The chat will start when you send the first message.
1Yoramu, mwana wa Ahabu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli huko Samaria katika mwaka wa 18 wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme miaka 12.[#2 Fal. 1:17.]
2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, lakini hakuzidi kama baba yake na mama yake, akaiondoa nguzo ya mawe ya kumtambikia Baali, baba yake aliyoitengeneza.[#1 Fal. 16:32.]
3Lakini makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, aligandamana nayo, hakuyaacha.[#1 Fal. 12:30.]
4Mesa, mfalme wa Wamoabu, aliyekuwa mfuga kondoo alikuwa akimletea mfalme wa Waisiraeli wana kondoo 100000 na manyoya ya madume ya kondoo 100000.
5Lakini Ahabu alipokufa, mfalme wa Wamoabu akamvunjia mfalme wa Waisiraeli hayo maagano.
6Siku hiyo mfalme Yoramu akatoka Samaria kuwakagua Waisiraeli wote.
7Kisha akatuma kwa Yosafati, mfalme wa Wayuda, kumwuliza hivyo: Mfalme wa Wamoabu amenivunjia maagano; utakwenda pamoja na mimi vitani kupigana na Wamoabu? Akasema: Nitapanda kwenda huko; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, nao farasi wangu ni kama farasi wako.[#1 Fal. 22:4.]
8Alipouliza: Tupande na kushika njia ipi? akasema: Njia ya nyika ya Edomu.
9Basi, wakaenda mfalme wa Waisiraeli na mfalme wa Wayuda na mfalme wa Waedomu. Walipokwenda na kuzunguka njia ya siku saba, walikuwa hawana maji ya vikosi vya makambini wala ya nyama waliozifuata nyayo zao.
10Ndipo, mfalme wa Waisiraeli aliposema: Yoi! Bwana amewaita hawa wafalme watatu, awatie mikononi mwa Wamoabu!
11Yosafati akauliza: Je? Hakuna mfumbuaji wa Bwana wa kumwuliza Bwana, yatakayokuwa? Ndipo, mmoja wao watumishi wa mfalme wa Waisiraeli akajibu: Yuko Elisa, mwana wa safati, aliyemmiminia Elia maji mikononi pake.[#1 Fal. 19:19,21; 22:5,7.]
12Yosafati akasema: Kwake yeye neno la Bwana liko. Ndipo, mfalme wa Waisiraeli na Yosafati na mfalme wa Waedomu waliposhuka kuja kwake.
13Elisa akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Tuna bia gani mimi na wewe? Nenda kwa wafumbuaji wa baba yako na kwa wafumbuaji wa mama yako! Mfalme wa Waisiraeli akamwambia: La! Kweli Bwana amewaita hawa wafalme, awatie mikononi mwa Wamoabu.
14Elisa akasema: Hivyo, Bwana Mwenye vikosi alivyo Mwenye uzima, ambaye ninasimama mbele yake, kama nisingeutazama uso wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, wewe nisingekuelekezea macho, nisikuone![#1 Fal. 18:15; Sh. 15:4.]
15Sasa nileteeni mpiga zeze! Ikawa, huyu mpiga zeze alipolipiga zeze lake, mara mkono wa Bwana ukamjia,
16akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Chimbeni humu bondeni mashimo po pote!
17Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: hamtaona upepo, wala hamtaona mvua, lakini bonde hili litajazwa maji, mpate kunywa ninyi nao mlio nao na nyama wenu.
18Nayo haya ni mepesi machoni pake Bwana, maana nao wamoabu atawatia mikononi mwenu.
19Ninyi mtaiteka miji yote yenye maboma na miji yote iliyochaguliwa. Mtaikata miti mizuri yote, navyo visima vyote vya maji mtavifukia na mashamba mazuri yote mtayaharibu kwa kuyatupia mawe.
20Ikawa asubuhi, walipotolea vipaji vya tambiko, ndipo, walipoona, maji yakija katika njia ya kutoka Edomu, mara nchi hiyo ikajaa maji.
21Wamoabu wote waliposikia, ya kuwa hao wafalme wanawapandia kupigana nao, wakakusanywa wote walioweza kujivika mata nao walio wazee, wakajipanga kuusimamia mpaka.
22Wakaamka na mapema, jua lilipochomoza juu ya yale maji; ndipo, Wamoabu walipoyaona yale maji mbele yao kuwa mekundu kama damu.
23Wakasema: Ni damu hizo; kumbe hao wafalme wamekosana, wakauana kila mtu na mwenzake. Sasa ninyi Wamoabu, haya! Chukueni nyara!
24Walipofika kwenye makambi ya Waisiraeli, Waisiraeli wakawaondokea, wakawapiga Wamoabu, nao wakawakimbia, kisha wakaendelea kuingia kwao wakiwapiga Wamoabu.
25Wakaibomoa miji, tena penye mashamba mazuri wakayatupia kila mtu jiwe lake, hivyo wakayajaza mawe, navyo visima vyote vya maji wakavifukia, hata miti mizuri yote wakaikata, hawakusaza mji, ni boma la mawe la Kiri-Hareseti peke yake tu. Huu nao wapiga makombeo wakauzunguka, waupige.[#2 Fal. 3:19.]
26Mfalme wa Wamoabu alipoona, ya kuwa mapigano hayo yatamshinda, asiyaweze, akachukua watu 700, kila mmoja akiuchomoa upanga wake, wajivunjie njia ya kwenda kwa mfalme wa Waedomu, lakini hawakuweza.
27Ndipo, alipomchukua mwanawe wa kwanza aliyetaka kumpokea ufalme, mwenyewe atakapokufa, akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko, akamteketeza ukutani juu. Ndipo, machafuko makubwa yalipowainukia Waisiraeli, wakaondoka huko, wakarudi kwao katika nchi yao.