The chat will start when you send the first message.
1Dawidi akamwambia Bwana maneno ya wimbo huu, Bwana alipomponya mikononi mwa adui zake wote, namo mikononi mwa Sauli.
(2-51: Sh. 18:3-51.)2Akasema:
Bwana ni ngome yangu na boma langu, tena mponya wangu;
3ni Mungu aliye mwamba wangu, kwa hiyo ninamjetea, ni ngao yangu na pembe yangu ya kunipatia wokovu, kisha ni kingo langu, nipate pa kukimbilia, ni mwokozi wangu aniokoaye, nisije kukorofishwa.
4Bwana atukuzwaye ndiye, ninayemwitia; ndipo, ninapookolewa mikononi mwao walio adui zangu.
5Kwani mafuriko ya maji yauayo yalikuwa yameniasamia, nayo majito yaangamizayo yalinistusha,
6kamba zivutiazo kuzimuni zilikuwa zimenizunguka, nayo mafungo yauayo yalikuwa mbele yangu.
7Hapo niliposongeka nalimwita Bwana, yeye aliye Mungu wangu nikamlalamikia, akaisikia sauti yangu Jumbani mwake, malamamiko yangu yakamwingia masikioni mwake.
8Nchi ikatukutika na kutetemeka, nayo misingi ya mbingu ikatikisika kwa kutukuswa, kwani aliitolea makali yake yenye moto.
9Moshi ukapanda puani mwake, moto ulao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yakamulikamulika mbele yake.
10Akatanda mbingu ya kushukiapo, mawingu meusi yakawa chini ya miguu yake.
11Akapanda gari, nalo likarushwa, akaonekana mabawani mwa upepo.
12Akatumia giza kuwa kao, limfunike pande zote, ndio mawingu yenye mvua kali na kimbunga.
13Kwa nguvu ya kumulika mbele yake yakawashwa makaa ya moto.
14Bwana akapiga ngurumo kule mbinguni, Alioko huko juu akaivumisha sauti yake.
15Alipopiga mishale, akawatawanya, ngurumo zilipozidi, wakapigwa bumbuazi.
16Ndipo, vilipoonekana vilindi vya baharini, nayo misingi ya nchi ikafunuliwa kwa nguvu ya makaripio yake yeye Bwana na kwa ukali wa pumzi ya pua yake.
17Akakunjua mkono toka juu, akanikamata, mle mlimo na maji mengi akanichopoa.
18Akaniponya mikononi mwa adui yangu mwenye nguvu namo mwao walionichukia kwa kuwa na uwezo kuliko mimi.
19Walikuwa wamenijia mbele ile siku, nilipokuwa nimeshindwa, lakini Bwana akanijia kuwa shikizo.
20Akanitoa kwao, akanikalisha palipo papana; ndivyo, alivyoniopoa kwa kupendezwa nami.
21Bwana alinipa yaupasayo wongofu wangu, akanipatia tena yaupasayo ung'avu wa mikono yangu.
22Kwani naliziangalia njia zake Bwana, nisifanye kilicho kiovu mbele yake Mungu wangu.
23Kwani maamuzi yake yote yako mbele yangu, nayo maongozi yake sikuacha kuyafuata.
24Nikawa wake pasipo kuonywa, nikajiangalia, nisimkosee.
25Bwana akanipatia tena yaupasayo wongofu wangu, kwa kuwa nilikuwa nimeng'aa machoni pake.
26Wewe humwia mpole aliye mpole, naye aliye mkweli wote nawe humwia mkweli wote.
27Wewe humwia mng'avu aliye mng'avu, lakini aliye mpotovu nawe humpotokea.
28Walio wanyonge huwaokoa, lakini macho yako huwapingia wajivunao, uwanyenyekeze.
29Kwani wewe, Bwana, u taa yangu, naye Bwana huliangaza nalo giza langu.
30Kwani nitashambulia vikosi vizima kwa nguvu yako, kwa nguvu ya Mungu wangu narukia napo ukutani.
31Njia yake Mungu haipindiki, Neno lake Bwana limeng'azwa, yeye ni ngao yao wote wamkimbiliao.
32Kwani yuko nani aliye Mungu, asipokuwa Bwana?
Tena yuko nani aliye mwamba, asipokuwa Mungu wetu?
33Mungu ni ngome yangu yenye nguvu, njia yangu huifanya po pote, iwe imenyoka kabisa.
34Hunipatia miguu ikimbiayo kama ya kulungu, anisimamishe kwangu vilimani juu.
35Huifundisha mikono yangu kupiga vita, mpaka mikono yangu iweze kupinda hata uta wa shaba.
36Hunipa ngao ya kuniokoa, napo hapo, unaponinyenyekeza, hunikuza.
37Huipanulia miguu yangu, ipate pa kupitia, viwiko vya miguu yangu visiteleze.
38Na niwakimbize adui zangu, mpaka niwaangamize; sitarudi nisipokwisha kuwamaliza.
39Nitawamaliza na kuwaponda, wasiinuke tena, sharti waanguke miguuni pangu.
40Hunivika nguvu ya kupiga vita, huwalaza chini yangu wao waniinukiao.
41Hunipa adui zangu, niwaone migongo, nipate kuwanyamazisha wachukivu wangu.
42Hakuna mwokozi, wanapolalamika, wanapomwitia Bwana, hawaitikii.
43Nitawaponda, mpaka wabunguke kama mavumbi ya nchi, nikiisha kuwaseta, niwazoe kama mataka viwanjani.
44Kwenye magomvi yao walio ukoo wangu ulinitoa, ukaniangalia, nipate kuwa kichwa chao wao wamizimu, watu, ambao nilikuwa siwajui, wanitumikie.
45Hao watokao mbali hunipongeza, masikio yao yanaponisikia, hunitii.
46Hao watokao mbali walikuwa wamenyauka walipotoka mabomani kwao na kutetemeka.
47Bwana Mwenye uzima ni mwamba wangu upasao kusifiwa, yeye Mungu wa mwamba wangu aliyeniokoa sharti atukuke!
48Mungu ndiye aliyenipatia malipizi na kushurutisha makabila ya watu, wanitii,
49Ndiye aliyenitoa mikononi mwao walio adui zangu, kwao waniinukiao ukaniweka kuwa mkuu wao, kwao waliozidi kunikorofisha ukaniponya.
50Kwa hiyo nitakushukuru, Bwana, kwenye wamizimu, nalo Jina lako nitaliimbia.
51Mfalme wake alimpatia wokovu mwingi, aliyempaka mafuta humfanyizia yenye upole; huyo ni Dawidi naye aliye uzao wake kale na kale.