The chat will start when you send the first message.
1Wanafunzi wa wafumbuaji wakamwambia Elisa: Tazama, mahali hapa, tunapokaa machoni pako, ni padogo, hatuenei hapa.
2Na twende Yordani, tuchukue huko kila mtu nguzo moja, tujitengenezee huko mahali pa kukaa. Akajibu: Nendeni!
3Mmoja wao akasema: Ingefaa, wewe uende pamoja na watumishi wako. Akasema: Basi, nami nitakwenda.
4Akaenda nao; walipofika Yordani, wakakata miti.
5Ikawa, mmoja alipokata nguzo yake, chuma cha shoka yake kikaanguka majini, akalia kwamba: E bwana wangu! Nacho kimekopwa kwa mtu!
6Yule mtu wa Mungu akauliza: Kimeangukia wapi? Alipomwonyesha pale mahali, akakata kijiti, akakitupa hapohapo; ndivyo, alivyokieleza kile chuma.
7Kisha akamwambia: Kiokote! Naye akaunyosha mkono wake, akakikamata.
8Mfalme wa Ushami akawa akiwapelekea Waisiraeli vita. Lakini kila alipopatana na watumishi wake kwamba: Nitapiga makambi yangu mahali fulani,
9yule mtu wa Mungu akatuma kwa mfalme wa Waisiraeli kumwambia: Angalia, usipitie mahali hapo! kwani ndiko, Washami watakakoshukia.
10Kwa hiyo mfalme wa Waisiraeli alipotaka kutuma watu kwenda mahali pale, yule mtu wa Mungu alipomkataza, akapona hapo, tena si mara moja wala mbili tu.
11Ndipo, moyo wa mfalme wa Ushami ulipochafuka kwa ajili hiyo, akawaita watumishi wake, akawauliza: Hamwezi kuniambia, kama ni nani wa kwetu aliye upande wa mfalme wa Waisiraeli?
12Mmoja wao watumishi wake akasema: Sivyo, bwana wangu mfalme, kwani mfumbuaji Elisa alioko kwao Waisiraeli humsimulia mfalme wa Waisiraeli nayo maneno, unayoyasema chumbani mwako mwa kulalia.
13Ndipo, alipoagiza: Nendeni kutazama, aliko! Kisha nitatuma kumkamata. Alipopashwa habari kwamba: Yuko Dotani,
14akatuma kikosi kikubwa chenye farasi na magari kwenda huko; wakafika usiku, wakauzunguka ule mji.
15Mtumishi wa yule mtu wa Mungu alipoamka asubuhi, aondoke kutoka nje, akaona, ya kuwa kiko kikosi kinachouzunguka huo mji pamoja na farasi na magari; ndipo, yule mtoto wake alipomwambia: E bwana wangu, tufanyeje?
16Akajibu: Usiogope! Kwani walio upande wetu ndio wengi kuliko wao walio upande wao.[#2 Mambo 32:7.]
17Kisha Elisa akaomba na kusema: Bwana, mfumbue macho, apate kuona! Ndipo, Bwana alipomfumbua yule kijana macho, apate kuona, akaona, ya kuwa huo mlima wote umejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisa pande zote.
18Wale askari walipomshukia, Elisa akamwomba Bwana kwamba: Wapige wamizimu hawa, wapofuke! Akawapiga, wakapofuka, kama Elisa alivyoomba.[#1 Mose 19:11.]
19Kisha Elisa akawaambia: Njia hii siyo, wala mji huu sio; nifuateni, niwapeleke huko, yule mtu, mnayemtafuta, aliko! Akawapeleka Samaria.
20Walipofika Samaria, Elisa akasema: Bwana, wafumbue watu hawa macho! Ndipo, Bwana alipowafumbua macho, wakaona, ya kuwa wameingia katikati ya mji wa Samaria.
21Mfalme wa Waisiraeli alipowaona akamwuliza Elisa: Baba, niwapige? Ukisema, nitawapiga!
22Akajibu: Usiwapige! Je? Uliowateka kwa upanga wako na kwa upindi wako huwapiga? Waandalie vyakula na vya kunywa, wale, wanywe, kisha waende zao kwa bwana wao![#2 Mambo 28:15; Fano. 25:21.]
23Ndipo, alipowatengenezea karamu kubwa, wakala, wakanywa; kisha akawapa ruhusa, wakaenda zao kwa bwana wao. Kisha vikosi vya Ushami havikurudi tena kuingia katika nchi ya Waisiraeli.
24Hayo yalipokwisha kufanyika, Benihadadi, mfalme wa Ushami, akavikusanya vikosi vyake vyote, akapanda, akausonga Samaria kwa kuuzinga.
25Mle Samaria ikajamo njaa kubwa; hapo, walipousonga kwa kuuzinga, kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa fedha 80, ndio shilingi 320, nacho kibaba cha mavi ya njiwa kikapata fedha 5, ndio shilingi 20.
26Siku moja mfalme alipotembea bomani, mwanamke akamlilia kwamba: Bwana wangu mfalme, nisaidie!
27Akajibu: Bwana asipokusaidia, mimi nitawezaje kukusaidia? Je? Ninacho kitokacho penye kupuria ngano au penye kukamulia zabibu?
28Kisha mfalme akamwuliza: Shauri lako nini? Akasema: Huyu mwanamke mwenzangu aliniambia: Nipe mwanao, tumle leo! Kisha kesho tutamla wangu.
29Basi, tukampika mwanangu, tukamla. Tena kesho yake, nilipomwambia: Nipe mwanao, tumle! akamficha.[#5 Mose 28:53.]
30Mfalme alipoyasikia maneno ya huyu mwanamke, akayararua mavazi yake papo hapo, alipokuwa anatembea bomani; nao watu walipomtazama, wakaona, ya kuwa amevaa gunia ndani penye mwili wake.
31Akasema: Mungu anifanyizie hivi na hivi, Elisa, mwana wa Safati, akishinda leo mwenye kichwa chake!
32Naye Elisa alikuwa akikaa nyumbani mwake, nao wazee walikaa kwake. Lakini mfalme alikuwa ametuma mtu kwenda mbele yake; huyu mjumbe alipokuwa hajafika bado kwake, yeye Elisa akwaambia wazee: Je? mmeona, ya kuwa amemtuma huyu mwuaji, anikate kichwa? Angalieni! Mjumbe atakapofika, fungeni mlango na kumzuia mlangoni! Je? Hili silo shindo la miguu ya bwana wake anayemfuata?
33Angali akisema nao, mara mjumbe yule akashuka kufika kwake, akasema: Tazameni, mabaya haya yametoka kwake Bwana! Iko nini tena, tutakayongojea, itoke kwake Bwana?[#Amo. 3:6.]