2 Samweli 14

2 Samweli 14

Yoabu anatumia mwanamke wa Tekoa kumpatia Abisalomu upole kwa Dawidi.

1Yoabu, mwana wa Seruya, alipotambua, ya kuwa moyo wa mfalme umerudi kumwelekea Abisalomu,

2Yoabu akatuma Tekoa kumchukua huko mwanamke aliye mwerevu wa kweli, akamwambia: Jitendekeze kuwa mwenye kufiwa, ukivaa nguo za matanga pasipo kujipaka mafuta, uwe sawasawa na mwanamke anayemlilia mfu siku nyingi.

3Kisha uende kwa mfalme, mwambie maneno kama haya! Naye Yoabu akamwambia, atakayoyasema na kinywa chake.

4Basi, huyo mwanamke wa Tekoa akaja kusema na mfalme akijiangusha chini kifudifudi, kwamba amwangukie, akasema: Nisaidie, mfalme!

5Mfalme alipomwuliza: Una nini? akasema: Mimi ni mwanamke mjane kweli, maana mume wangu amekufa.

6Tena kijakazi wako alikuwa na wana wawili wa kiume, nao wakagombana shambani; kwa kuwa hakuwako aliyewaamua, mmoja akampiga ndugu yake, mpaka akamwua.

7Mara ukoo wote ukamwinukia kijakazi wako na kusema: Mtoe aliyempiga ndugu yake, tumwue kwa ajili ya roho ya ndugu yake, aliyemwua, tumtoweshe naye atakayelichukua fungu lake! Ndivyo, wanavyotaka kulizima nalo kaa la mwisho lililosalia, wasimwachie mume wangu huku nchini jina wala sao lo lote.[#5 Mose 19:11-13.]

8Mfalme akamwambia huyu mwanamke: Jiendee nyumbani kwako! Mimi nitatoa amri kwa ajili yako.

9Ndipo, huyu mwanamke wa Tekoa alipomwambia mfalme: Bwana wangu mfalme, manza ni zangu na za mlango wa baba yangu, mfalme hayumo, wala kiti chake cha kifalme.

10Mfalme akamwambia: Atakayekutakia kitu mlete kwangu, asiendelee kukugusa tena.

11Akajibu: Mfalme, mkumbuke Bwana Mungu wako, mwenye kulipiza damu asizidi kufanya mabaya, wakimwangamiza mwanangu. Akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, unywele mmoja tu wa mwanao hautaanguka chini.[#1 Sam. 14:45; 1 Fal. 1:52.]

12Ndipo, huyu mwanamke alipomwuliza: Kumbe kijakazi wako ataweza kumwambia bwana wangu mfalme neno? Akajibu: Sema

13Basi! huyu mwanamke akasema: Mbona unawawazia watu walio wa Mungu mambo kama hayo? Kwa kulisema neno hili mfalme anakuwa kama mtu aliyekora manza, mfalme asipomrudisha yule mtu wake aliyefukuzwa.

14Kwani hatuna budi kufa; tunafanana na maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kukusanywa tena; lakini Mungu haondoi roho ya mtu, ila huwaza, jinsi inavyowezekana, mtu aliyefukuzwa asikae na kufukuzwa kwake vivyo hivyo.[#Ez. 18:23.]

15Sasa nimefika kumwambia bwana wangu mfalme neno hili, kwa kuwa watu wamenitisha. Kwa hiyo kijakazi wako alisema: Na nimwambie mfalme, labda mfalme atalifanya neno la kijakazi wake.

16Kwani mfalme, atanisikia, amponye kijakazi wake mkononi mwa yule mtu anayetaka kuniangamiza pamoja na mwanangu, nisikae na fungu, Mungu alilonipa.

17Kwa hiyo kijakazi wako akasema: Neno la bwana wangu mfalme litanipatia utulivu, kwani kama malaika wa Mungu alivyo, ndivyo, bwana wangu mfalme alivyo, asikie mema na mabaya. Naye Bwana Mungu wako awe na wewe![#2 Sam. 19:27.]

