2 Samweli 4

2 Samweli 4

Isiboseti anauawa.

1Isiboseti, mwana wa Sauli, aliposikia, ya kuwa Abineri amekufa huko Heburoni, mikono yake ikamlegea, nao Waisiraeli wote wakastushwa.

2Huyo mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili waliokuwa wakuu wa vikosi, mmoja jina lake Baana, wa pili jina lake Rekabu, wana wa Rimoni wa Beroti waliokuwa wana wa Benyamini, kwani nchi ya Beroti ilihesabiwa kuwa ya Benyamini.

3Nao Waberoti walikuwa wamekimbilia Gitaimu; ndiko, wanakokaa ugenini hata leo hivi.

4Yonatani, mwana wa Sauli, alikuwa na mtoto mume aliyelemaa miguu yote miwili; huyu alikuwa mwenye miaka mitano, ile habari ya kufa kwao Sauli na Yonatani ilipofika kutoka Izireeli; hapo mlezi wake akamchukua, akimbie naye. Ikawa, alipojihimiza kukimbia, yule mtoto akaanguka, akakipata hicho kilema cha miguu, nalo jina lake Mefiboseti.[#2 Sam. 9:3.]

5Wale wana wa Rimoni wa Beroti, Rekabu na Baana, wakaenda; napo, jua la mchana lilipokuwa kali, wakaingia nyumbani mwa Isiboseti, naye alikuwa amelala kupumzikia mchana.

6Nao wakaingia mpaka katikati ya nyumba wakichukua ngano; ndipo, walipomchoma tumboni, kisha Rekabu na ndugu yake Baana wakakimbia.

7Vilikuwa hivi: walipoingia nyumbani, yeye alikuwa amelala kitandani pake katika chumba cha kulalia; nao walipokwisha kumwua kwa kumchoma, wakamkata kichwa, wakakichukua kichwa chake, wakaenda zao na kushika njia ya jangwani usiku kucha.

8Hicho kichwa cha Isiboseti wakakipeleka Heburoni kwa Dawidi, wakamwambia mfalme: Hiki ni kichwa cha Isiboseti, mwana wa Sauli, aliyekuwa mchukivu wako, aliyeitaka roho yako. Siku hii ya leo Bwana amempatia bwana wangu malipizi kwake Sauli na kwa kizazi chake.

9Ndipo, Dawidi alimpomjibu Rekabu na ndugu yake Baana, wana wa Rimoni wa Beroti, akiwaambia: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyeikomboa roho yangu katika masongano yote,

10nilimkamata yule aliyeniletea habari ya kwamba: Tazama, Sauli amekufa! Naye alijiwazia kuwa mwenye habari njema, lakini nikamwua huko Siklagi kuwa mshahara, niliompa wa habari zake.[#2 Sam. 1:15.]

11Nanyi m wabaya zaidi wasiomcha Mungu mlipomwua mtu mwongofu nyumbani mwake, akiwa amelala kitandani pake. Sasa itakuwaje? Sitailipiza damu yake mikononi mwenu na kuwang'oa katika nchi?

12Kisha Dawidi akawaagiza vijana wake, wakawaua, kisha wakawakata mikono na miguu, wakawatungika penye ziwa la Heburoni. Nacho kichwa cha Isiboseti wakakichukua, wakakizika kaburini kwa Abineri kule Heburoni.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania