Matendo ya Mitume 20

Matendo ya Mitume 20

Paulo katika Makedonia.

1Lile fujo lilipotulia, Paulo akatuma watu kuwaita wanafunzi, akawatuliza mioyo, akaagana nao, akaondoka kwenda Makedonia.

2Akapita pande zile akiwatuliza mioyo na kuwaambia maneno mengi, kisha akafidka Ugriki.

3Akakaa huko miezi mitatu. Alipotaka kuingia chomboni, aende Ushami, Wayuda walimlia njama. Kwa hiyo akapendezwa kurudi na kupita Makedonia.

4Waliofuatana naye mpaka Asia ni Sopatiro, mwana wa Puro wa Beroya, na Aristarko na Sekundo wa Tesalonike na Gayo wa Derbe na Timoteo; tena Tikiko na Tirofimo wa Asia.[#Tume. 17:10; 19:29.]

5Hao walitangulia, wakatungoja Tiroa.[#Tume. 16:8.]

6Siku za mikate isiyotiwa chachu zilipopita, nasi tukatweka, tukaondoka Filipi, tukawafikia huko Tiroa siku ya tano, tukaa huko siku saba.

Eutiko.

7Siku ya kwanza ya juma tulipokuwa tumekusanyikia kumegeana mkate, Paulo akasema nao; kwa sababu alitaka kuondoka kesho yake, akaendelea kusema mpaka usiku wa manane.[#Tume. 2:42,46; 1 Kor. 16:2.]

8Mkawa na taa nyingi katika chumba cha juu, tulimokuwa tumekusanyika.

9Mlikuwa na kijana, jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, akasinzia mno. Paulo alipofuliza kusema, akashindwa na usingizi, akaanguka toka dari ya tatu mpaka chini, akainuliwa amekufa.

10Lakini Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema: Msipige makelele! Kwani roho yake ingalimo mwake.[#1 Fal. 17:21.]

11Akapanda tena, akamega mkate, akala, akaongea mengi nao, mpaka kulipopambazuka. ndivyo, alivyotoka huko.

12Lakini yule kijana walimleta, yuko mzima, kwa hiyo mioyo yao ikawatulia kabisa.

13Lakini sisi tulitangulia kuingia chomboni, tukatweka kwenda Aso; ndiko, tulikotaka kumpakia Paulo. Kwani alikuwa ametuagiza hivyo; mwenyewe alitaka kufika huko kwa miguu.

14Naye alipokutana nasi huko Aso, tukampakia, tukafika Mitilene.

15Tukatweka huko, kesho yake tukaelekea Kio; kesho kutwa tukatia nanga Samo, tukakaa Tirogilio, mtondogoo tukafika Mileto.

16Kwani Paulo alitaka kupita Efeso kwa chombo, asipate kukawia katika Asia, maana alikwenda mbiombio, kwa sababu alitaka ikiwezekana, kuila sikukuu ya Pentekote huko Yerusalemu.[#Tume. 18:21.]

Paulo na wazee wa Efeso.

17*Lakini toka Mileto alituma mtu Efeso kuwaita wazee wa wateule.

18Hao walipofika kwake, akawaambia: Ninyi mnajua, nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ya kwanza, nilipofika Asia:[#Tume. 18:19; 19:10.]

19nimemtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, hata nilipoulizwa, hata nilipojaribiwa na Wayuda mara kwa mara, wakininyatia.[#Tume. 20:3.]

20Hakuna neno lenye kufaa, nililowanyika nikiacha kulitangaza, tena sikuacha kuwafundisha mkikusanyika au nikienda nyumba kwa nyumba.

21Kwa ushahidi wangu nimewahimiza Wayuda na Wagriki, wajute na kurudi kwake Mungu, tena wamtegemee Bwana wetu Yesu.

22Sasa tazameni, kwa hivyo, nilivyofungwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu, nisijue yatakayonipata huko.[#Tume. 19:21.]

23Naijua hii tu, ya kuwa Roho Mtakatifu hunishuhudia mijini mote, nifikamo, kwamba: Mapingu na maumivu yananingoja.[#Tume. 9:16; 21:4,11.]

24Lakini ninajiwazia kwamba: Si kitu, mwenyewe nikiangamia; lakini kilicho kitu, ni kuumaliza mwendo wangu na utumishi wangu, niliopewa na Bwana Yesu, niushuhudie Utume mwema wa gawio lake Mungu.[#Tume. 21:13.]

25Sasa tazameni, mimi ninajua, ya kuwa hamtauona tena uso wangu ninyi nyote, ambao nilipita kwao na kuutangaza ufalme.

26Kwa hiyo ninawaambia waziwazi siku hii ya leo kwamba: Ninyi nyote hakuna, ambaye ninawiwa naye damu ya mtu.[#Tume. 18:6; Ez. 3:17-19.]

27Kwani sikuacha kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.

28Jilindeni wenyewe na kikundi chote! Kwani Roho Mtakatifu amewaweka, mwe wakaguzi wao, mwachunge wateule wake Mungu, aliojichumia kwa kuitoa damu yake mwenyewe.[#1 Tim. 4:16; 1 Petr. 5:2-4.]

29Mimi najua: Nitakapokwisha kuondoka, wataingia chui wakali kwenu wasiowaonea huruma wao wa kikundi hiki.[#Mat. 7:15.]

30Tena miongoni mwenu wenyewe watainuka watu wakaofundisha mapotovu, wapate kuwavuta nao walio wanafunzi, wawaandamie.[#1 Yoh. 2:18.]

31Kwa hiyo kesheni na kukumbuka, ya kuwa miaka mitatu sikuacha usiku na mchana kumwonya kila mmoja kwa kutoa machozi!

32Sasa hivi ninawaweka mikononi mwake Mungu, awagawie Neno lake linaloweza kuwajenga na kuwapa fungu kwao wote waliotakaswa.

33Sikutaka fedha au dhahabu au mavazi ya mtu.[#1 Sam. 12:3; Mat. 10:8; 1 Kor. 9:12.]

34Mnatambua wenyewe: hii mikono yangu imetumika kunichumia yaliyotulisha mimi na wenzangu waliokuwa pamoja nami.[#Tume. 18:3; 1 Kor. 4:12; 1 Tes. 2:9; 4:11.]

35Kwangu mimi nimewaonyesha yote, ya kuwa imetupasa kusumbukia kazi vivyo hivyo, tupate kuwasaidia wanyonge, tukiyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyoyasema mwenyewe: Kumpa mtu huna upato kuliko kupewa.

36Alipokwisha kusema hivyo akapiga magoti pamoja nao wote, akaomba.[#Tume. 21:5.]

37Wote wakalia sana, wakamkumbatia Paulo lshingoni, wakamnonea.

38Lililowasikitisha zaidi ni neno lile, alilolisema, ya kuwa hawatamwona tena uso kwa uso. Kisha wakamsindikiza hata chomboni.*[#Tume. 20:25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania