2 Wafalme 7

2 Wafalme 7

Elisa anawafumbulia Wasamaria mwisho wa njaa.

1Elisa akasema: Sikilizeni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kesho saa zizi hizi pishi ya unga wa ngano itauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili hapo mlangoni pa mji huu wa samaria.[#2 Fal. 7:16.]

2Ndipo, mkuu wa askari thelathini, ambaye mfalme alimwegemea mkono wake, alipomjibu yule mtu wa Mungu akisema: Ijapo, Bwana aweke madirisha mbinguni, neno hilo litawezekanaje? Akamjibu: Tazama, na uvione mwenyewe kwa macho yako, lakini hutakula wewe.[#2 Fal. 5:18; 7:17.]

Washami wanafukuzwa na Bwana, neno la Elisa likatimia.

3Kulikuwa na watu wanne wenye ukoma waliokaa hapo pa kuliingilia lango la mji, wakasemezana wao kwa wao: Sisi tunakalia nini huku, hata tutakapokufa?[#3 Mose 13:46.]

4Tukisema: Tuingie mjini, njaa imo, nasi tutakufa; tukikaa huku, tutakufa vilevile. Sasa twende, tujipenyeze makambini kwa Washami! Wasipotuua, tutapona; wakituua, basi, tutakufa.[#Est. 4:16.]

5Kulipokwisha kuwa usiku, wakaondoka kuingia katika makambi ya Washami, Walipofika pembeni kwa makambi ya Washami. Wakitazama, hamna watu.

6Kwani Bwana alikuwa amevumisha kwenye makambi ya Washami sauti kama mashindo ya kikosi kikubwa chenye farasi na magari; ndipo, waliposemezana wao kwa wao: Kumbe mfalme wa Waisiraeli ametuletea wafalme wa Wahiti wa wafalme wa Misri, aliowakodisha, watujie![#2 Fal. 19:7.]

7Basi, wakaondoka papo hapo usiku, wakakimbia na kuyaacha mahema yao na farasi wao na punda wao na makambi yote hivyo, yalivyokuwa, wakakimbilia tu kujiponya wenyewe.

8Ikawa, wale wenye ukoma walipofika pembeni kwa makambi, wakaingia katika hema moja, wakala, wakanywa, wakachukua humo fedha na dhahabu na nguo; kisha wakaenda, wakazichimbia mchangani. Waliporudi wakaingia katika hema jingine, namo humo wakachukua mali, kisha wakaenda kuzichimbia nazo mchangani.

9Kisha wakasemezana wao kwa wao: Tunayoyafanya siyo! Leo ni siku ya mbiu njema, lakini sisi tukinyamaza tu na kungoja, mpaka kuche, tutakora manza. twenda sasa hivi kupasha habari nyumbani mwa mfalme!

10Wakaja, wakamwita mngoja lango la mji, wakawapasha habari kwamba: Tumeingia makambini mwa Washami, lakini hamna mtu wala sauti ya mtu, wamo farasi tu waliofungwa na punda waliofungwa, tena mahema yamo vivyo hivyo, yalivyoachwa.

11Ndivyo, walivyowaitia wangoja lango la mji, nao wakapasha habari mjini nyumbani mwa mfalme.

12Mfalme alipoamka usiku akawaambia watumishi wake: nitawaelezea haya, Washami waliyotufanyizia: Kwa kuwa wanajua, ya kuwa tuko na njaa, wametoka makambini, wajifiche porini kwamba: Watakapotoka mjini, tutawakamata, wakiwa wa hai, kisha tutaingia mjini.

13Mmoja wao watumishi wake akamjibu akisema: Chukueni farasi watano waliosalia katika wao waliosazwa humu mjini, kwani nao ni sawa kama wale Waisiraeli wengi mno waliosazwa humu mjini, maana nao watakuwa wa kufa tu kama wale Waisiraeli wengi waliokwisha kumalizika. Kwa hiyo na tuwatume, tuone yatakayokuwa.

14Wakachukua magari mawili yenye farasi, ndiyo, mfalme aliyoyatuma kuwafuata Washami waliotoka makambini, akawaambia: Nendeni, mwatazame!

15Wakawafuata mpaka kwenye Yordani, wakaona, njia hiyo yote imejaa mavazi na mata, Washami waliyoyaacha wakikimbia upesiupesi. Ndipo, wale wajumbe waliporudi kumpasha mfalme habari.

16Basi, watu wakatoka mjini, wakayateka makambi ya washami. Kisha pishi ya unga wa ngano ikauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili, kama Bwana alivyosema.[#2 Fal. 7:1.]

17Yule mkuu wa askari thelathini, ambaye mfalme alimwegemea mkono wake, akamweka langoni mwa mji, awasimamie watu, lakini watu wakamkanyaga mle langoni, akafa palepale, kama yule mtu wa Mungu alivyosema hapo, mfalme aliposhuka kufika kwake.[#2 Fal. 7:2.]

18Hapo yakawa yaleyale, yule mtu wa Mungu aliyomwambia mfalme kwamba: Kesho saa zizi hizi pishi ya unga wa ngano itauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili hapa langoni pa mji huu wa Samaria.

19Ndipo, yule mkuu wa askari thelathini alipomjibu yule mtu wa Mungu akisema: Ijapo, Bwana aweke madirisha mbinguni, neno hilo litawezekanaje? Naye yule alikuwa amemjibu: Tazama, na uvione mwenyewe kwa macho yako, lakini hutakula wewe.

20Ndiyo yaliyotimia hapo, watu walipomkanyaga penye lango la mji, mpaka akifa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania