The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, mfalme alipokaa nyumbani mwake, kwa kuwa Bwana alikuwa amemtuliza akiwanyamazisha adui zake zote waliomzunguka,
2ndipo, mfalme alipomwambia mfumbuaji Natani: Tazama, mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa miangati, lakini Sanduku la Mungu linakaa katika mapazia tu.[#Sh. 132.]
3Natani akamwambia mfalme: Yote yaliyomo moyoni mwako nenda, uyafanye! Kwani Bwana yuko pamoja na wewe.
4Lakini usiku uleule neno la Bwana likamjia Natani kwamba:
5Nenda, umwambie mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe unijengee nyumba, nikae?[#1 Fal. 5:3; 1 Mambo 22:8.]
6Kwani sikukaa nyumbani tangu siku ile, nilipowatoa wana wa Isiraeli huko Misri nikiwaleta huku, mpaka siku hii ya leo, nikawa nikienda na kukaa katika hema lililokuwa Kao langu.[#1 Fal. 8:16,27; Yes. 66:1.]
7Je? Hapo pote, nilipokwenda pamoja na wana wote wa Isiraeli, nilimwambia hata mmoja wao wa mashina ya Waisiraeli, niliowaagiza kuwachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, na kumwuliza neno la kwamba: Mbona hamnijengei nyumba ya miangati?
8Kwa hiyo umwambie sasa mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mimi nilikuchukua malishoni, ulipowafuata kondoo, uwe mwenye kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli.[#1 Sam. 16:11-13.]
9Nikawa pamoja na wewe po pote, ulipokwenda, nikawaangamiza adui zako wote mbele yako; nitakupatia jina kubwa lililo sawa na majina ya wakubwa walioko huku nchini.
10Nao walio ukoo wangu wa Waisiraeli nitawapatia mahali, nitakapowapanda, wapate kukaa hapo pasipo kuhangaika tena, wala watu waovu wasiwakorofishe tena kama huko kwanza
11tangu siku zile, nilipowaagiza waamuzi, wawatawale walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Lakini wewe nitakupa kutulia nikiwanyamazisha adui zako wote, nawe wewe Bwana anakupasha habari, ya kuwa yeye Bwana atakutengenezea nyumba.
12Kwani siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako, ndipo, nitakapoinua nyuma yako mzao wako atakayetoka mwilini mwako, niusimike ufalme wake.[#1 Fal. 8:20; Yes. 9:7.]
13Yeye ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba, nami nitakisimamisha kiti cha ufalme wake, kipate kuwapo kale na kale.[#1 Fal. 5:5; 6:12; Sh. 89:4-5.]
14Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; atakapofanya kiovu, nitamchapa kwa fimbo ya kiwatu na kwa mapigo yapasayo wana wa watu.[#Sh. 89:27; Luk. 1:32; Ebr. 1:5.]
15Lakini upole wangu hautaondoka kwake, kama nilivyouondoa kwake Sauli, nilipomwondoa usoni pako.[#1 Sam. 15:23,26.]
16Mlango wako na ufalme wako utakuwa umeshupaa kale na kale machoni pako, nacho kiti chako cha kifalme kitakuwa kimesimamishwa kale na kale.[#Sh. 72:17; Yes. 55:3.]
17*Natani akamwambia Dawidi haya maneno yote sawasawa, kama alivyoambiwa mwenyewe na kuonyeshwa.[#1 Mambo 17:5.]
18Kisha mfalme Dawidi akaingia pake Bwana, akakaa hapo akisema: Bwana Mungu, mimi ni nani? nao mlango wangu ni nini, ukinileta, nifike hapa?[#1 Mose 32:10.]
19Lakini hayo yakawa madogo machoni pako, Bwana Mungu, kwa hiyo umeyasema yatakayoujia mlango wa mtumishi wako katika siku zilizo mbali bado, hayo nayo umeyasema kimtu, Bwana Mungu.
20Dawidi akuambie nini tena? Maana wewe unamjua mtumishi wako, Bwana Mungu.
21Kwa ajili ya Neno lako na kwa mapenzi ya moyo wako umeyafanya hayo makubwa yote, umjulishe mtumishi wako.
22Kwa hiyo u mkubwa, Bwana Mungu, kwani hakuna anayefanana na wewe, hakuna Mungu, asipokuwa wewe, kwa hayo yote, tuliyoyasikia kwa masikio yetu.
23Tena liko taifa moja tu huku nchini linalofanana na ukoo wako wa Waisiraeli? Hao ndio, Mungu aliokwenda kuwakomboa, wawe ukoo wake, ajipatie Jina kwa kufanya kwao katika nchi yako matendo makubwa yanayoogopesha, ulipofukuza wamizimu na miungu yao mbele yao walio ukoo wako, uliowakomboa, wawe wako, ulipowatoa huko Misri.[#5 Mose 4:7.]
24Ukajiwekea ukoo wako wa Waisiraeli kuwa ukoo wako kale na kale, wewe Bwana ukawa Mungu wao.
25Sasa, Bwana Mungu, neno hilo, ulilolisema la mtumishi wako na la mlango wake, lisimamishe kuwapo kale na kale ukifanya, kama ulivyosema!
26Ndivyo, Jina lako litakavyokuwa kubwa kale na kale kwamba: Bwana Mwenye vikosi ni Mungu wa Isiraeli, tena ndivyo, mlango wa mtumishi wako Dawidi utakavyokuwa wenye nguvu mbele yako.
27Kwani wewe Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, umelifunua sikio la mtumishi wako, asikie ya kwamba: Mimi nitakujengea nyumba. Kwa hiyo mtumishi wako amejipa moyo wa kukuomba maombo haya.[#Yes. 50:5.]
28Sasa Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu; kwa hiyo maneno yako yatatimia kweli, hayo mema, uliyomwambia mtumishi wako, yapate kuwa.
29Sasa na ikupendeze kuubariki mlango wa mtumishi wako, uwepo kale na kale usoni pako! Kwani wewe, Bwana Mungu, umeyasema; kwa hiyo mlango wa mtumishi wako utakuwa umebarikiwa kale na kale kwa kuipata mbaraka yako.*