2 Timoteo 3

2 Timoteo 3

Wapotevu wa siku za mwisho.

1Lakini yatambue haya: siku za mwisho patakuwa na siku ngumu.[#1 Tim. 4:1.]

2Kwani watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye choyo, wenye kujitutumua na kujikweza, wenye matusi, wasiwatii wazazi, wasishukuru, wasimche Mungu,

3wasiwapende wenzao, wasitake kupatanishwa na mtu kwa kupenda usengenyaji, wasijikataze lo lote, wasionyeke, wasipende mema yo yote,

4ila watakuwa wachongezi na wakorofi na wenye majivuno; kuzifuata tamaa za miili watakupenda kuliko kumfuata Mungu;[#Fil. 3:19.]

5watajitendekeza kuwa wenye kumcha Mungu, lakini nguvu yake huipingia. Walio hivyo uwaepuke![#Mat. 7:15,21; Tit. 1:16.]

6Kwani wenzao ndio wale wanaonyemelea nyumbani mwa watu, watongoze wanawake wanyonge waliolemewa na makosa, wakiongozwa na tamaa nyingi;[#Mat. 23:14; Tit. 1:11.]

7hao hufundishwa toka kale, lakini hapana, watakapoweza kuufikia utambuzi wa kweli.

8Kama Yane na Yambure waliombisha Mose, ndivyo, hata hao wanavyoyabisha yalio ya kweli; hufanana nao wenye wazimu, wakajulika kuwa wenye kumtegemea Mungu bure tu.[#2 Mose 7:11,22.]

9Lakini hawataendelea sana, kwani upumbavu wao utawatokea wote waziwazi, kama hata upumbavu wao wale ulivyojulika.

Nguvu ya Neno la Mungu.

10Lakini wewe umeufuata ufundisho wangu na mwenendo wangu na mawazo yangu na njia yangu ya kumtegemea Mungu na utulivu wangu na upendo wangu na uvumilivu wangu,

11hata mafukuzo na mateso yangu, niliyoyapata huko Antiokia na Ikonio na Listra. Nami niliyavumilia hayo mafukuzo yote, naye Bwana akaniokoa katika yote.[#Sh. 34:20; Tume. 13:50; 14:5,19.]

12Nao wote wanaotaka kuishi na kumcha Mungu kwa kuwa wake Kristo Yesu sharti wapate mafukuzo.[#Mat. 16:24; Tume. 14:22.]

13Lakini watu walio wabaya na wadanganyi wataendelea, wajifikishe palipo pabaya; hupoteza watu, tena hupotezwa wenyewe.[#1 Tim. 4:1.]

14*Lakini wewe ukae na kuyashika yale, uliyofundishwa, uliyoyatambua kwamba: Ndiyo ya kweli, maana unajua, waliokufundisha walivyo.[#2 Tim. 2:2.]

15Tena kwa sababu umeyajua Maandiko matakatifu tangu utoto wako, haya yanaweza kukuerevusha, uokoke kwa kumtegemea Kristo Yesu.[#Yoh. 5:39.]

16Kwani kila neno la Maandiko, mtu aliloambiwa na Mungu, linafaa, litufundishe, lituonyeshe ubaya wetu, liitulize mioyo yetu, lituonye, tupate wongofu;[#2 Petr. 1:19-21.]

17ndivyo, anavyotengenezewa mtu wa Kimungu ajikazaye kufanya kazi njema zo zote.*[#Mat. 5:48; 1 Tim. 6:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania