The chat will start when you send the first message.
1Ahitofeli akamwambia Abisalomu: Na nichague watu 12000, niondoke kumfuata Dawidi upesi na usiku.[#Sh. 71:11.]
2Nitakapofika kwake, atakuwa amechoka, nayo mikono yake itakuwa imelegea; nikimstusha, akiwa hivyo, watu wote waliokuwa naye wakatimbia, nami nitampata mfalme, nimpige, akiwa peke yake.
3Kisha nitawarudisha watu wote kwako; hao watu wote, unaowatafuta wewe, watakaporudi, basi, huu ukoo wote mzima utakaa na kutengemana.
4Neno hili likanyoka machoni pake Abisalomu napo machoni pao wazee wote wa Waisiraeli.
5Lakini Abisalomu akasema: Mwite naye Mwarki Husai, tuyasikie nayo yaliyomo kinywani mwake![#2 Sam. 16:16.]
6Husai alipofika kwake Abisalomu, Abisalomu akamwambia kwamba: Ahitofeli amesema haya na haya; nasi tulifanye, alilolisema, au tuache? Sema wewe!
7Husai akamwambia Abisalomu: Mara hii shauri, Ahitofeli alilolitoa, si jema.
8Husai akasema: Wewe unamjua baba yako na watu wake, ya kuwa wao ndio mafundi wa vita wenye ukali rohoni mwao kama chui mke aliyenyang'anywa watoto wake, naye baba yako ni mtu wa vita, hatalala usiku kwa watu wake.
9Tazama, sasa yeye amekwisha kujificha katika shimo moja au penginepo palipo hivyo; lakini itakapokuwa, mwanzoni watu wa kwetu wauawe kwa kupigana nao, kila atakayevisikia atasema: Watu wanaomfuata Abisalomu wameshindwa katika mapigano.
10Ndipo, hata mwenye nguvu aliye mwenye moyo kama wa simba atakapoyeyuka kabisa, kwani Waisiraeli wote wanajua, ya kuwa baba yako ni fundi wa vita, nao watu waliokuwa naye ni wenye nguvu.
11Kwa hiyo shauri langu ni hili: Kwako na wakusanyike Waisiraeli wote toka Dani mpaka Beri-Seba, wawe wengi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari, kisha mwenyewe nenda nao vitani!
12Kisha tutamshambulia mahali pamoja; atakapoonekana, tumwangukie, kama umande unavyoiangukia nchi, tusisaze kwake hata mtu mmoja miongoni mwao wote waliokuwa naye!
13Kama atakimbilia mjini, Waisiraeli wote na waupeleke mji huo kamba, tuufunge, tuuvute na kuukokota mpaka mtoni, pasionekane pake tena hata kijiwe kimoja tu.
14Ndipo, Abisalomu na watu wote wa Waisiraeli waliposema: Shauri la Mwarki Husai ni jema kuliko shauri la Ahitofeli. Lakini alikuwa Bwana aliyeagiza kulitengua shauri jema la Ahitofeli, kusudi Bwana ampatie Abisalomu mabaya.[#2 Sam. 15:31,34.]
15Kisha Husai akawaambia watambikaji Sadoki na Abiatari: Ahitofeli amempa Abisalomu na wazee wa Waisiraeli mashauri haya na haya, lakini mimi nimewapa shauri hili.
16Sasa tumeni upesi kumpasha Dawidi habari za kwamba: Usilale usiku huu penye mbuga za nyikani, sharti uvuke mtoni, mfalme asimezwe na mabaya pamoja na watu wote waliokuwa naye.
17Yonatani na Ahimasi walikuwa wakikaa penye Chemchemi ya Wafua nguo; kwa hiyo kijakazi mmoja akaenda kuwapasha habari, nao wakaenda kumpasha mfalme Dawidi hizo habari. Ilikuwa hivyo, watu wasipate kuwaona wakiingia mjini.[#1 Fal. 1:9.]
18Lakini kijana aliwaona, naye akampasha Abisalomu habari. Nao wote wawili wakaenda na kupiga mbio, wakaingia nyumbani mwa mtu mle Bahurimu, naye alikuwa na kisima uani pake; ndimo, walimoshukia.
19Kisha mwanamke akachukua blanketi, akalitanda juu ya kisima hicho, akaanika humo ngano zilizotwangwa, lisijulikane neno lo lote.
20Watumishi wa Abisalomu walipofika nyumbani kwa huyu mwanamke na kumwuliza: Ahimasi na Yonatani wako wapi? huyu mwanamke akwaambia: Wamekwenda kukivuka kile kijito. Basi, walipowatafuta pasipo kuwaona, wakarudi Yerusalemu.
21Hao walipokwisha kwenda, wale wakatoka kisimani, wakaenda kumpasha mfalme Dawidi habari, wakamwambia Dawidi: Ondokeni, mvuke upesi mtoni! Kwani haya ndiyo mashauri, Ahitofeli aliyoyatoa kwa ajili yenu.
22Ndipo, Dawidi alipoondoka pamoja na watu wote waliokuwa naye, wakauvuka Yordani. Mapema yalipopambazuka, hakusalia hata mmoja asiyeuvuka Yordani.
23Ahitofeli alipoona, ya kuwa shauri lake halikufanywa, akamtandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mjini kwake, akayatengeneza mambo ya nyumbani, kisha akajinyonga, akafa, akazikwa kaburini mwa baba yake.[#Mat. 27:5.]
24Dawidi alipofika Mahanaimu, ndipo, Abisalomu alipouvuka Yordani, yeye na watu wote wa Waisiraeli pamoja naye.
25Naye Abisalomu alimweka Amasa kuwa mkuu wa vikosi mahali pake Yoabu; Amasa alikuwa mwana wa mtu aitwaye Itira wa Isiraeli; ndiye aliyeingia kale kwa Abigaili, binti Nahasi, umbu la Seruya aliyekuwa mama yake Yoabu.[#2 Sam. 19:13.]
26Waisiraeli na Abisalomu wakapiga makambi katika nchi ya Gileadi.
27Ikawa, Dawidi alipoingia Mahanaimu, ndipo, Sobi, mwana wa Nahasi wa Raba wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-Debari, na Mgileadi Barzilai wa Roglimu,[#2 Sam. 9:4; 1 Fal. 2:7.]
28walipoleta vitanda na mabakuli na vyombo vya udongo na ngano na mawele na unga na bisi na kunde na mbaazi na bisi za mchele,
29na asali na siagi na mbuzi na kondoo na maziwa mabivu ya ng'ombe, wakampelekea Dawidi na watu waliokuwa naye, wayale, kwani walisema: Watu hawa wana njaa, tena wamechoka kwa kupatwa na kiu za nyikani.[#2 Sam. 16:2.]