Matendo ya Mitume 14

Matendo ya Mitume 14

Ikonio.

1Ikawa, walipokusanyika huko Ikonio nyumbani mwa kuombea mwa Wayuda, wakawaambia maneno yayo hayo, hata Wayuda na Wagriki wengi mno wakaja kuyategemea.

2Lakini Wayuda waliokataa kutii wakaichokoza mioyo ya wamizimu na kuwawazisha maovu, wachukizwe na hao ndugu.[#Tume. 13:45.]

3Wakakaa huko siku nyingi wakitangaza waziwazi, walivyoshikamana na Bwana, naye akayashuhudia hayo maneno, waliyoyasema ya magawio yake akitokeza vielekezo na vioja vilivyofanyizwa na mikono yao.[#Tume. 19:11; Ebr. 2:4.]

4Watu waliokuwamo mle mjini wakakosana, wengine walikuwa upande wa Wayuda, wengine upande wa mitume.

5Lakini wamizimu na Wayuda pamoja na wakubwa wao walitaka kuwashambulia, wawakorofishe na kuwapiga mawe.[#Tume. 14:19; 2 Tim. 3:11.]

6Walipoyatambua wakakimbilia miji ya Likaonia na Listira na Derbe na mingine iliyoko kandokando.

7Wakakaa huko wakiipiga hiyo mbiu njema.[#Tume. 11:19-20.]

Kiwete katika Listira.

8Listira kulikuwa na mtu aliyekaa hawezi miguu; ni kiwete tangu hapo, alipotoka tumboni mwa mama yake, hakuweza kwenda kamwe.[#Tume. 3:2.]

9Huyu alimsikiliza Paulo, alipokuwa akisema. Naye alipomkazia macho, akamwona, ya kuwa anatazamia kuponywa,[#Mat. 9:28.]

10akamwambia kwa sauti kuu: Inuka, usimame kwa miguu yako, inyoke! Ndipo, alipoinuka na kuruka na kuzungukazunguka.

11Makundi ya watu walipoona, Paulo alilolifanya, wakapaza sauti wakisema kwa Kilikaonia: Miungu imegeuka kufanana na sisi watu, ikatushukia.[#Tume. 28:6.]

12Wakampa Barnaba jina lake Zeu na Paulo jina lake Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.

13Kisha mtambikaji wa nyumba ya Zeu iliyokuwa nje ya mji akaleta ng'ombe na vilemba vya maua malangoni, yeye na makundi ya watu wakataka kuwachinjia ng'ombe za tambiko.

14Lakini mitume Barnaba na Paulo walipoyasikia wakayararua mavazi yao, wakayarukia hayo makundi, wakapaza sauti

15wakisema: Waume, haya mnayafanyia nini? Hata sisi tu watu wenye kufa kama ninyi. Tunawapigia mbiu njema, mwiache miungu hii ya bure, mmgeukie Mungu Mwenye uzima aliyeziumba mbingu na nchi na bahari navyo vyote vilivyomo.[#Tume. 4:24; 10:26.]

16Siku zilizopita aliwaacha wamizimu wote, wazishike njia zao;[#Tume. 17:30.]

17lakini hakujitowesha kwenu, maana alifanya mema akiwapa mvua toka mbinguni na miaka ya mavuno mazuri, hivyo aliishibisha mioyo yenu vyakula na mashangilio.[#Sh. 147:8; Yer. 5:24.]

18Wakisema hivyo, ilisalia kidogo tu, wasiweze kuwazuia hao watu wengi, wasiwachinjie ng'ombe za tambiko.

Paulo anapigwa mawe.

19Kisha Wayuda wakaja huko toka Antiokia na Ikonio, wakachokoza makundi ya watu, wakampiga Paulo mawe, wakamtoa mjini na kumburura wakidhani, amekwisha kufa.[#2 Kor. 11:25; 2 Tim. 3:11.]

20Lakini wanafunzi walipomsimamia kwa kumzungukia, akainuka, akaingia mjini. Kesho yake akatoka pamoja na Barnaba kwenda Derbe.

21Ule mji nao wakaupigia hiyo mbiu njema, wakapata wanafunzi wengi; kisha wakarudi kwenda Listira na Ikonio na Antiokia.

22Wakaishupaza mioyo ya wanafunzi, wakawahimiza, wafulize kumtegemea Bwana, wakawaambia: Inatupasa kupatwa na maumivu mengi, tukiingia katika ufalme wa Mungu.[#Tume. 11:23; Rom. 5:3-5; 1 Tes. 3:3.]

23Kila mahali penye wateule wakawawekea wazee, wakawapeleka kwa Bwana, ambaye walianza kumtegemea, wakiwaombea pamoja na kufunga.[#Tume. 13:1-2.]

24Wakaikata nchi ya Pisidia, wakafika Pamfilia,

25wakalitangaza lile Neno mle Perge, wakatelemka kwenda Atalia.

26Huko wakajipakia chomboni kwenda Antiokia; ndiko, walikotoka kwa kutumwa, wenzao wakiwaombea, Mungu awaongoze kwa upole katika kazi ile, waliyokwisha kuitimiza.

27Walipofika wakawakusanya wateule, wakawasimulia yote, Mungu aliyoyafanya kwa kuwa nao, hata alivyowafungulia wamizimu mlango, nao wapate kumtegemea.[#1 Kor. 16:9.]

28Siku, walizokaa huko pamoja na wanafunzi, si chache.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania