The chat will start when you send the first message.
1Makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli tena, kwa hiyo akamhimiza Dawidi kuwaponza akimwambia: Wahesabu Waisiraeli na Wayuda![#2 Sam. 21:1.]
2Ndipo, mfalme alipomwambia Yoabu, mkuu wa vikosi aliyekuwa naye: Zunguka katika mashina yote ya Waisiraeli toka Dani mpaka Beri-Seba, mwahesabu watu, nipate kuzijua hesabu za watu.
3Yoabu akamwambia mfalme: Bwana Mungu wako na aendelee kuwaongeza watu vivyo hivyo mara mia, naye bwana wangu mfalme na ayaone kwa macho yake! Lakini neno hilo bwana wangu mfalme analitakia nini?
4Lakini neno la mfalme likapata nguvu, asimsikie Yoabu wala wakuu wa vikosi; ndipo, Yoabu alipotoka na wakuu wa vikosi machoni pa mfalme kwenda kuwahesabu watu wa Waisiraeli.
5Walipokwisha kuuvuka Yordani wakapiga kambi kule Aroeri kuumeni kwa mji ulioko katikati ya Bonde la Gadi kuelekea Yazeri.
6Kisha wakafika Gileadi na nchi ya Tatimu-Hodisi, kisha wakafika Dani-Yani, wakazunguka kwenda Sidoni.
7Kisha wakafika katika boma la Tiro, hata miji yote ya Wahiti na ya Wakaanani wakaiingia, kisha wakatoka kwenda kusini kuingia Yuda mpaka Beri-Seba.
8Walipokwisha kuzunguka katika nchi zote, wakafika Yerusalemu, miezi 9 na siku 20 zilipokwisha pita.[#Yos. 18:9.]
9Ndipo, Yoabu alipompa mfalme jumla ya hesabu za watu: Waisiraeli wenye nguvu wanaoweza kushika panga walikuwa watu 800000, nao Wayuda watu 500000.
10Dawidi alipokwisha kuwahesabu watu, moyo ukampiga; ndipo, Dawidi alipomwambia Bwana: Nimekosa sana kwa kulifanya hilo. Sasa Bwana, umwondolee mtumishi wako hizo manza, nilizozikora! Kwani nimefanya kisichopasa kabisa.
11Dawidi alipoamka kesho yake, neno la Bwana likamjia mfumbuaji Gadi aliyekuwa mchunguzaji wa Dawidi, kwamba:
12Nenda kumwambia Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mimi ninakuwekea mambo matatu, ndimo uchague moja lao, nikufanyizie.
13Gadi akaja kwa Dawidi, akampasha hiyo habari na kumwuliza: Ikujie katika nchi yako miaka saba ya njaa? Au ukimbizwe miezi mitatu nao wakusongao, wakikufuata upesiupesi? Au uwe siku tatu katika nchi yako ugonjwa mbaya uuao? Sasa yawaze moyoni, uone nitakayomjibu aliyenituma.[#Yer. 24:10; 29:17; Ez. 6:12.]
14Dawidi akamwambia Gadi: Nimesongeka sana, lakini na nijitupe mkononi mwake Bwana, kwani huruma zake ni nyingi, nisijitupe mikononi mwa watu.
15Ndipo, Bwana alipowauguza Waisiraeli ugonjwa mbaya uuao tangu asubuhi, mpaka utimie muda, aliouweka. Toka Dani mpaka Beri-Seba wakafa kwao walio wa ukoo huo watu 70000.
16Malaika alipoukunjua mkono wake kuuangamiza Yerusalemu, Bwana akageuza moyo kwa ajili ya huo ubaya, akamwambia yule malaika aliyewaangamiza watu: Sasa inatosha, ulegeze mkono wako! Naye yule malaika wa Bwana alikuwa penye kupuria ngano pa Myebusi Arauna.
17Dawidi alipomwona yule malaika, jinsi alivyowapiga watu, akamwambia Bwana kwamba: Tazama, mimi nimekosa, mimi nimekora manza; lakini hawa kondoo wamefanya nini? Kwa hiyo mkono wako na unipige mimi na mlango wa baba yangu.[#4 Mose 16:22.]
18Siku hiyo Gadi akaja kwake Dawidi, akamwambia: Mtengenezee Bwana pa kutambikia penye kupuria ngano pa Myebusi Arauna!
19Kwa hilo neno la Gadi Dawidi akapanda, kama Bwana alivyoagiza.
20Arauna alipochungulia akamwona mfalme na watumishi wake, wakipanda kuja kwake; ndipo, Arauna alipotoka, akamwangukia mfalme usoni pake hapo chini.
21Kisha Arauna akauliza: Ni kwa sababu gani, bwana wangu mfalme akija kwa mtumishi wake? Dawidi akamwambia: Ninataka kununua kwako hapa pako pa kupuria ngano, nijenge pa kumtambikia Bwana, huku kuuawa kwa watu kukomeshwe.
22Arauna akamwambia Dawidi: Bwana wangu mfalme na apachukue tu, atambike, kama yalivyo mema machoni pake. Tazama, nakupa hawa ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nayo haya magari na vyombo vya ng'ombe nakupa kuwa kuni.
23Haya yote, mfalme, Arauna anampa mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme: Bwana Mungu wako na apendezwe na wewe!
24Lakini mfalme akamwambia Arauna: Sivyo, ila nitapanunua kabisa kwako na kulipa kilicho kiasi chake; sitamtolea Bwana Mungu wangu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nisizozilipa. Kisha Dawidi akapanunua hapo pa kupuria pamoja na ng'ombe kwa fedha 50.
25Kisha Dawidi akamjengea Bwana hapo mahali pa kumtambikia, akamtolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vipaji vya tambiko vya kumshukuru. Ndipo, Bwana aliposikia akiombwa kwa ajili ya nchi hiyo, nako kuuawa kwao Waisiraeli kukakomeshwa.[#2 Sam. 21:14.]