2 Samweli 10

2 Samweli 10

Dawidi anawapelekea Waamoni wa Washami vita.

(Taz. 1 Mambo 19.)

1Hayo yalipokwisha, akafa mfalme wa wana wa Amoni, naye mwanawe Hanuni akawa mfalme mahali pake.

2Dawidi akasema: Nitamfanyizia Hanuni, mwana wa Nahasi, mambo ya upole, kama baba yake alivyonifanyizia nami mambo ya upole. Kwa hiyo Dawidi akatuma wajumbe, wamtulize moyo kwa ajili ya baba yake. Lakini watumishi wa Dawidi walipofika katika nchi ya wana wa Amoni,

3wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia bwana wao Hanuni; Je? Dawidi anataka kweli kumheshimu baba yako machoni pako akituma kwako wajumbe wa kukutuliza moyo? Dawidi hakuwatuma watumishi wake kwako kuuchunguza mji huu na kuupeleleza, apate kuufudikiza?

4Ndipo, Hanuni alipowakamata watumishi wa Dawidi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akawakatia mavazi yao nusu kuyafikisha matako yao, kisha akawapa ruhusa kwenda zao.

5Watu walipompasha Dawidi habari hizo, akatuma wengine kuwaendea njiani, kwa kuwa watu hawa walikuwa wametwezwa sana; mfalme akawaambia: Kaeni Yeriko, mpaka ndevu zenu zikue tena, kisha rudini!

6Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa wamejichukizisha kwake Dawidi, ndipo, wana wa Amoni walipotuma watu kuwakodisha Washami wa Beti-Rehobu na Washami wa Soba, ni askari waliokwenda kwa miguu 20000, tena mfalme wa Maka na watu 1000 na watu 12000 wa Tobu.

7Dawidi alipoyasikia akamtuma Yoabu na vikosi vyote vya mafundi wa vita.

8Wana wa Amoni wakatoka, wakajipanga penye lango la mji, wapige vita, nao Washami wa Soba na wa Rehobu na watu wa Tobu na wa Maka wakawa peke yao shambani.

9Yoabu alipoona, ya kuwa wamejipanga kupiga vita usoni na mgongoni pake, akachagua wengie katika wateule wote wa Waisiraeli, akawapanga, wapigane na Washami.

10Nao watu waliosalia akawatia mkononi mwa ndugu yake Abisai, akawapanga, wapigane na wana wa Amoni,

11akasema: Kama Washami wanapata nguvu za kunishinda, sharti uje kunisaidia. Tena kama wana wa Amoni wanapata nguvu za kukushinda, sharti nije, nikusaidie.

12Jipe moyo, tushikizane mioyo, tuwapiganie watu wa kwetu na miji ya Mungu wetu! Ndipo, Bwana atakapoyafanya, aliyoyaona kuwa mema.

13Kisha Yoabu na watu wake, aliokuwa nao, wakawasogelea Washami kupigana nao, lakini wao wakawakimbia.

14Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa Washami wamekimbia, ndipo, nao walipomkimbia Abisai, wakaigia mjini mwao, lakini Yoabu akarudi akitoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu.

15Washami walipoona, ya kuwa wameshindwa nao Waisiraeli, wakakusanyika pamoja.

16Kisha Hadadezeri akatuma watu kuwachukua Washami walioko ng'ambo ya huko ya jito hilo; nao wakaja Helamu, naye mkuu wa vikosi vya Hadadezeri, jina lake Sobaki, akawaongoza.

17Dawidi alipopashwa habari hizi, akawakusanya Waisiraeli wote, akauvuka Yordani, akaja Helamu; ndipo, Washami walipojipanga kukutana na Dawidi, wakapigana naye.

18Kisha Washami wakawakimbia Waisiraeli, Dawidi akaua kwao Washami farasi waliovuta magari 700 na wapanda farasi 40000, hata Sobaki, mkuu wa vikosi vyao, akampiga, naye akafa papo hapo.

19Wafalme wote waliomtumikia Hadadezeri walipoona, ya kuwa wameshindwa na Waisiraeli, wakafanya mapatano na Waisiraeli, wakawatumikia. Kwa hiyo Washami wakaogopa kuwasaidia wana wa Amoni tena.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania