2 Samweli 8

2 Samweli 8

Vita na mali za Dawidi.

(Taz. 1 Mambo 18.)

1Hayo yalipokwisha, Dawidi akawapiga Wafilisti, akawashinda; kisha Dawidi akaishika mwenyewe hatamu ya mji mkuu, isishikwe tena na Wafilisti.

2Nao Wamoabu akawapiga, akawapima kwa kamba akiwalaza chini, akapima hivyo: wa kamba mbili wakawa wa kuuawa, nao wote wa kamba moja wakawa wa kuachwa uzimani; nao Wamoabu wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo.

3Kisha Dawidi akampiga Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kuusimika tena ufalme wake huko kwenye jito la Furati.

4Dawidi akateka kwake wapanda farasi 1700 na askari waliokwenda kwa miguu 20000, nao farasi wote wa kuvuta magari Dawidi akawakata mishipa, akajisazia farasi wa magari mia tu.[#Yos. 11:9.]

5Washami Wa Damasko walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Dawidi akapiga kwao Washami watu 22000.

6Dawidi akaweka askari kwao Washami wa Damasko, hao Washami wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo, ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda po pote, alipokwenda.

7Dawidi akazichukua ngao za dhahabu, watumishi wa Hadadezeri walizokuwa nazo, akazipeleka Yerusalemu.

8Namo mle Beta na Berotai iliyokuwa miji ya Hadadezeri Dawidi akachukua shaba nyekundu nyingi mno.

9Toi, mfalme wa Hamati, aliposikia, ya kuwa Dawidi amevipiga vikosi vyote vya Hadadezeri,

10Toi akamtuma mwanawe Yoramu kwake mfalme Dawidi kumpongeza na kumbariki, kwa kuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda, kwani Toi na Hadadezeri walikuwa wakipigana vita, naye akampelekea mkononi mwake vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na vyombo vya shaba.

11Hivi navyo mfalme Dawidi akavitakasa kuwa mali za Bwana, kama alivyozitakasa nazo fedha na dhahabu, alizozichukua kwa mataifa yote, aliyoyashinda,

12kama kwao Washami na Wamoabu na wana wa Amoni na Wafilisti na Waamaleki, hata nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

13Dawidi aliporudi kwa kuwapiga Washami akajipatia jina kuu kwa kuua watu 18000 Bondeni kwa Chumvi.[#Sh. 60:2.]

14Kisha Dawidi akaweka askari kwa Waedomu, kwao Waedomu akaweka askari po pote, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Dawidi. Ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda po pote, alipokwenda.[#1 Mose 27:40.]

15Dawidi akawa mfalme wa Waisiraeli wote, naye Dawidi akawatengenezea watu wake wote mashauri yaliyokuwa sawa, maana yaliongoka.

16Naye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa vikosi, naye Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa.[#2 Sam. 20:23-26.]

17Naye Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiatari, walikuwa watambikaji, naye Seraya alikuwa mwandishi.

18Naye Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wao Wakreti na Wapuleti, nao wana wa Dawidi walikuwa watambikaji.[#1 Sam. 30:14; 2 Sam. 15:18; 1 Fal. 4:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania