The chat will start when you send the first message.
1Kulikuwa na mwanamke wa wanafunzi wa wafumbuaji, akamlilia Elisa kwamba: Mume wangu, mtumishi wako, amekufa, nawe unajua, ya kuwa mtumishi wako alikuwa mwenye kumcha Bwana; tena mtu, aliyemkopa, amekuja kuwachukua wanangu mawili, wawe watumwa wake.
2Elisa akamwuliza: Nikufanyizie nini? Niambie, nyumbani mwako unavyo vyombo gani? Akajibu: Kijakazi wako hanacho cho chote nyumbani, ni kitungi cha mafuta tu.[#1 Fal. 17:12.]
3Akamwambia: Nenda kujiombea vyombo vitupu huko nje kwao wote walio majirani zako, lakini usichukue vichache!
4Kisha ingia mwako, ukaufunge mlango nyuma yako na nyuma ya wanao! Kisha yale mafuta yako uyatie katika hivyo vyombo vyote; kimoja kikijaa, kiweke!
5Akaondoka kwake, akaja kuufunga mlango nyuma yake na nyuma ya wanawe; nao wakamletea vyombo, naye akavitia mafuta.
6Vyombo vilipojaa, akamwambia mwanawe: Niletee chombo kingine. Akamwambia: Hakuna tena chombo kingine. Ndipo, yale mafuta yalipokoma.
7Basi, akaenda kumsimulia yule mtu wa Mungu yaliyokuwa, naye akamwambia: Nenda, uyauze hayo mafuta, umlipe yule anayekudai! Yatakayosalia yatumie wewe na wanao!
8Ikawa siku moja, Elisa akaenda Sunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mkuu; huyu akakaza kumwomba, ale chakula kwake. Kwa hiyo kila mara alipopita hapo akafikia kwake kula chakula.[#Yos. 19:18.]
9Kisha yule mwanamke akamwambia mumewe: Tazama, nimetambua, ya kuwa yule mtu asiyekawa kufikia kwetu ni mtu mtakatifu wa Mungu.
10Na tumtengenezee darini chumba kidogo, tukaweke mle kitanda na meza na kiti na taa, kila atakapokuja kwetu afikie mlemle.
11Ikawa siku nyingine, alipokuja huko akafikia mle chumbani, akalala humo.
12Akamwambia mtoto wake Gehazi: Mwite huyo mwanamke wa Sunemu! Akamwita, naye akaja kusimama mbele yake.
13Akamwambia Gehazi: Mwambie: Nimeona, ulivyotusumbukia hayo masumbuko yote; nami nikufanyie nini? Unalo neno la kukusemea kwa mfalme au kwa mkuu wa vikosi? Akajibu: Mimi ninajikalia katikati yao walio ukoo wangu.
14Alipouliza tena: Nimfanyie nini? Gehazi akajibu: Hana mtoto. Naye mumewe ni mzee.
15Akasema: Mwite! Alipomwita, akaja, akasimama mlangoni.
16Akamwambia: Mwaka utakapopita, wakati kama huu utabeba mwana wa kiume kifuani. Akajibu: Bwana wangu, u mtu wa Mungu, uwimwongopee kijakazi wako![#1 Mose 18:10,14.]
17Lakini yule mwanamke akapata mimba, nao mwaka ulipopita, wakati huohuo akazaa mwana wa kiume, kama Elisa alivyomwambia.
18Mtoto alipokua, siku moja akatoka kwenda kwa baba yake shambani kwenye wavunaji.
19Mara akamwambia baba yake: Kichwa changu! Kichwa changu! Ndipo, alipomwambia kijana: Mpeleke kwa mama yake!
20Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, akakaa magotini kwake mpaka saa sita; ndipo, alipokufa.
21Akampeleka juu, akamlaza kitandani pake yule mtu wa Mungu, akafunga mlango nyuma yake, akatoka.
22Kisha akamwita mumewe, akamwambia: Tuma kwangu kijana mmoja na punda jike moja, nipige mbio kwenda kwake yule mtu wa Mungu, kisha nirudi!
23Akamwuliza: Sababu gani unataka kwenda kwake leo hivi? Hakuna mwandamo wa mwezi wala siku ya mapumziko. Akajibu: Si neno.
24Kisha akamtandika punda, akamwambia kijana wake: Uende ukimkimbiza, usinikawilishe safarini, nisipokuambia!
25Ndivyo, alivyokwenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu mlimani kwa Karmeli. Yule mtu wa Mungu alipomwona ng'ambo ya huko akamwambia mtoto wake Gehazi: Tazama, yule kule ni mwanamke wa Sunemu![#2 Fal. 2:25.]
26Sasa piga mbio, umkute njiani, umwulize: Hujambo? Naye mumeo hajambo? Naye mtoto hajambo? Akajibu: Hawajambo.
27Alipofika mlimani kwake yule mtu wa Mungu akamshika miguu; ndipo, Gehazi alipokuja, amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akamwambia: Mwache! Kwani anayo machungu rohoni; naye Bwana amenificha jambo hili, hakuniambia.
28Ndipo, yule mwanamke aliposema: Bwana wangu, nilikuomba kunipatia mtoto? Sikukuambia: Usinidanganye?[#2 Fal. 4:16.]
29Naye Elisa akamwambia Gehazi: Funga viuno vyako, uichukue fimbo yangu mkononi mwako, uende! Ukiona mtu, usimwamkie! Kama anakuamkia, usimjibu! Uiweke fimbo yangu usoni pa mtoto![#Luk. 10:4.]
30Ndipo, mama ya mtoto aliposema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa! Ndipo, alipoinuka kufuatana naye.
31Lakini Gehazi alikuwa amekwenda mbele yao, akaiweka ile fimbo usoni pa mtoto, lakini haikuwako sauti wala pumzi. Ndipo, aliporudi kukutana naye mwenyewe, akamwambia kwamba: Mtoto hakuamka.
32Elisa alipoingia mle chumbani akamwona mtoto, ya kuwa ni mfu, amelazwa kitandani pake.
33Akaenda, akajifungia mlango, wawe wawili tu, yeye na mtoto, kisha akamwomba Bwana.[#Tume. 9:40.]
34Akapanda, akamlalia mtoto akiweka kinywa chake kinywani pake na macho yake machoni pake navyo viganja vyake viganjani pake; alipomlalia hivyo, mwili wake mtoto ukapata jasho.[#1 Fal. 17:21.]
35Kisha Elisa akaondoka tena, akatembea chumbani mara moja huku, mara moja huko, kisha akapanda tena kumlalia hivyo; ndipo, mtoto alipopiga chafya mara saba, kisha akayafumbua macho yake.
36Akamwita Gehazi, akamwambia: Mwite huyo mwanamke wa Sunemu! Akamwita. Alipoingia kwake, akamwambia: Mchukue mwanao![#Luk. 7:15; Ebr. 11:35.]
37Akaja, akamwangukia miguuni pake na kumwinamia; kisha akamchukua mwanawe, akatoka.
38Elisa aliporudi Gilgali, kulikuwa na njaa katika nchi hiyo. Wanafunzi wa wafumbuaji walipokuja kukaa mbele yake, akamwambia mtoto wake: Weka chungu kikubwamotoni, uwapikie hawa wanafunzi wa wafumbuaji chakula.
39Mmoja akaenda shambani, akachuma mboga, akaona mtango wa mwituni, akachuma kwake hayo matango ya mwituni, akaijaza nguo yake, kisha akaja, akayakatakata chunguni kuwa chakula, kwani hawakuyajua.
40Kisha wakawaita watu, waje kula. Ikawa, walipokila chakula hicho wakalia kwamba: Kifo kimo chunguni, wewe mtu wa Mungu! Hawakuweza kula.
41Akasema: Leteni unga! Akautupa chunguni, akasema: Wapakulieni watu hawa, wapate kula! Hakikuwamo tena mle chunguni kilichokuwa kibaya.
42Kisha akaja mtu kutoka Baali-Salisa, akamletea yule mtu wa Mungu mikate ya malimbuko, nayo ilikuwa mikate ishirini ya mawele, tena gunia lenye masuke mabichi, akasema: Wapeni, watu hawa wale!
43Mtumishi wake akamwambia: watu mia niwaandalie hii mikate namna gani? Akasema: Wape tu watu hawa, wale! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Watakula, kisha wasaze.[#Mat. 15:33; Yoh. 6:9.]
44Ndipo, alipowaandalia, wakala, wakasaza, kama Bwana alivyosema.[#Mat. 16:9-10.]