipisha nchi hii vipande 100 vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000, na kipande kimoja cha dhahabu, ndio shilingi 220000.[#Ez. 19:4.]
34Kisha Farao Neko akamfanya Eliakimu, mwana wa Yosia, kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, akaligeuza jina lake, akamwita Yoyakimu. Lakini Yoahazi akamchukua, aje naye Misri; ndiko, alikokufa.
35Zile fedha na dhahabu Yoyakimu akampa Farao; lakini hakuwa na budi kuitoza nchi machango, apate kuzilipa hizo fedha, Farao alizozitaka; watu wa hiyo nchi yake akamtoza kila mmoja kwa mali, alizowaziwa kuwa nazo; ndivyo, alivyowachangisha hizo fedha na dhahabu za kumpa Farao Neko.[#2 Fal. 15:20.]
36Yoyakimu alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Zebuda, binti Pedaya, wa Ruma.
37Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, baba zake waliyoyafanya.