The chat will start when you send the first message.
1Katika siku za Dawidi kulikuwa na njaa mwaka kwa mwaka, miaka mitatu; naye Dawidi alipoutafuta uso wa Bwana, Bwana akasema: Ziko manza za damu, Sauli nao wa mlango wake walizozikora walipowaua watu wa Gibeoni.
2Ndipo, mfalme alipowaita Wagibeoni kusema nao; nao Wagibeoni hawakuwa wana wa Isiraeli, ila walikuwa masao yao Waamori, nao wana wa Isiraeli walikuwa wamefanya maagano nao na kuapa, lakini Sauli alitaka kuwaua kwa kuona wivu kwa ajili ya wana wa Isiraeli na wa Yuda.[#Yos. 9:15,19.]
3Ndipo, Dawidi alipowauliza Wagibeoni: Niwafanyizie nini? Tena yale makosa niyalipe namna gani, mpate kuwabariki walio fungu lake Bwana?
4Wagibeoni wakamwambia: Sisi hatutaki fedha wala dhahabu kwake Sauli, wala kwao walio wa mlango wake, tena haitupasi kuua watu wa kwao Waisiraeli. Alipouliza tena: Mwasemaje? Niwafanyizie nini?
5wakamwambia mfalme: Yule mtu aliyetumaliza kwa kutaka kutuangamiza kabisa, tusikae tena katika mipaka yote ya Waisiraeli,
6basi, na tupewe wanawe saba, tuwanyonge machoni pa Bwana kule Gibea kwa Sauli aliyekuwa mteule wa Bwana. Mfalme akawaambia: Mimi nitawapa.[#4 Mose 25:4.]
7Mfalme akamhurumia Mefiboseti, mwana wa Yonatani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo, alichokiapa na kumtaja Bwana, awe shahidi wao, yeye Dawidi naye Yonatani, mwana wa Sauli.[#1 Sam. 20:15-17.]
8Kwa hiyo mfalme akachukua wana wawili wa Risipa, binti Aya, aliomzalia Sauli, ndio Armoni na Mefiboseti, na wana watano wa Mikali, binti Sauli aliomzalia Adirieli, mwana wa Barzilai wa Mehola.[#1 Sam. 18:19; 2 Sam. 3:7.]
9Akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawanyonga mlimani juu machoni pa Bwana; nao wote saba wakauawa pamoja; walipouawa, ni siku za kwanza za mavuno, watu walipoanza kuvuna mawele.
10Kisha Risipa, binti Aya, akachukua gunia, akalitandika la kulalia mwambani juu tangu hapo, watu walipoanza kuvuna, mpaka mvua zitokazo mbinguni zikawanyeshea wale wafu, hakuacha ndege wa angani kuwakalia mchana, wala nyama wa porini kuwafikia usiku.
11Dawidi alipopashwa habari za mambo hayo, Risipa, binti Aya, suria yake Sauli, aliyoyafanya,
12Dawidi akaenda akaichukua mifupa ya Sauli nayo mifupa ya mwanawe Yonatani kwa wenyeji wa Yabesi wa Gileadi walioiiba uwanjani kwa Beti-Sani; ndiko, Wafilisti walikoitungika siku hiyo, Wafilisti walipomwua Sauli huko Gilboa.[#1 Sam. 31:12.]
13Alipoichukua huko mifupa ya Sauli na mifupa ya mwanawe Yonatani, wakaikusanya nayo mifupa yao hao walionyongwa,
14wakaizika mifupa ya Sauli nayo ya mwanawe Yonatani katika nchi ya Benyamini kule Sela kaburini kwa baba yake Kisi. Walipokwisha kuyafanya yote, mfalme aliyoyaagiza, baadaye Mungu akasikia alipoombwa kwa ajili ya nchi hiyo.[#2 Sam. 24:25.]
15Baadaye Wafilisti walipokuja tena kupigana na Waisiraeli, Dawidi akashuka pamoja na watumishi wake. Walipopigana na Wafilisti, Dawidi akachoka.
16Ndipo, alipotokea Isibi-Benobu aliyekuwa mmoja wao yale Majitu marefu; huyu alikuwa na mkuki wenye ncha ya shaba, nayo ilipopimwa, uzito wake ulikuwa sekeli 300, ndio nusu ya frasila; naye alikuwa amejifunga mata mapya, akataka kumwua Dawidi.
17Ndipo, Abisai, mwana wa Seruya, alipomsaidia na kumpiga yule Mfilisti, hata akafa. Hapo ndipo, watumishi wa Dawidi walipomwapia kwamba: Wewe hutatoka tena pamoja na sisi kwenda vitani, usiizime taa ya waisiraeli![#2 Sam. 23:18.]
(18-22: 1 Mambo 20:4-8.)18Hayo yalipokwisha yakawa mapigano mengine nao Wafilisti kule Gobu; ndiko, Sibekai wa Husa alikomwua Safu aliyekuwa naye mmoja wao yale Majitu marefu.
19Kisha kule Gobu yakawa mapigano mengine na Wafilisti; ndiko, Elihanani wa Beti-Lehemu, mwana wa Yare-Orgimu, alikomwua Goliati wa Gati; huyu uti wa mkuki wake ulikuwa kama majiti ya wafuma nguo.[#1 Sam. 17:7.]
20Kisha yakawa mapigano tena kule Gati; huko kulikuwa na mtu mrefu sana, vidole vya mikono yake na vidole vya miguu yake vilikuwa sita sita, vyote pamoja ni 24, naye alikuwa amezaliwa kwao yale Majitu marefu.
21Alipowatukana Waisiraeli, Yonatani, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akamwua.[#1 Sam. 17:10.]
22Hawa wanne walizaliwa Gati kwao yale Majitu marefu, wakauawa kwa mikono ya Dawidi na kwa mikono ya watumishi wake.