18Mfalme akajibu na kumwambia huyu mwanamke: Usinifiche kabisa, nitakalokuuliza! Huyu mwanamke akasema: Bwana wangu mfalme na aseme!

19Ndipo, mfalme alipouliza: Je? Mkono wa Yoabu haumo katika mambo haya yote? Huyu mwanamke akajibu kwamba: Hivyo roho yako, bwana wangu mfalme, ilivyo nzima, hakuna njia kuumeni wala kushotoni ya kupita penye maneno yote, bwana wangu mfalme aliyoyasema; kweli mtumishi wako Yoabu ndiye aliyeniagiza hivyo, naye ndiye aliyeniambia na kinywa chake, kijakazi wako atakayoyasema.

20Kwa kutaka kuligeuza jambo hili, upande wake mwingine uonekane, mtumishi wako Yoabu amelifanya hili neno, naye bwana wangu anao werevu wa kweli ulio kama werevu wa malaika wa Mungu wa kuyajua yote yaliyopo nchini.[#2 Sam. 14:17.]

21Kisha mfalme akamwambia Yoabu: Tazama, nitalifanya jambo hili. Nenda, umrudishe yule kijana Abisalomu.

22Ndipo, Yoabu alipojiangusha chini kifudifudi kumwangukia na kumbariki mfalme, kisha Yoabu akasema: Leo hivi mtumishi wako anajua, ya kuwa nimeona upendeleo machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amelifanya neno la mtumishi wake.

23Kisha Yoabu akaondoka, akaenda Gesuri, akamleta Abisalomu humo Yerusalemu.[#2 Sam. 13:37.]

24Lakini mfalme akasema: Na aende kuingia nyumbani mwake pasipo kuonana na mimi uso kwa uso. Kwa hiyo Abisalomu akaingia nyumbani mwake pasipo kuonana na mfalme uso kwa uso.

25Kwao Waisiraeli wote hakuwako mtu, watu waliyemsifu sana kwa uzuri wake wa mwili kama Abisalomu, toka wayo wa mguu wake mpaka kwenye utosi wake hakikuwako cho chote kisicho kizuri.

26Kila mara siku za mwaka mmoja zilipopita akazinyoa nywele za kichwani, naye huzinyoa, zikimlemea kwa uzito; tena alipokwisha kuzinyoa huzipima hizo nywele za kichwani pake, nazo huwa kama sekeli 200, ndio ratli 7 kwa kipimo cha mfalme.

27Kisha kwake Abisalomu wakazaliwa wana wa kiume watatu na wa kike mmoja, jina lake Tamari; naye alikuwa mwanamke mwenye sura nzuri.[#2 Sam. 13:1.]

28Abisalomu alipokaa Yerusalemu miaka miwili pasipo kuonana na mfalme uso kwa uso,

29ndipo, Abisalomu alipotuma kwa Yoabu, apate kumtuma kwa mfalme, lakini akakataa kufika kwake. Akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kufika.

30Ndipo, alipowaambia watumishi wake: Tazameni, liko shamba la Yoabu linalopakana na langu, nalo ni la mawele yake. Nendeni, mlichome moto! Ndipo, watumishi wa Abisalomu walipolichoma moto hilo shamba.

31Ndipo, Yoabu alipoondoka, akaja kwa Abisalomu nyumbani kwake, akamwuliza: Mbona watumishi wako wamelichoma shamba langu moto?

32Abisalomu akamjibu Yoabu: Tazama, nalituma kwako kwamba: Njoo hapa, nikutume kwa mfalme kumwambia: Mbona nimekuja na kutoka Gesuri? Ingenifaa, nikae huko bado. Lakini sasa na nitokee usoni pake mfalme, kama ziko manza, nilizozikora, basi, na aniue.

33Yoabu alipokwenda kwa mfalme kumpasha hizi habari, akamwita Abisalomu; naye alipofika kwa mfalme akamwangukia mfalme na kujiangusha chini kifudifudi, ndipo, mfalme alipomnonea Abisalomu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania