2 Wafalme 5

2 Wafalme 5

Elisa anamponya Mshami Namani ukoma wake.

1*Namani, mkuu wa vita wa mfalme wa Ushami, alikuwa mtu mkubwa machoni pa bwana wake na mtu mwenye macheo, kwani Bwana alimtumia, awapatie Washami wokovu. Huyu mtu aliyekuwa fundi wa vita mwenye nguvu akaugua ukoma.

2Siku zilizopita, Washami walipokuwa wametoka kwao vikosi kwa vikosi, waliteka katika nchi ya Waisiraeli mtoto mdogo wa kike, naye akamtumikia mkewe Namani.

3Huyu akamwambia bibi wake: Kama bwana wangu angemtokea mfumbuaji alioko huko Samaria, yeye angemponya ukoma wake.

4Ndipo, Namani alipokwenda kwa bwana wake kumsimulia kwamba: Yule mtoto aliyetoka katika nchi ya Waisiraeli amesema hivi na hivi.

5Mfalme wa Ushami akasema: Haya! Nenda huko! Nami nitakupa barua kwa mfalme wa Waisiraeli. Akaenda akichukua mkononi mwake vipande 10 vya fedha, ndio shilingi 120000 na vipande vidogo vya dhahabu 6000, ndio shilingi 450000 na nguo 10 za sikukuu.

6Akampelekea mfalme wa Waisiraeli ile barua iliyosema: Hapo, barua hii itakapofika kwako, utamwona mtumishi wangu Namani, ninayemtuma kwako, umponye ukoma wake.

7Ikawa, mfalme wa Waisiraeli alipoisoma barua hii, akayararua mavazi yake na kusema: Je? Mimi ni Mungu, niweze kuua na kurudisha uzimani, huyu akimtuma mtu wake kwangu, nimponye ukoma wake? Jueni hili, mwone, jinsi huyu anavyonichokoza![#1 Fal. 20:7.]

8Ikawa, Elisa, yule mtu wa Mungu, alipoyasikia, ya kuwa mfalme wa Waisiraeli ameyararua mavazi yake, akatuma kwa mfalme kumwambia: Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje kwangu, apate kujua, ya kuwa katika Waisiraeli yuko mfumbuaji.

9Ndipo, Namani alipokuja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni penye nyumba ya Elisa.

10Elisa akatuma mjumbe kwake kumwambia: Nenda koga mara saba mle Yordani! Ndivyo, nyama za mwili wako zitakavyokuwa nzuri tena, nawe utatakata.

11Ndipo, Namani alipojiendea na kukasirika, akasema: Nimewaza moyoni kwamba: Atanitokea, asimame na kulitambikia Jina la Bwana Mungu wake, kisha pagonjwa apabandikie mkono wake, auponye ukoma.

12Tena ile mito ya Damasko, Abana na Paripari, siyo mizuri kuliko maji yote ya Isiraeli? Siwezi koga humo, nipate kutakata? Kwa hiyo akageuka, akaenda zake na kuchafuka.

13Lakini watumishi wake wakamsogelea, wakamwambia: Baba, kama mfumbuaji angalikuambia neno kubwa, hungalilifanya? Tena je? Akikuambia: Nenda koga, upate kutakata, usilifanye?

14Basi, akashuka, akajizamisha mara saba mle Yordani, kama yule mtu wa Mungu alivyomwambia; ndipo, nyama za mwili wake ziliporudi kuwa kama za mtoto, akatakata.[#Luk. 4:27.]

15Kisha akarudi kwa yule mtu wa Mungu, yeye nao wote, aliosafiri nao, akaja, akasimama mbele yake, akasema: Nitazame! Ninajua, ya kuwa hakuna Mungu katika nchi zote, isipokuwa katika nchi ya Isiraeli. Sasa pokea matunzo mkononi mwa mtumishi wako![#2 Fal. 5:5.]

16Akajibu: Hivyo, Bwana, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, sitachukua cho chote. Akamhimiza, ayachukue, lakini akakataa.

17Namani akasema: Kama hutaki, basi, lakini mtumishi wako na apewe mzigo wa mchanga unaochukulika na nyumbu wawili, kwani mtumishi wako hatatolea tena miungu mingine ng'ombe au vipaji vingine vya tambiko, ila Bwana peke yake.

18Neno hili tu Bwana na amwondolee mtumishi wako, bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni kutambika mle, naye akijiegemeza mkononi pangu, akijiangusha chini mle nyumbani mwa Rimoni, nami nikijiangusha chini mle nyumbani mwa Rimoni. Basi, neno hili Bwana na amwondolee mtumishi wako![#2 Fal. 7:2.]

19Akamwambia: Jiendee na kutengemana! Ndipo, alipotoka kwake.*

Gehazi anapata ukoma wa Namani.

20Alipokwisha kwenda kipande kizima, ndipo, Gehazi, mtoto wa Elisa, yule mtu wa Mungu, aliposema: Mbona bwana wangu amemwacha huyu Mshami Namani, asizichukue mkononi mwake zile mali, alizozileta! Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, mimi nitapiga mbio, nimfuate, nichukue mojamoja kwake.

21Basi, Gehazi akakimbia akimfuata Namani. Namani alipomwona, akimfuata mbiombio, Namani akaruka kutoka garini, akamwendea, akamwuliza: Ni habari njema?

22Akasema: Ni njema; bwana wangu amenituma kwamba: Tazama, sasa hivi wamekuja kwangu vijana wawili waliotoka milimani kwa Efuraimu kwa wanafunzi wa wafumbuaji. Wape kipande cha fedha, ndio shilingi 12000 na nguo mbili za sikukuu!

23Namani akamwambia: Itafaa, uchukue vipande viwili vya fedha, ndio shilingi 24000; akamhimiza sana, akazifunga zile fedha katika mifuko miwili pamoja na nguo mbili za sikukuu, akampa nao vijana wawili, wamchukulie.

24Alipofika kilimani akazichukua mikononi mwao, akaziweka mle nyumbani; nao wale watu akawapa ruhusa, wakaenda zao.

25Naye alipoingia kumtumikia bwana wake, Elisa akamwuliza: Unatoka wapi, Gehazi? Akajibu: Mtumishi wako hakwenda huko wala huko.

26Akamwambia: Roho yangu haikwenda na wewe, yule mtu alipogeuka garini mwake, akuone? Je? Siku hii ni siku ya kuchukua fedha na nguo za sikukuu na mashamba ya michekele na ya mizabibu na mbuzi na kondoo na ng'ombe na watumwa na vijakazi?

27Ukoma wa Namani utakuambukiza wewe na vizazi vyako kale na kale. Alipotoka kwake alikuwa mwenye ukoma uliong'aa kama theluji.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania