The chat will start when you send the first message.
1Vita vya kupigana kwao na mlango wa Sauli nao wa mlango wa Dawidi vikawa vya siku nyingi, lakini Dawidi akaendelea kupata nguvu, nao wa mlango wa Sauli wakaendelea kuwa wanyonge.[#2 Sam. 5:10.]
2Naye Dawidi akazaa wana huko Heburoni: mwanawe wa kwanza alikuwa Amunoni wa Ahinoamu wa Izireeli.[#1 Mambo 3:1; 2 Sam. 13:1.]
3Naye wa pili alikuwa Kilabu wa Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli, naye wa tatu alikuwa Abisalomu, mwana wa Maka, binti Talmai, mfalme wa Gesuri.
4Naye wa nne alikuwa Adonia, mwana wa Hagiti, naye wa tano alikuwa Sefatia, mwana wa Abitali.[#1 Fal. 1:5.]
5Naye wa sita alikuwa Itiramu, mwana wa Egla, mkewe Dawidi. Hawa ndio waliozaliwa kwake Dawidi huko Heburoni.
6Ikawa hapo, vita vya kupigana kwao wa mlango wa Sauli nao wa mlango wa Dawidi vilipokuwa, ndipo, Abineri alipoendelea kupata nguvu kwao wa mlango wa Sauli.
7Sauli alikuwa na suria, jina lake Risipa, binti Aya. Naye Isiboseti akamwuliza Abineri: Mbona umeingia kwake suria ya baba yangu?[#2 Sam. 21:8.]
8Ndipo, Abineri alipokasirika sana kwa ajili ya hayo maneno ya Isiboseti, akasema: Je? Mimi ni kichwa cha mbwa wa Kiyuda, kwa kuwa nimewafanyizia matendo mema walio wa mlango wa Sauli na ndugu zake na rafiki zake mpaka siku hii ya leo? Wewe nawe sikukutoa mkononi mwake Dawidi? Nawe unanisingiziaje leo kuwa mwenye manza kwa kukosa na yule mwanamke?
9Basi, Mungu na amfanyizie Abineri hivi na hivi, nisipomfanyizia Dawidi yaleyale, Bwana aliyoapa kumfanyizia!
10Nitauondoa ufalme kwao wa mlango wa Sauli, nikisimamishe kiti cha kifalme cha Dawidi, awatawale Waisiraeli na Wayuda toka Dani mpaka Beri-Seba.
11Naye hakuweza tena kumjibu Abineri hata neno moja kwa kumwogopa.
12Papo hapo Abineri akatuma wajumbe kwake Dawidi kwamba: Nchi ni ya nani? Haya! Fanya agano lako na mimi! Ndipo, mkono wangu utakapokusaidia kuwageuza Waisiraeli wote, wakufuate.
13Naye akasema: Basi, mimi nitafanya agano na wewe, lakini liko neno moja, ninalolitaka kwako, ni hili: Hutauona uso wangu, usipomleta kwanza Mikali, binti Sauli. Kisha utakuja kuuona uso wangu.
14Dawidi akatuma wajumbe kwake Isiboseti, mwana wa Sauli, kumwambia: Nipe mke wangu Mikali niliyempata, awe mke wangu kwa kutoa magovi 100 ya Wafilisti.[#1 Sam. 18:25-27.]
15Ndipo, Isiboseti alipotuma kumchukua kwa mumewe Paltieli, mwana wa Laisi.[#1 Sam. 25:44.]
16Huyo mumewe akaenda naye akimsindikiza na kulia machozi mpaka Bahurimu; ndipo, Abineri alipomwambia: Nenda, urudi! Naye akarudi.
17Kisha Abineri akasema na wazee wa Waisiraeli kwamba: Tangu jana na juzi mlikuwa mkimtaka Dawidi, awe mfalme wenu.
18Sasa yafanyeni! Kwani Bwana amemwambia Dawidi kwamba: Kwa kuutumia mkono wa mtumishi wangu Dawidi nitawaokoa walio ukoo wangu wa Waisiraeli mikononi mwa Wafilisti namo mikononi mwa adui zao wote.
19Yayo hayo Abineri akayasema hata msikioni pao Wabenyamini. Kisha Abineri akaenda kusema masikioni pa Dawidi huko Heburoni yote yaliyokuwa mema machoni pao Waisiraeli, hata machoni pao wote walio wa mlango wa Benyamini.
20Abineri alipofika Heburoni kwake Dawidi pamoja na watu 20, Dawidi akamfanyizia karamu Abineri pamoja na wale watu waliokuwa naye.
21Ndipo, Abineri alipomwambia Dawidi: Naondoka, niende kuwakusanya Waisiraeli wote kwake bwana wangu mfalme, wafanye agano na wewe, uwe mfalme wao na kufanya yote, roho yako itakayoyatamani. Dawidi akampa Abineri ruhusa kwenda zake, naye akaenda na kutengemana.
22Mara watumishi wa Dawidi wakaja pamoja na Yoabu kutoka vitani, wakaleta vitu vingi, walivyoviteka; lakini Abineri alikuwa hayuko tena Heburoni kwake Dawidi, kwani alimpa ruhusa kwenda zake, naye alikuwa amekwenda na kutengemana.
23Yoabu na kikosi chote kilichokuwa naye walipofika, watu wakamsimulia Yoabu kwamba: Abineri, mwana wa Neri, amekuja kwa mfalme, naye akampa ruhusa, akaenda zake na kutengemana.
24Ndipo, Yoabu alipokuja kwa mfalme, akamwambia: Umefanya nini? Tazama, Abineri alipofika kwako, mbona umempa ruhusa, akapata kwenda zake?
25Humjui Abineri, mwana na Neri ya kuwa amekuja tu kukudanganya, apate kujua kutoka kwako na kuingia kwako na kuyajua yote, wewe unayoyafanya?
26Yoabu alipotoka kwa Dawidi, akatuma wajumbe, wamfuate Abineri, wamrudishe kwenye kisima cha Sira, lakini Dawidi hakuvijua.
27Abineri alipofika Heburoni tena, Yoabu akamchukua langoni katikati na kumpeleka kando, apate kusema naye kinjamanjama; huko akamchoma tumboni, afe kwa ajili ya damu ya ndugu yake Asaheli.[#1 Fal. 2:5; 2 Sam. 2:23.]
28Baadaye Dawidi alipoyasikia akasema: Mimi na ufalme wangu hatumo kale na kale katika damu ya Abineri, mwana wa Neri, naye Bwana anavijua.
29Sharti imrudie Yoabu kichwani pake nao wote walio wa mlango wa baba yake. Katika mlango wa Yoabu asikoseke aliye mwenye kisonono au mwenye ukoma au mwenye mikongojo makwapani au mwenye kuuawa na upanga au mkosefu wa chakula!
30Lakini Yoabu na ndugu yake Abisai walimwua Abineri, kwa kuwa alimwua ndugu yao Asaheli kule Gibeoni katika mapigano.
31Dawidi akamwambia Yoabu, nao watu wote waliokuwa naye: Yararueni mavazi yenu! Kisha vaeni magunia, mwombolezeeni Abineri mkimtangulia! Naye mfalme Dawidi akalifuata jeneza lake.
32Walipomzika Abineri kule Heburoni, mfalme akaipaza sauti yake na kulia kule kaburini kwake Abineri, nao watu wote wakalia.[#1 Sam. 30:4.]
33Mfalme akamwombolezea Abineri kwamba:
Je? Abineri amekufa kama mpumbavu?
34Mikono yako haikufungwa, wala miguu yako haikutiwa pingu! Kama mtu anavyoangushwa nao wenye maovu, ndivyo, ulivyoangushwa nawe wewe!
Ndipo, watu wote walipoendelea kumlilia.
35Watu wote walipokuja kumpa Dawidi chakula, mchana ungaliko, Dawidi akaapa kwamba: Mungu na anifanyizie hivi na kupita hivi, nikionja mkate au cho chote kingine kabla ya kuchwa kwa jua.
36Watu wote walipoyaona kuwa kweli, yakawa mema machoni pao, kama mengine yote, mfalme aliyoyafanya, yalivyokuwa mema machoni pa watu.
37Siku hiyo watu wote na Waisiraeli wote wakajua, ya kama hilo shauri la kumwua Abineri, mwana wa Neri, halikutoka kwake mfalme.
38Kisha mfalme akawaambia watumishi wake: Hamjui, ya kuwa siku hii ya leo kwao Waisiraeli ameanguka mkuu mwenye ukubwa wa kweli?[#1 Sam. 26:15.]
39Mimi leo ni mnyonge bado, ijapo nimepakwa mafuta, niwe mfalme; lakini hawa wana wa Seruya ni wakali kuliko mimi. Bwana na amlipishe aliyeufanya ubaya huo kwa hivyo, ubaya wake ulivyo.