The chat will start when you send the first message.
1Hayo yalipokwisha kufanyika, Abisalomu, mwana wa Dawidi, alikuwa na umbu lake, jina lake Tamari, naye alikuwa mzuri; kwa hiyo Amunoni, mwana wa Dawidi, akampenda.[#2 Sam. 3:2.]
2Naye Amunoni akasongeka moyoni, akapata kuwa mgonjwa kwa ajili ya umbu lake Tamari, kwani alikuwa mwanamwali, naye Amunoni akaviona kuwa vigumu sana kumfanyizia lo lote.
3Lakini Amunoni alikuwa na mwenzake, jina lake Yonadabu, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi; huyu Yonadabu alikuwa mwerevu sana.[#1 Sam. 16:9.]
4Huyu akamwuliza: Mbona wewe, mwana wa mfalme, unanyongeka hivyo kila kunapokucha? Huwezi kunisimulia sababu yake? Ndipo, Amunoni alipomwambia: Mimi nampenda Tamari, umbu lake ndugu yangu Abisalomu.
5Yonadabu akamwambia: Lala kitandani pako kuwa kama mgonjwa sana! Kisha baba yako akija kukutazama, umwambie: Kama umbu langu Tamari angekuja kuniandalia chakula na kukitengeneza hicho chakula machoni pangu, nipate kuviona, basi, ningekula na kuvipokea mkononi mwake.
6Kwa hiyo Amunoni akalala kitandani kuwa kama mgonjwa. Mfalme alipokuja kumtazama, Amunoni akamwambia mfalme: Kama umbu langu Tamari angekuja kuandalia machoni pangu vikate viwili, ningevila na kuvipokea mkononi mwake.
7Ndipo, Dawidi alipomtuma Tamari kwenda mle nyumbani kwamba: Nenda nyumbani mwa umbu lako Amunoni, umtengenezee chakula!
8Ndipo, Tamari alipokwenda nyumbani mwa umbu lake Amunoni, naye alikuwa amelala; akachukua unga, akaukanda, akautengeneza machoni pake kuwa vikate, akavioka hivyo vikate.
9Kisha akakichukua kikaango, akavitia katika sahani machoni pake, lakini Amunoni akakataa kuvila, akasema: Watoeni watu wote humu mwangu! Walipokwisha kuwatoa watu wote mwake,
10Amunoni akamwambia Tamari: Kilete hicho chakula chumbani humu, nikile na kukipokea mkononi mwako! Tamari akavichukua hivyo vikate, alivyovitengeneza, akampelekea umbu lake Amunoni mle chumbani.
11Alipompa, avile, akamshika na kumwambia: Njoo, umbu langu, ulale kwangu![#3 Mose 18:9.]
12Lakini akamwambia: Sivyo, umbu langu, usinichukue kwa nguvu. Kwani mambo kama hayo hayafanywi kwao Waisiraeli, nawe usiufanye upumbavu huu![#5 Mose 22:21.]
13Mimi nami nitakwenda wapi nikitwezwa hivyo? Wewe nawe utakuwa mpumbavu mwenzao walio hivyo kwao Waisiraeli. Ila sema na mfalme sasa, kwani hatakukataza kunioa.
14Lakini hakutaka kuyasikia, aliyomwambia, akamkamata kwa nguvu na kumshurutiza, mpaka akimpata, alale naye.
15Kisha Amunoni akaingiwa na machukizo makubwa sana ya kuchukizwa naye, nayo hayo machukizo yake ya kuchukizwa naye yakawa makubwa kuliko ule upendo wake wa kwanza wa kumpenda; kwa hiyo Amunoni akamwambia: Ondoka, uende zako!
16Naye akamwambia: La, sivyo! Kibaya hiki cha kunifukuza kingekuwa kikubwa kuliko kile, ulichonifanyizia, lakini akakataa kumsikia,
17akamwita kijana aliyemtumikia, akamwambia: Mtoeni huyu humu mwangu, aende nje! Tena funga mlango, akiisha kutoka.
18Naye alikuwa amevaa rinda refu la nguo za rangi, kwani ndiyo mavazi, watoto wa kike wa mfalme waliyoyavaa siku za kuwa wanawali. Yule mtumishi wake alipomtoa nje na kufunga mlango, alipokwisha kutoka,
19Tamari akachukua uvumbi, akautia kichwani pake, akalirarua lile rinda la nguo za rangi, alilokuwa amelivaa, akabandika mkono kichwani pake, akaenda zake na kulia.[#Iy. 2:12.]
20Ndipo, Abisalomu alipomwuliza umbu lake: Umbu lako Amunoni amekuwa kwako? Umbu langu, sasa nyamaza tu! Ndiye umbu lako. Neno hili usiliweke moyoni mwako! Basi, Tamari akakaa na ukiwa wake nyumbani mwa Abisalomu, umbu lake.
21Mfalme Dawidi alipoyasikia mambo haya, akachafuka sana.
22Lakini Abisalomu hakusema na Amunoni wala neno baya wala jema, kwani Abisalomu alimchukia Amunoni, kwa kuwa alimchukua umbu lake Tamari kwa nguvu.
23Miaka miwili ilipopita, Abisalomu akajipatia watu wa kukata manyoya ya kondoo kule Baali-Hasori upande wa Efuraimu; ndipo, Abisalomu alipowaalika wana wote wa mfalme.
24Abisalomu akaja hata kwa mfalme, akamwambia: Tazama, wako wenye kukata manyoya ya kondoo kwa mtumishi wako, mfalme naye na aje pamoja na watumishi wake kwa mtumishi wako!
25Mfalme akamwambia Abisalomu: Sivyo, mwanangu, tusije sote kwako, tusikulemee. Hata alipomhimiza, hakutaka kwenda, ila akambariki.
26Abisalomu akamwambia: Kama huji, ndugu yangu Amunoni na aende na sisi. Mfalme akamwuliza: Unamtakia nini kwenda na wewe?
27Abisalomu alipomhimiza, akampa Amunoni ruhusa kwenda pamoja naye pamoja na wana wote wa mfalme.
28Kisha Abisalomu akawaagiza vijana wake kwamba: Angalieni! Moyo wa Amunoni utakapochangamka kwa kunywa mvinyo, nitawaambieni: Mpigeni Amunoni! Ndipo, mtakapomwua pasipo kuogopa. Kwani ni mimi ninayewaagiza ninyi kuvifanya. Jipeni mioyo, mpate kuwa wenye nguvu![#3 Mose 20:17.]
29Vijana wa Abisalomu wakamfanyizia Amunoni, kama Abisalomu alivyowaagiza. Ndipo, wana wote wa mfalme walipoondoka, wakapanda kila mmoja nyumbu wake, wakakimbia.
30Hao walipokuwa njiani, Dawidi akapata habari kwamba: Abisalomu amewaua wana wote wa mfalme, asisalie kwao hata mmoja.
31Ndipo, mfalme alipoinuka, akayararua mavazi yake, akajilaza chini, nao watumishi wake wote wakawa wamesimama wenye mavazi yaliyoraruliwa.
32Naye Yonadabu, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akaanza kusema kwamba: Bwana wangu asiwaze, ya kwamba wamewaua vijana wote walio wana wa mfalme, kwani Amunoni amekufa peke yake, kwani shauri hili lilikuwa limekatwa na kinywa chake Abisalomu tangu siku ile, yule alipomchukua umbu lake Tamari kwa nguvu.
33Sasa bwana wangu mfalme asiliweke neno hili moyoni mwake la kwamba: Wana wote wa mfalme wamekufa! Ila ni Amunoni peke yake aliyekufa.
34Lakini Abisalomu alikuwa amekimbia. Kijana wa mfalme aliyekuwa mlinzi alipoyainua macho yake, aone vema, mara akaona watu wengi wanaotelemka katika njia iliyoko mgongoni kwake upande wa milimani.
35Ndipo, Yonadabu alipomwambia mfalme: Tazama, wana wa mfalme wanakuja! Kama mtumishi wako alivyosema, ndivyo, inavyokuwa.
36Alipokwisha kusema, ndipo, wana wa mfalme walipofika, wakapaza sauti zao, wakalia; naye mfalme na watumishi wake wote wakalia kilio kikubwa sana.
37Abisalomu alipokimbia akaenda kwa Talmai, mwana wa Amihudi, mfalme wa Gesuri. Naye Dawidi akamlilia mwanawe kila siku.[#2 Sam. 3:3; 14:23.]
38Naye Abisalomu akakaa miaka mitatu kule Gesuri, alikokwenda kwa kukukimbilia.
39Naye mfalme Dawidi akatamani sana kwenda kumtokea Abisalomu, alipokwisha kuutuliza moyo wake kwa ajili ya kufa kwake Amunoni.