2 Samweli 6

2 Samweli 6

Dawidi analipeleka Sanduku la Agano Yerusalemu.

(1-11: 1 Mambo 13.)

1Dawidi akawakusanya tena wapiga vita wote waliochaguliwa kwao Waisiraeli, watu 30000.[#Yos. 15:9; 2 Mose 25:22.]

2Kisha Dawidi akaondoka, akaenda nao hao watu wote waliokuwa naye kwenda Bale wa Yuda kulichukua huko Sanduku la Mungu lililoitwa jina lake kwa Jina la Bwana Mwenye vikosi akaaye juu ya Makerubi.

3Wakalipandisha Sanduku la Mungu katika gari jipya wakilitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa kilimani juu; nao Uza na Ayo, wana wa Abinadabu, wakaliendesha hilo gari jipya.[#1 Sam. 7:1.]

4Walipokwisha kulitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa kilimani juu, wakalipeleka Sanduku la Mungu, Ayo akilitangulia Sanduku.

5Dawidi mwenyewe nao watu walio wa mlango wa Isiraeli wakalitangulia na kucheza mbele ya Bwana na kupiga vyombo vyote vya kuchezea vilivyotengenezwa kwa mivinje kama mazeze na mapango na patu na njuga na matoazi.

6Walipofika pake Nakoni pa kupuria, Uza akalipelekea Sanduku la Mungu mkono, alishike, kwa kuwa ng'ombe walijikwaa.

7Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Uza, naye Mungu akampiga huko kwa ajili ya hilo kosa, akafa papo hapo penye Sanduku la Mungu.[#4 Mose 4:15; 1 Sam. 6:19.]

8Hapo Dawidi akaingiwa na uchungu, ya kuwa Bwana amempiga Uza pigo kama hilo, wakapaita mahali pale Peresi-Uza (Pigo la Uza) mpaka siku hii ya leo.

9Siku hiyo Dawidi akashikwa na woga wa kumwogopa Bwana kwamba: Sanduku la Bwana litawezaje kufika kwangu?

10Kwa hiyo Dawidi hakutaka kuliingiza Sanduku la Bwana kwake mjini kwa Dawidi, Dawidi akashika njia nyingine, akaliweka nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati.

11Humo nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati Sanduku la Bwana likakaa miezi mitatu, naye Bwana akambariki Obedi-Edomu na mlango wake wote.

(12-16: 1 Mambo 15.)

12Mfalme Dawidi alipopashwa habari kwamba: Bwana ameubariki mlango wa Obedi-Edomu nayo yote yaliyo yake kwa ajili ya Sanduku la Mungu, Dawidi akaenda, akalitoa Sanduku la Mungu nyumbani mwa Obedi-Edomu, akalipandisha mjini kwa Dawidi kwa furaha.

13Ikawa, wao wachukuzi wa Sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng'ombe ya tambiko na ndama aliyenona.[#1 Fal. 8:5.]

14Dawidi akawa akicheza kwa nguvu zote mbele ya Bwana, naye Dawidi alikuwa amevaa kisibau cheupe cha ukonge.

15Ndivyo, Dawidi na mlango wote wa Waisiraeli walivyolipandisha Sanduku la Bwana kwa kushangilia na kupiga mabaragumu.

16Ikawa, Sanduku la Bwana lilipoingia mjini kwa Dawidi, Mikali, binti Sauli, alichungulia dirishani; naye alipomwona mfalme Dawidi, alivyorukaruka na kuchezacheza mbele ya Bwana, ndipo, alipombeza moyoni mwake.

(17-19: 1 Mambo 16.)

17Walipokwisha kuliingiza Sanduku la Bwana wakaliweka mahali pake katikati ya lile hema, Dawidi alilolipigia. Kisha Dawidi akamtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kumshukuru.

18Dawidi alipokwisha kuzitoa hizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani akawabariki watu katika Jina la Bwana Mwenye vikosi.[#1 Fal. 8:55.]

19Kisha akawagawia watu wote wa huo mkutano wote wa Waisiraeli, waume kwa wake, kila mtu kipande kimoja cha mkate na kipande kimoja cha nyama na andazi moja la zabibu, kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake.

20Dawidi naye aliporudi kuwabariki walio wa mlango wake, Mikali, binti Sauli, akamwendea Dawidi njiani, akasema: Kweli leo mfalme wa Waisiraeli amejitukuza alipojivua nguo machoni pa vijakazi wa watumishi wake, kama mmoja wao walio wa ovyoovyo tu anavyojivika uchi.

21Lakini Dawidi akamwambia Mikali: Bwana ndiye aliyenichagua na kumwacha baba yako na mlango wake wote, aliponiagiza mimi kuwa mkuu wao walio ukoo wake Bwana nao wao Waisiraeli, naye yeye Bwana ndiye, ambaye ninataka kucheza mbele yake.[#2 Sam. 5:2.]

22Tena ninataka kujipunguza kupapita hapo pa leo, niwe mnyenyekevu machoni pangu mwenyewe; ndivyo, nitakavyojipatia utukufu kwao vijakazi, uliowasema.

23Lakini Mikali, binti Sauli, hakuwa na mwana mpaka siku hiyo, alipokufa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania